HONGERA ULANGA COMMUNITY RESOURCE CENTRE

photos

Welcome to UCRC

About Me

Ulanga Community Resource Centre is a not-for-profit company limited by guarantee which was initiated with the aim of capacitating the resident peoples of Ulanga and Kilombero Districts and Tanzania in general to secure the right information and hold their duty bearers accountable in a bid to promote sustainable community development. UCRC as well aims at promoting educational activities in Ulanga District through facilitation of necessary educational resources in the area which include well equipped libraries and study centers. UCRC also works on land and natural resource rights for the marginalized rural people in Tanzania which also include sustainable use of such resources. It also provides legal aid and assistance to the poor, particularly women, children, the disabled and other disadvantaged groups in the society on different themes including land and gender.

Wednesday, October 31, 2012

WAFUGAJI WAVAMIZI, WAKULIMA WALIOINGIA HIFADHINI KUONDOKA KWA NGUVU

Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero.

SERIKALI Wilayani Kilombero imetangaza kwa Wafugaji wavamizi walioshauriwa kuondoka waanze kufanya hivyo kabla ya Oparesheni maalumu ya kuwaondoa kuanza Rasmi Mwisho wa Mwezi Oktoba.

Bwana Hassan Masala,Mkuu wa Wilaya ya Kilombero katika Tangazo alilolitoa amesema kuwa wale wote Wafugaji wenye mifugo mingi waliovamia maeneo yasiyoruhusiwa waondoke mapema kabla ya tarehe 30 Oktoba 2012 ambapo oparesheni maalum itaanza.
Ametanabaisha kuwa Wafugaji wavamizi ni wale walioingia kijijini bila ya kupokelewa na Serikali ya kijiji na Kuthibitishwa na Mkutano wa Kijiji huku pia kukiwa na kundi jingine la Wafugaji lenye Mifugo ambayo haijapigwa Chapa na kutambuliwa na Serikali kufuatana na eneo la Malisho lililotengwa kwa Kijiji husika.

Wataalamu wa Idara ya Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero wametenga maeneo ya Malisho kwa Kila Kijiji chenye Wafugaji huku eneo hilo likipimwa kwa idadi maalumu ya Mifugo inayotakiwa kuwepo kutokana na ukubwa wa eneo hilo.
Mbali ya Suala la Wafugaji wavamizi Mkuu wa Wilaya amewataka Wakulima waliovamia eneo la Hifadhi ambalo kisheria haliruhusiwi kufanyika shughuli za Kibinadamu  waondoke mara moja sanjari na Wafugaji wavamizi.

Serikali ilitangaza ifikapo Septemba 7 kuwa Mwisho wa kuondoa mifugo kwa Hiari Katika Bonde la Mto Kilombero lakini kutokana na shughulili za Kitaifa za Sensa na Mchakato wa kupata Katiba Mpya zoezi la kuwaondoa kwa nguvu likasogezwa mbele na kwa sasa limeandaliwa rasmi kuanza mmwisho wa Mwezi huu.

Madiwani upinzani wasusia kikao Kilombero


 Na Senior Libonge, Ulanga

MADIWANI wa kambi ya upinzani katika baraza la halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro jana walilazimika kutoka nje na kususia kikao cha baraza hilo kufutia hoja ya kutaka diwani wa mteule wa viti maalum kupitia tiketi  ya chama cha wananchi (CUF),Maricena Mchanga, kutupiliwa mbali na baraza hilo.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5.00 asubuhi muda mfupi mara baada ya mwenyekiti wa baraza hilo, Furaha Lilonge, kufungua kikao hicho na kutaka madiwani kupitisha agenda za kikao hicho na baada ya hapo hoja ya kupishwa kwa diwani huyo ilijitokeza.

Kujitokeza kwa hoja hiyo pia kulifuatia mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Isabera Chilumba, kusema kuwa katika agenda za hikao hicho kulisahaulika agenda zingine mbili za kuapishwa kwa diwani huyo na kupokea ujumbe kutoka tume ya utumishi wa umma ambao ulitaka kuzungumza na baraza hilo.

Hoja ya mkurugenzi huyo ilizua mabishano baina ya madiwani wa halmashauri hiyo huku upande wa madiwani kutoka chama tawala chama cha mapinduzi (CCM), wakitaka kanuni za uendeshaji wa kikao cha baraza zizingatiwe kwa madai kuwa kuapishwa kwa diwani huyo kulipaswa kufanyika kabla ya kufunguliwa kwa kikao hicho na kwamba kikao hicho kwa vile kilikwisha anza hakikuwa sahihi kutumika kumuapisha.

Kauli hiyo aliyotolewa na diwani wa wa kata ya Mawasiliano katika tarafa ya Mahenge, Mwanaidi Mkalimoto, na kupingwa vikali na kambi ya upinzani ikiongozwa na diwani wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Said Tilla, ambaye alitaka haki ya diwani huyo mteule izingatiwe.

Hata hivyo, malumbano hayo yalimlazimu mwanasheria wa halmashauri hiyo, Bahati Kikoti, kutoa ufafanuzi kuwa kanuni za wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), kuhusu uapishwaji wa madiwani zinaeleza kuwa diwani ataapishwa kabla ya kikao chake cha kwanza na kushauri kuwa bado agenda ya kuapishwa kwa diweani huyo ingeingizwa katika agenda za kikao hicho.

Licha ya kutoa ufafanuzi huo wa mwanasheria, lakini mwenyekiti alisimamia hojas yake kwa kusema kuwa agenda ya kuapishwa kwa diwani huyo mteule haitaingizwa miongoni mwa agenda hizo kutokana na kanuni za uendeshaji wa baraza hilo kwa madai kuwa kwa kuwa madiwani walikwisha pitisha agenda hizo agenda za ziada hazitaruhusiwa.

Hatua hiyo ya mwenyekiti wa halmashauri iliwalazimu madiwani tisa wa kambi ya upinzani kunyanyuka na kutoka nje wakipinga kuondolewa kwa hoja hiyo.

Diwani wa kata ya Lupiro (Chadema), Nassoro Mcharange ameiambia blog hii kuwa maamuzi yaliyotolewa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo hayakuwa sahihi kwa vile diwani mteule alifika katika baraza hilo kufutia barua ya halmashauri yenye kumbukumbu namba UDC/ADM/E.20/4/35 ikimtaka diwani huyo mteule kuhuzulia kikao hicho ili kuapishwa na kushiriki kikao.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Sofi katika tarafa ya Beatus Daud, kupitia tiketi ya TLP, alilalamikia maamuzi yanayotolewa na mwenyekiti huyo kwa mdai kuwa amekuwa akiegemea kwenye chama chake cha CCM.
Hata hivyo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo akijibu tuhuma hizo alisema kuwa uendeshaji wa baraza hilo amekuwa akiufanya kwa kuzingatia kanuni za uendeshaji baraza tofauti na madai yanayotolewa na madiwani wa kambi ya upinzani.

Akitoa ufafanuzi wa madiwani hao kususia kikao hicho na kutoka nje alisema kuwa yako makosa yaliyofanywa na halmsahuri hiyo juu ya uteuzi wa diwani mteule huyo kwa maelezo huwa chama cha CUF kinadiwani mmoja wa kuchaguliwa hivyo hakikuwa na sifa ya kuwa na diwani wa viti maalum.

Alidai kuwa chama cha Chadema na TLP vimekuwa na sifa hiyo kutokana na kuwa na madiwani watatu kila kimoja na CCM ilipata madiwani wanane wa viti maalum kwa kuwa na madiwani 24 wa kuchaguliwa na wabunge wawili na kwamba kwa sifa ya diwani watatu kukiwezesha chama kupata diwani wa viti maalum basi sifa hiyo ilikuwa ni CCM kuongezewa diwani mmoja na siyo CUF.


“Tatizo linaonekena liko kwenye uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kuipotosha tume ya uchaguzi kuipatia taarifa zilizoiwezesha tume kumteua diwani wa CUF, haki hiyo ilikuwa ni ya CCM hivyo CCM wanapaswa kuidai haki hiyo,” alisema Lilongeli.

Naye diwani mteule aliyetarajiwa kuapishwa katika baraza hilo, Mchwanga, alisema kuwa kutokjuapishwa kwake katika kikao hicho kumemsikitisha kwa vile aliandikiwa barua na halmsahuri kuhusu uteuzi uliofanywa na tume ya uchaguzi Agosti 14, mwaka huu na kumtaka kuhuzulia kikao hicho ili aweze kuanza kutekeleza majukumu yake.

WAASWA KUFUATA SHERIA KATIKA ZOEZI LA KUONDOA WAFUGAJI KILOMBERO


Na Henry Bernard Mwakifuna, Itete-Ulanga

WATUMISHI watakaohusika na Operesheni Okoa Bonde la Kilombero wametakiwa kutenda Haki kwa Kufuata Sheria.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bwana Saidi Mecky Sadiq amesema kuwa suala la uonevu na ukihukwaji wa sheria halina nafasi katika  zoezi la kuwaondosha Wafugaji na Wakulima Wavamizi kuwa watakaobainika watachukulia Hatua kali dhidi yao kwa muujibu wa Sheria.

Amewataka Maaskari watakaoendesha Operesheni hiyo kutotumia Nguvu isiyo ya Lazima kupita kiasi huku akiwataka pia Wananchi nao kutochukua sheria mkononi kwa Silaha za jadi ili kuepusha mapambano baina yao.

Bwana Sadiq ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Wa Dar es Salaam alikuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Operesheni Okoa Bonde la Kilombero iliyofanyika katika Kata ya Itete Wilayani Ulanga.

Wakati huo huo Mifugo itakayokamatwa ndani ya Hifadhi ya Pori Tengefu la Kilombero itapigwa Mnada kwa Muujibu wa Sheria.

Bwana Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero akisoma Taarifa ya Hali Halisi ya Bonde la Kilombero amesema Mifugo hiyo pamoja na ile isiyosajiliwa na kupigwa Chapa itauzwa na Serikali kwa kufuata utaratibu wa Kisheria ulioandaliwa.

Amesema Vituo 11 vimetengwa  kwa Wilaya za Ulanga na Kilombero kwa ajili ya kuhifadhia Mifugo itakayokamatwa kwa kukihuka utaratibu.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilombero alikuwa akisoma Taarifa iliyoandaliwa juu ya Hali Halisi ya Bonde la Mto Kilombero linalojumiisha  Wilaya za Ulanga na Kilombero Mkoani Morogoro.

Ifakara wapania kutokomeza uvuvi haramu



Na Senior Libonge,Kilombero

JUMLA ya zana za uvuvi haramu yakiwemo makokoro 35 na nyavu ndogo 4 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 28.6 zimekamatwa katika doria zilizofanyika katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2012 katika mamlaka ya mji mdogo wa Ifakara.

Kwa mujibu wa afisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Ifakara Mercy Minja amesema mpaka sasa kesi zilizopelekwa mahakamani ni tano ambazo ni za kukamatwa na kokoro,kutishia kwa njia ya simu baada ya kukamatwa,kumiliki kokoro,kumiliki kokoro na kujeruhi kwa panga baada ya kukamatwa.

Mercy amesema lakini cha kushangaza hakuna mtuhumiwa aliyefungwa hadi sasa licha ya serikali kupitia mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera wakati akifungua miezi ya karibuni kuagiza jeshi la polisi na mahakama kutowachelewesha kuwahukumu wale wote watakaopatikana na hatia ya uvuvi haramu katika mto Kilombero.

Hata hivyo wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo wameiomba halmashauri ya wilaya kusimamia kwa umakini zoezi la doria kwa kushirikiana nao na hatimaye kuhakikisha vyombo vya sheria vinawahukumu haraka iwezekanavyo watuhumiwa ili kuwapa moyo wale wote wanaoendeleza doria katika mto huo.

Aidha mtendaji huyo wa mamlaka ya mji mdogo alizungumzia suala la ujenzi holela katika maeneo mbalimbali ya mamlaka ya mji mdogo Ifakara na kusema kuwa kumekuwepo na uvmizi wa ujenzi wa nyumba za makazi au za biashara katika maeneo hasa ya hifadhi ya barabara.

Amesema ujenzi huo unasababisha kushindikana kuwepo miundombinu ambayo inatakiwa kuwekwa pembezoni mwa barabara na kuitaja kuwa ni mifereji ya maji taka,upitishaji wa mkongo wa mawasiliano wa Taifa na nguzo za umeme.

Mercy amesema pia kumekuwepo na ubadilishaji wa matumizi ya ardhi bila ya kuwa na kibali cha kubadili matumizi ya ardhi hiyo kwa mfano kupewa eneo kwa ajili ya kujenga nyumba ya makazi lakini mtu anabadilisha na kujenga nyumba ya kulala wageni ama kiwanda bila kuwasiliana na mamlaka husika yenye jukumu hilo.

Amewaomba wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo kulisimamia na kuzuia watu kujichukulia sheria mkononi mwao kwa kuwazuia na kuwaelekeza nini cha kufanya ili waweze kuepuka kuendelea kubomolewa nyumba zao walizojenga bila kufuata kanuni,sheria na taratibu za ujenzi katika mamlaka ya mji mdogo.

IDADI KUBWA YA WANYAMA YATOWEKA BONDE LA KILOMBERO


Henry Bernard Mwakifuna, Itete-Ulanga

UVAMIZI wa Makazi, Kilimo na Mifugo ni sababu kubwa zinazopelekea kutoweka kwa baadhi ya Wanyama katika Hifadhi ya Bonde Tengefu la Kilombero.

Bwana Hassan Masala, Mkuu wa Wailaya ya Kilombero akisoma Risala ya Hali Halisi ya Bonde Tengefu la Kilombero katika uzinduzi wa Operesheni Okoa Bonde la Kilombero iliyofanyika hii leo Tarehe 30/10/2012 katika Kata ya Itete Wilayani Ulanga amesema kuwa Wanyama waliokuwapo katika Bonde hilo wamepungua kwa asilimia kubwa .

Amesema kuwa kulikuwa na Nyati 35,301 Mwaka 1991 lakini Mwaka 2009 Sensa ya Wanyama hao imebakia ni 1462 ni asilimia 4 tu ya wanyama hao, Mwaka 1991 kulikuwa na Tembo 1848 lakini Sensa ya Mwaka 2009 wamebakia Tembo 1,535.

Wakati Wanyama adimu aina ya Sheshe ambao ni jamii ya wanyama wanaopatikana sehemu 18 tu Duniani ikiwemo Kilombero wamebakia 18,161 Mwaka 2009 kutoka 36,569 Mwaka 1991 kwa muujibu wa Takwimu zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori nchini (TAWIRI).


Bonde Tengefu la Kilombero ni Makazi ya Asilimia 75 ya Sheshe wote wanaopatikana Duniani na Wito umetolewa kuweza kuwalinda wanyama hao wanaotoweka kwa kasi Ulimwenguni.

Operesheni Okoa Bonde la Kilombero imezinduliwa leo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bwana Said Mecky Sadiq, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Tuesday, October 23, 2012

Wafugaji Ulanga/Kilombero hatarini kukubwa na baa la njaa

Na Senior Libonge, Ulanga.

ZAIDI ya kaya 250 za wafugaji wa jamii ya wasukuma zipo katika hatari ya kukumbwa na janga la njaa baada ya familia hizo kudaiwa kuacha mazao ya chakula wakati wa operesheni ya kuwaondoka kwa hiyari wafugaji katika bonde la hifadhi la mto Kilombero kwa upande wa wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Akizungumza na Blog hii katika kijiji cha Kiwale kitongoji cha Lubemende tarafa ya Malinyi Mwenyekiti wa Umoja wa wafugaji wilaya hiyo (UWADAMO), Luhende Maduka Ng’asha alisema kuwa zaidi ya kaya 250 za wafugaji wa jamii ya wafugaji zipo katika hatari kubwa ya kukumbwa na baa la nja baada ya wafugaji hao kuacha mazao ya chakula katika operesheni iliyoanza Septemba 8 mwaka huu.

Ng’asha alisema kuwa baa hilo la njaa linaweza kujitokeza endapo serikali haitafanya juhudi za haraka za kuzinusuru familia hizo kwa kuzipatia maeneo ya kulima mazao ya chakula ikiwemo na malisho kutokana na baadhi ya familia hizo kuwa na akiba kidogo ya chakula kufuatia chakula cha ziada kutelekezwa mashambani kabla ya kufunwa wakati wa operesheni hiyo.

Vyakula ambavyo vinadaiwa kutekezwa ndani ya hifadhi hiyo kabla ya kuvunwa ni pamoja na mpunga, mihogo na viazi ambavyo vilikuwa katika hatua za mwisho ya kuvunwa kwake.

Ng’asha alisema kuwa familia za wafugaji hao zinahitaji kupatiwa msaada wa haraka hasa baada ya kukosa maeneo ya kulima na maeneo ya malisho kufuatia maeneo ambayo walikuwa wakiishi kuingizwa ndani ya hifadhi ya bonde hilo la mto Kilombero.

Hatua hiyo ya familia hizo kuacha mazao ya chakula katika maeneo yao ambayo walikuwa wakiishi kwa muda mrefu imekuja baada ya awamu ya pili ya uwekaji wa alama za mipaka kutengenisha hifadhi na vijiji hali ambayo awamu hiyo ya pili imeweka njia panda kufuatia kuingia ndani ya hifadhi huku baadhi ya vijiji vikidaiwa kubakiwa na maeneo madogo ya ardhi kwa ajili ya matumizi ya mpango wa matumizi bora ya ardhi. Alisema Ng’asha.

Ng’asha alisema kuwa kwa sasa familia hizo zimekuwa zikiishi katika mazingira magumu zaidi kutokana na kuacha makazi yao ya kudumu zikiwemo nyumba na mashamba ambayo yalikuwa yakitumiwa kwa ajili ya kilimo na nyumba za kudumu baada ya alama za mipaka ya awamu ya pili.

“Hapa kuna janga la njaa litatokea muda wowote kwa familia za wafugaji ambao wengi wao ni wale ambao walikuwa wakiishi nje ya hifadhi ya bonde la mto Kilombero lakini hali hiyo imetokana na mipaka ya awali kuwakuta wapo nje ya hifadhi na awamu ya pili mipaka hiyo imewakuta wapo ndani ya hifadhi hivyo na kuleta hali ya taharuki kwa familia hizo. Alisema Ng’asha.

Aliongeza kuwa familia hizo baada ya kuacha mazao ya chakula katika maeneo hayo imejikuta ikibakiwa na chakula kidogo ambazo hakikidhi mahijita kwani familia moja ina watu zaidi ya 30 na janga hilo la njaa linaweza kuwakumba kati ya Novemba na Disemba mwaka.

Wengi wao  kupoteza mwelekeo wa maisha ya baada ya wenzao ambao walielekea wilaya ya Namtumbo mkoani Songea kurudishwa katika wilaya ya Ulanga.

Operesheni ya wafugaji ya kuondoka katika bonde la Kilombero kwa hiyari  limewaweka njia panda wafugaji ambao walikuwa nje ya hifadhi hiyo ambapo kwa sasa shughuli za kilimo na malisho zimekuwa za shida kutokana na kuondoka ndani ya hifadhi na kuvamia maeneo mengine ambayo yaliyomilikishwa kihalali na wafugaji wengine.” alisema Ng’asha.

Ng’asha alisema kuwa katika mchakato wa kuelekea katika operesheni hiyo mambo mengi ya msingi hayakufuatwa na kukiuka baadhi ya taratibu za kisheria zilizowekwa na serikali ya Ulanga kwa madai kuwa baadhi ya watendaji wake waliwatoza wafugaji pesa nyingi isivyo halali.

Katika zoezi hilo la upigaji wa chapa mifugo ndilo moja ya mazoezi ambayo yanadaiwa kukiukwa kwa taratibu hasa baada ya watendaji hao kudaiwa kutoza kiasi cha pesa kuanzia sh 3,000, 5,000 na sh 10,000 kwa ng’ombe mmoja tofauti na kiasi cha sh1,000 ambacho kilitangazwa na wilaya hiyo.

“Hawa wafugaji ni moja ya jamii ambayo zimekuwa ikiishi kwa maisha duni hapa nchini na na kuonewa kutokana na ufahamu finyu hii imetokana na baadhi ya watendaji serikalini kutumia mwanya huo kujipatia pesa kwa kisingizio cha kukiuka baadhi ya sheria kwa wafugaji hao” alisema Mwenyekiti huyo.

Alitaja kero ambazo kwa sasa wafugaji hao wanazipata baada ya operesheni hiyo ni akinamama kujifungua chini ya miti, kukosa makazi na maeneo kwa ajili ya kilimo na malisho ambapo wafugaji hao waliingia katika maeneo hayo na kuishi zaidi ya miaka 20 kabla ya mwaka huu kutimuliwa kulingana na mipaka iliyowekwa.

Serikali ndiyo iliyotoa amri ya kuondoa wafugaji katika hifadhi ya bonde la mto Kilombero lakini pia inayo jukumu la kuwatafutia wafugaji maeneo ya malisho na pakuwa wafugaji wa jamii ya wafugaji wanajishughulisha na kufuga na kulima serikali nayo iliione hilo kwa kuwatafuatia maeneo kulingana na mahitaji yao. Ng’asha.

Mkuu wa wilaya ya Ulanga Francis Miti akizngumzia suala hilo alisema kuwa suala la njaa halitajitokeza kwa sababu ni kweli baadhi ya wafugaji waliacha vyakula katika maeneo hayo lakini serikali iliweka utaratibu mzuri wa wafugaji hao kuomba vibali na kumalizia kuchukua mazao hayo.

Sunday, October 21, 2012

Ifakara waaswa kutunza mazingira

Na Henry Bernard Mwakifuna- Ifakara

Afisa Tarafa Kata ya Ifakara Bi Hawa Lumuli Mposo amewataka wakazi wa Wilaya ya Kilombero kuyatunza mazingira yanayo wazunguka pamoja na kuchunguza makazi yao ili kuepukana na  tatizo la majanga.
Bi.Hawa ameeleza kuwa ni vyema kupanda miti mingi ili kuzuia kimbunga,kuacha kilimo cha  kuhamahama,pia ni vyema kuzuia mwendo kasi na ujazo wa abiria katika vyombo vya usafiri ili kuzuia majanga ya ajari za barabarani.
Aidha Bi. Hawa amewataka watu kuchunguza nyaya za umeme katika nyumba zao ili kupunguza maafa ya moto na kuwataka wananchi wawe na vifaa vya asili kwa ajili ya kuzimia moto.
Pia amesema Tatizo la mafuriko linasababishwa na watu wanao chimba mchanga ndani ya mto nakuzuia mifereji ya kupitishia maji kutoka mito midogomidogo kwenda kwenye mto mkubwa wa Kilombero watu wanatumia mifereji hiyo kama sehemu ya kutupia taka mto ukijaa unasababisha mafuriko na kuleta majanga.

Ulanga yapania kuboresha huduma za Afya

Na Senior Libonge,Ulanga
HALMASHAURI ya wilaya ya Ulanga imeiomba serikali itoe kipaumbele kwa hospitali ya wilaya hiyo ili iweze kukamilisha ukarabati wa majengo yake ambayo hayakidhi mahitaji halisi ya wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa wodi ya kisasa ya wazazi katika hospitali hiyo mganga mkuu wa wilaya ya Ulanga Dk Jacob Frank amesema majengo yaliyopo hivi sasa ni ya zamani na hayakidhi mahitaji halisi hivyo ukarabati wake utaboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dk Frank ameamua kutoa ombi hilo baada ya serikali kuikabidhi hospitali hiyo asilimia 30 tu ya fedha yote inayohitajika kwa ajili ya ukarabati huo tangu mwaka 2007/2008 ambayo ni shilingi milioni 600 wakati hospitali hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 2.
Amesema licha ya changamoto ya uchakavu wa majengo pia wanatatizo la upungufu wa watumishi wenye ujuzi,kukosekana kwa gari la kubebea wagonjwa,upungufu wa madawa na vitendea kazi na uchakavu wa majengo.
Hata hivyo mganga mkuu huyo amesema kwa hivi sasa matarajio yao ni kuendelea kuomba nafasi za kuajiri watumishi wenye ujuzi wa kada mbalimbali,kuongeza bajeti ya kununulia madawa na vitendea kazi kutoka vyanzo mbalimbali kana CHF,NHIF na Basket Fund ili kukidhi mahitaji halisi na kuendelea kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali.
Ameishukuru serikali pamoja na wafadhili wao wa Afya taasisi ya World Lung Foundation kwa misaada wanayipata katika kuboresha huduma za mama na mtoto wilayani humo.
Mganga mkuu huyo amesema kuwa taasisi ya World Lung Foundation licha ya kuwatengenezea wodi ya upasuaji kwa ajinamama pia wameviongezea hadhi vituo vya afya vya Mtimbira na Mwaya ambavyo vimeshaanza kutoa huduma za upasuaji na pia wanatoa mafunzo kwa watumishi wa kada mbalimbali ambao hufanya shughuli za upasuaji na utoaji wa dawa za usingizi kwenye vyumba vya upasuaji.
Kwa upande wake meneja mradi wa World Lung Foundation Dismas Masumbuko amesema kwa awamu hii inayomalizika mwaka 2015 wametenga dola za kimarekani milioni 8.5 lakini fedha zitaongezeka hadi kufikia dola milioni 15.5 punde ikimalizika awamu hii ya kwanza.
Masumbuko amesema toka wafungue vituo vya afya na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya katika maeneo mbalimbali nchini huduma ya uzalishaji salama wa akinamama umeongezeka toka kinamama 20 hadi kufikia akinamama 120 kwa mwezi na kusema kuwa ili kuboresha zaidi huduma wameanzisha kutoa huduma kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano.

Wednesday, October 17, 2012

HIFADHI YA UDZUNGWA WAKABIDHI ZAHANATI KISEGESE

Henry Bernard Mwakifuna. Kisegese-Kilombero

JUMLA ya Shilingi Milioni 95,703,587 zimetumika kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kisegese kilichopo kata ya Idete katika Wilaya ya Kilombero.
Akisoma Taarifa ya Makabidhiano ya Zahanati ya kijiji cha Kisegese mbele ya Mgeni Rasmi Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero Bwana Evarist Mmbaga, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa Bwana Vitalis Peter Uruka amesema Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi hiyo limechangia jumla ya Shilingi Milioni 87,042,320 katika ujenzi pamoja na Uwekaji wa Samani na Vifaa Tiba.

Amesema Mchango wa jamii katika mradi huo Zahanati ni Shilingi Milioni 8,661,267.
Ujenzi wa Zahanati hiyo umefanyika kwa Ushirikiano wa Jamii na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kupitia Idara za Afya na Uhandisi.
Ameongeza kuwa uwepo wa Zahanati hiyo ni utekelezaji wa Sera ya Serikali ya kutoa Huduma ya afya hivyo Jamii watanufaika kwa kupunguza umbali wa Wagonjwa kutembea kufuata Huduma za Matibabu.
Kuboresha na kuinua kiwango cha Afya hasa katika Huduma ya Mama Wajawazito kupata Huduma na kujifungua salama na kuwawezesha Wagonjwa kupata Matibabu mapema kwa Maradhi yanayoweza kutibika.
Bwana Vitalis ameongeza kuwa uwepo wa Zahanati hiyo ya Kisegese utaongeza ari na Tija kwa Wananchi kuwawezesha kufanya shughuli za kimaendeleo na za kujiongezea kipato kama kilimo, Biashara na hivyo kuinua uchumi wao.
Hifadhi ya Milima ya Udzungwa ni Mojawapo ya Hifadhi 16 zinazosimamiwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa(TANAPA) na ni Sehemu ya Safu ya Miliam ya Tao la Mashariki.

Wananchi Ulanga walia ughali wa pembejeo za kilimo

Na Senior Libonge,Ulanga
WANANCHI wilayani Ulanga wamedai kuwa licha  pembejeo za ruzuku za kilimo kuchelewa kufika kwa wakati pia pembejeo hizo zimekuwa bei ghali na hali hiyo umfanya mkulima wa chini kushindwa kuipata na kutimiza malengo yake katika kilimo..
Wakizungumza katika mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma sekta ya kilimo wilaya ya Ulanga yanayotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya kikundi cha wanawake wa St.Maria Magdalena ya Ifakara wananchi hao wamesema kuwa serikali inatakiwa kushirikisha viongozi wa vitongoji katika ugawaji na sio kamati ya vocha.
Wamesema kuwa kutokana na kuchelewa kufika kwa wakati kwa mbolea hizo imepelekea wananchi kulima bila kutumia mbolea na punde mbolea ikifika ulundikana katika ofisi za serikali kwani zinakuwa hazina kazi tena.
Julius Mwere mkazi wa Kivukoni amesema kuwa gharama ya mfuko mmoja wa mbolea ya minjingu uuziwa mkulima hadi kiasi cha shilingi 80,000 na hali hiyom umfanya mkulima kushindwa kununua mbolea hiyo kutokana na gharama kuwa kubwa.
Naye Hassan Mkamla mkazi wa Lupiro ambaye ni mlemvu amesema kuwa hata wao hawapatiwi mbolea hizo na wakifuatilia kwa watendaji wa vijiji uambiwa kuwa wakaonana na wakala wao na hata wakienda huko huwa wanazungushwa na hakuna wanachopata.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji cha Kivukoni  Josephat Masanyoni alikiri kweli kuwa malalamiko ya wananchi hao ni ya msingi na kuelezea suala la mbolea kuwa kweli ilichelewa kufika na licha ya kufika baadhi ya wananchi walikosa na tatizo kubwa ni uchangiaji wa fedha toka kwa wananchi.
Masanyoni alisema uchelewaji wa mbolea hizo umepelekea mifuko kadhaa ya mbolea kulundikana katika ofisi yake baada ya wakulima kukataa kuipokea kwa madai kuwa imefika muda ambao sio wa kwake kwani wakulima walikuwa wamekwisha panda na wanasubiria kuvuna.
Mratibu wa mafunzo hayo Bi Christina Kulunge amesema mafunzo yameendeshwa katika kata za Kivukoni,Minepa na Lupiro huku lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wananchi kuhusu ufuatiliaji wa pembejeo za ruzuku katika sekta ya kilimo na  mradi huo ni wa mwaka mmoja na una gharama ya shilingi milioni 43 ambazo zimefadhiliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya The Foundation for civil society.

ULANGA WAZINDUA WODI YA KISASA YA UPASUAJI KWA WAZAZI



Na Senior Libonge,Ulanga


KATIKA kuboresha huduma za akinamama wajawazito ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na madhara wakati wa kujifungua,wilaya ya Ulanga imezindua wodi ya wazazi ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 205,904,500.
Uzinduzi huo ulifanyika jana katika hospitali ya wilaya mbele ya katibu tawala wa mkoa wa Morogoro Eliya Ntandu ambapo katika uzinduzi mtoto wa kwanza wa kiume alizaliwa baada ya mzazi wake kufanyiwa upasuaji wa kwanza uliokuwa wa mafanikio.

Mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa upasuaji baada ya uzinduzi wa wodi hiyo


 Katibu tawala mkoa wa Morogoro Eliya Ntandu akizungumza na wananchi wa mji wa Mahenge wakati wa uzinduzi wa wodi ya kujifungulia akinamana, kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Ulanga Francis Miti na kulia kwake ni mwenyekiti wa halmashauri Furaha Lilongeri.

Katibu tawala mkoa wa Morogoro Eliya Ntandu akikata utepe kuashiria uzinduzi wa wodi ya upasuaji kwa akinamamaa katika hospitali ya wilaya ya Ulanga,kushoto ni meneja mradi wa World Lung Foundation Abbas Masumbuko na kulia ni mkuu wa wilaya ya Ulanga Francis Miti

Kwa mujibu wa mganga mkuu wa wilaya ya Ulanga Dk Jacob Frank amesema mradi wa ujenzi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2010 baada ya makubaliano kati ya halmashauri ya wilaya ya Ulanga na shirika la World Lung Foundation kutoka nchini Marekani.
Dk Frank alisema kazi ya ujenzi wa jingo hilo ulitekelezwa kwa awamu mbili kwa awamu ya kwanza kugharimu shilingi milioni 91,395,500 ikiwa ni fedha zilizotolewa na World Lung Foundation na kazi zilizofanyika ni kusafisha eneo,kuchimba na kujenga msingi,kujenga ukuta na kupaua.
Amesema awamu ya pili ilihusisha kazi ya umaliziaji wa ujenzi wa jengo ambapo kiasi cha shilingi milioni 82,192,450 zilitumika ambazo zilitengwa na halmashauri ya wilaya ya Ulanga lakini ilibidi halmashauri hiyo kutumia force account na hadi kukamilika kwa mradi huo halmashauri hiyo imekwisha tumia gharama ya shilingi milioni 114,509,000.
Mganga huyo amesema ili licha ya kugharamia jengo pia wafadhili hao wa World Lung Foundation wametoa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 45 ikiwemo kitanda cha upasuaji,baby cot,air condition,suction machine,vifaa vya upasuaji,pass oxmiter,mashine ya kutolea dawa ya usingizi na vitanda vya kujifungulia.
Licha ya kuzindua wodi hiyo ya kisasa kujifungulia akinamama wajawazito hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi wenye ujuzi hasa madaktari,wauguzi,matabibu na wateknolojia maabara,kukosekana kwa gari la wagonjwa,upungufu wa madawa na vitendea kazi na uchakavu wa majengo.
Kwa upande wake meneja mradi wa World Lung Foundation Dismas Masumbuko amesema kwa awamu hii inayomalizika mwaka 2015 wametenga dola za kimarekani milioni 8.5 lakini fedha zitaongezeka hadi kufikia dola milioni 15.5 punde ikimalizika awamu hii ya kwanza.
Masumbuko amesema toka wafungue vituo vya afya na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya katika maeneo mbalimbali nchini huduma ya uzalishaji salama wa akinamama umeongezeka toka kinamama 20 hadi kufikia akinamama 120 kwa mwezi na kusema kuwa ili kuboresha zaidi huduma wameanzisha kutoa huduma kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano.
Naye mgeni rasmi Katibu tawala mkoa wa Morogoro Eliya Ntandu amewapongeza wafadhili hao kwa kutekeleza malengo yao tofauti na baadhi ya taasisi nyingine ambazo azifuati sera zao.
Ntandu amewataka akinamama wajawazito wilayani humo kwenda kwa wingi kujifungulia katika hospitali ya wilaya na kuacha kujifungulia majumbani hasa baada ya huduma kuboreshwa ila amewataka watumishi wa afya kutumia vyema vifaa walivyopata ili kuokoa vifo vya akinamama na wajawazito.

 

Thursday, October 11, 2012

Upungufu wa Maji unatisha mto Kilombero

Na Ferdinand Nachenga

Jana nilipata bahati ya kutembelea kivuko cha Mto Kilombero maarufu kama kivukoni mida ya saa kumi na mbili jioni. Nikakaa kwenye pub ya upande wa Ifakara japo ilikua inanuka maana kuna choo kisichosafichwa kwa muda mrefu karibu na hiyo pub.

Hapakua na watu,nikaagiza kinywaji kisha nikapanda juu na kuanza kuangalia mandhari ya bonde la Kilombero. Nilichoshuhudia ni jinsi gani kilimo na ufugaji vilivyoathiri mto kilombero. Sijawahi kuona maji ya mto huu kukauka kiasi kile,nadhani ulimaji karibu kabisa na mto pamoja na ufugaji inabidi vipigwe vita sana ili kunusuru mto huu na bonde kwa ujumla.

Pantoni lilikua linaendelea na shughuri zake japo wanasema mwisho saa kumi na mbili jioni. cha ajabu ni kwamba pantoni haina taa inatumia taa za magari yanayopakiwa humo dah nilisikitika sana huku niki...kumbuka kilichotokea miaka kadhaa iliyopita.

Kufika saa mbili hivi nikashuka chini na kuona mlinzi anazuia watu wasiingie maana muda umeisha lakini kama una 500 unaruhusiwa na pikipiki ni 2000 bila kutoa risiti. Nami nikajifanya nataka kuvuka lakini jamaa alisema bila 500 nisubiri kesho na mia mbili yangu.

Wenye pesa walienda na wengi masikini walikwama hasa wakina mama. Nilipouliza kwa nini wanafanya hivyo nikaambiwa wao wakale wapi? kwa hiyo zile zote ni zao. Niliumia sana lakini huo ndio uozo wa uongozi wa wilaya yetu. yani hata taa ya pantoni hawawezi kununua? Ajali ikitokea nani alaumiwe? nani atafidia wahanga?kwa gharama ipi? ..we need to act now guys....

Umaskini katikati ya msitu wa ndizi mbingu.



Na Rwambogo Edson

Kata ya Mbingu ipo kusini mwa wilaya ya kilombero. wilaya hiyo inaunda jimbo moja la uchaguzi ambalo ni jimbo la kilombero mkoani Morogoro. Mkoa wa morogoro una ukubwa wa kilometa za mraba 70,799. Kata ya mbingu ipo kilometa 290 kutoka Morogoro mjini, mji ambao ni makao makuu ya mkoa. Umbali kutoka makao makuu ya wilaya Ifakara ni kilometa 60. Kijiografia upande wa magharibi na kaskazini kata ya mbingu imepakana na hifadhi ya Milima ya Udzungwa. Sehemu kubwa ya kata hii ni tambalale na baadhi ya vijiji vipo milimani.

Wakazi wa kijiji cha Mbingu ni wakulima wa ndizi maarufu kwa jina la ndizi Mzuzu. Pamoja na zao hilo kustawishwa kwa wingi katika maeneo mengi ya wilaya ya kilombero ikiwemo Mbingu, lakini pia mazao kama Cocoa, mahindi, mpunga, miwa na mazao mengine pia hustawishwa kwa wingi katika kijiji hiki. Mzee madeje anasema ata jina mbingu inasemekana lilitokana na kuwa kila kitu kinacholimwa mbingu kinastawi pamoja na umbali uliopo kutoka miji mingine.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mpofu Bwana John Haule John anasema kata ya mbingu imegawanyika sehemu za milimani na mabondeni. Wanakijiji cha mpofu kilichopo uwanda wa milimani hutegemea zaidi kilimo cha ndizi, wananchi hao hulima kwa mwaka mzima zao hilo ata wakati wa masika. Tofauti na Wakazi wa vijiji vya mabondeni wakati wa masika hulima kilimo mseto zaidi kwa kuchanganya kilimo cha mpunga, mahindi, maharagwe na mazao mengine.

Bwana haule anaongeza kuwa wakati wa masika biashara ya ndizi kwa upande wa vijiji vya milimani huwa nzuri kwani bei ya ndizi hupanda kidogo. Mkungu mmoja huanzia bei ya shilingi mia nane kwa mikungu midogo maarufu kwa jina la viserebende mpaka elfu tano kwa mkungu mkubwa. Lakini wakati wa kiangazi mkungu mdogo huuzwa kwa shilingi mia mbili mpaka mia tano na wakati mwingine hutolewa kama nyongeza kwa wafanya biashara wakubwa.

Kijana Harrison Makaye mwanafunzi mkazi wa kijiji cha mpofu aliyehitimu masomo ya mawasiliano ya umma mwaka huu anasema, wakati wa masika biashara huwa ngumu zaidi kwa kuwa magari mengi kama fuso hayafiki kutokana na sehemu iliyopo barabara kuu kutoka makao makuu ya wilaya Ifakara ipo sehemu ya bonde, kutokana na mafuriko ya mto Lwipa barabara hujaa maji baadhi ya sehemu korofi.

Anasema hali hiyo huwalazimu wakulima kusafirisha ndizi kwa usafiri wa baiskeli mpaka kijiji cha Namawala ambapo magari kutoka sehemu mbalimbali huishia. Lakini pia walanguzi hutumia nafasi hiyo kuwa kandamiza wakulima kwa kuwapangia bei wanazozitaka kwani umbali kutoka mbingu mpaka Namawala ni zaidi ya kilometa kumi na tano kwa hiyo wakulima hawawezi kurudi na mzigo majumbani mwao kutokana na umbali huo. Wakati mwingine wakulima hulazimika kutupa ndizi wanazoshindwa kupata soko lake huko wanakopereka .

Wanakijiji cha mbingu, pamoja na kuwa na utajiri wa ardhi inayokubali kustawisha kila aina ya zao, lakini bado hawana shule za msingi za uwakika. Mwanafunzi Filbert Madeje anasema inatokana na wazazi wao kuwa na kipato kidogo na kisicho cha uwakika katika kuchangia maendeleo ya shule. Mfano wananfunzi wa Shule ya Msingi Mpofu wanasomea chini ya Mti na wengine katika madarasa yaliyoezekwa kwa nyasi bila kuzibwa pembeni. Mzee hamisi mfanya biashara na mlanguzi wa ndizi kwa kipindi kirefu anasema inatokana na serikali kutokuongeza idadi ya majengo kulingana na ongezeko la watu.

Mzee Hamis Anasema wakati wanaanza biashara ya ndizi hapakuwa na watu wengi kama ilivyo sasa. Anasema ata vituo vya Polisi kwa ajiri ya usalama wa raia pia havijaongezwa, hospiatali ipo moja nayo muda wote haina madawa ya kutosha. Barabara nayo inaharibika bila kufanyiwa marekebisho, mfano daraja ambalo ni kiunganishi kati ya kijiji cha mpofu na Londo ni bovu na tangu lilipojengwa kwa nguvu za wananchi miaka mitano iliyopita limebaki lile lile la mbao ambalo linahatarisha wanaolitumia na halina uwezo wa kupitisha vyombo vya usafiri zaidi ya baiskeri.

Mradi wa Soko la pamoja la ndizi lililotarajiwa kujengwa kwa ajiri ya wakulima wadogo umebakia historia tangu lilipoanza kujengwa na kuishia kwenye msingi, imepita miaka minne bila kumaliziwa.

Kuhusu usafiri wa reli ya Uhuru mkulima wa ndizi kijiji cha Londo Bwana Philimoni Mgogo anasema, ufanisi mdogo wa reli ya Uhuru umewaathiri, hasa ikizingatiwa miaka ya tisini wakulima walikuwa wakiuza ndizi nyingi sana kwa kuwa wateja wao walikuwa wanabeba mzigo mkubwa kupitia usafiri wa reli. Anasema usafiri wa reli haukuwa wa msimu ata wakati wa masika hawakuwahi kuwaza wangeuza wapi ndizi zao.

Nae mzee kondo anaongeza kwa kusema wafanya biashara wa Mbingu walikuwa wanabeba ndizi zao mpaka Dar es salaam na kuuzia steshen ya TAZARA. Anasema wakati mwingine walikuwa wakimaliza mzigo kabla hawajafika Dar es salaam na kugeuza wakiwa na hera ya kulipia watoto karo. Anasema hawakuwa ombaomba kama walivyo sasa kwa kuwa usafiri wa Reli sasa hivi hauna uwakika. Mfano unaweza ukaambiwa treni itapita saa tano asubuhi ikapita saa tano usiku, hali hiyo inawakatisha tamaa wafanya biashara wadogo hasa ikizingatiwa hawana vifaa vya kuhifadhia bidhaa zisiharibike .

Wakulima wa kijiji cha mbingu wanasema usafiri wa kutegemea magari unawaumiza, kwa sababu mafuta yakipanda ghalama za usafiri zinapanda pia. Lakini ghalama za ndizi zinabaki pale pale, pia magari yanasafirisha ndizi msimu wa kiangazi tu, wakati wa masika magari hayafiki, ata kipindi cha kiangazi ndizi huwa nyingi zaidi hali inayoperekea ndizi zinaendelea kubaki na wakati mwingine zinaoza.

Kuhusu mafuriko yaliyotokea mwezi wa nne mwaka huu, Afsa Mtendaji wa kijiji cha Mpofu bwana Charles Tapule anasema wananchi wengi wameathirika kutokana na mafuriko hayo. Kuna baadhi wamefiwa na mifugo yao, hifadhi ya chakula iriharibika na baadhi ya maeneo miundo mbinu iliharibiaka kabisa.

Lakini anawashukuru wahisani na Serikali kwa kujitolea mavazi pamoja na vyakula kwa ajiri ya wahanga wa tukio hilo. Pia anawaomba wakazi wa kijiji hicho kutumia misimu ya mvua vizuri inayokuja kuweka hifadhi ya chakula na kujenga vizuri makazi yao kwa ajiri ya kujikinga na hali hiyo. Wanakijiji wa kijiji cha Londo na maeneo mengine katika kata ya Mbingu waliathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua za masika zilizonyesha mwezi wa nne mwaka huu.

Lakini pamoja na hayo, Bwna tapule anatoa wito kwa Serikali kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi jinsi ya kutumia Mbolea za ruzuku. Hali hiyo inatokana na wananchi wengi kutoitikia mwito wa kutumia Mbolea kwenye mashamba ya Ndizi, kwa madai mbolea za viwandani zinaua rutuba ya ardhi na kusababisha baadhi ya mazao ya asili kutoweka.

Kauli hiyo inathibitishwa na Mzee Madeje, ambaye anasema ni kweli mazao mengi ya asili yametoweka baada ya wananchi kuanza kutumia Mbolea za viwandani. Mfano wa mazao hayo ni kama vile mbogamboga kama mchicha poli, Nyanya poli, mapera, mapensheni poli, mchunga, mnavu na mengine mengi. Anaongeza kwa kusema ata magonjwa ya mazao yamekuwa mengi sana kwani ata minazi na ndizi vinashambuliwa siku hizi.

Kuelekea miaka hamsini ya Uhuru mwenyekiti wa kijiji cha Mpofu anatoa wito kwa serikali kuliangalia upya suala la usafiri wa reli na kuiomba irudishe ufanisi wake kama zamani. Anasema alama ya wananchi wa mkoa wa Morogoro kuwa walipata uhuru ni ufanisi bora wa reli ya Uhuru. Anasema ata baadhi ya wanakijiji wanarazimika kuanza kukimbilia kulima mazao wasiyoyajua kama Cocoa kutokana na soko la ndizi kuendelea kudorola kila kukicha kutokana na ugumu wa usafiri.

nao baadhi ya wanakijiji wameanza kukata na kuchimbua migomba kama walivyofanya wananchi wa maeneo ya kilombero baada ya kuchimbua michungwa na kulima miwa. Uongozi na serikali umeanza kuwahamasisha wananchi wa Mbingu kulima miwa kwa ajiri ya kiwanda cha sukari cha kilombero.

Mfanya biashara ndogondogo Bi Magreti Benjamini anasema suala hilo lisipoangaliawa vizuri wananchi wengi watakipuuza kulimo cha ndizi na watageukia kwenye mazao ya Cocoa na Miwa. Kwa sababu wanunuzi wa miwa na cocoa wananunua kwa bei nzuri na hawasumbui. Anasema imefikia wakati baadhi ya walanguzi kutoka Dar es salaam wanawakopa wakulima wa ndizi, na kutokomea na hera zao wanazowadai wafanyabiashara wa Mbingu

WAKULIMA WASHAURIWA KUFUATA KANUNI BORA ZA KILIMO

Na Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero

WAKULIMA Wilayani Kilombero wameshauriwa kufuata kanuni Bora za Kilimo wanazokuwa wanazipata kutoka kwa Maafisa Ugani ili kuweza kuzalisha mazao yao kwa Tija.

Bi Hawa Ndapanya,Mtaalamu wa Kilimo Kitengo cha Huduma za Ugani upande wa Shamba Darasa Wilayani Kilombero amesema katika kuzalisha mazao bora mkulima lazima azingatie kulima kwa wakati,kuchagua Mbegu bora, kupanda kwa wakati na kuwa na matumizi sahihi ya pembejeo ndipo mavuno bora yawezekana.

Amesema kuwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo kwa wakati na msimu ukiwa mzuri kwa wakulima wa Mpunga wanaotumia Mbegu ya Salo au TXD 306 waweza kupata Magunia 35 kwa Hekari moja ya zao hilo.

Wakulima wakizingatia kanuni hizo na kuacha nafasi kati ya mimea kwa senimita 20 kwa 20 wilaya ya Kilombero itakuwa imefanikiwa kwa asilimia kubwa kutekeleza maagizo ya kilimo kwanza na dhamana kubwa ya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa.

Kwa kuzingatia kanuni zote za kilimo bora uzalishaji wa mazao Utaongezeka na kuweza kujitosheleza kwa Chakula na ziada kuweza kukidhi mahitaji mengine ya Wakulima.

Wakati huo huo,Bi Hawa amewashauri Wakulima kuendelea Kulima mazao yanayostahimili ukame kwani nayo ni mkombozi pindi hali ya Hewa inapokuwa si nzuri.

Amesema kwa Mkulima wa kawaida anapolima Hekari 3 anashauriwa kuwa na hekari moja ya zao la Biashara na Hekari mbili za Mazao ya Chakula zinazoweza kuhimili ukame.

Bi Hawa Ndapanya, ambaye pia ni Mwezeshaji Mkuu katika Mafunzo kwa Wataalamu wa Kilimo kuhusu dhana ya Shamba Darasa alikuwa akitoa mada ya Dhana ya Shamba Darasa kwa Washiriki wa Mafunzo ya Siku Nne kwa Wataalamu hao, mafunzo yanayosimamiwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na Uhifadhi wa Mazingira katika Bonde la Kilombero (KIVEDO) chini ya Ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Plan International.


SHAMBA DARASA KUPUNGUZA TATIZO LA MAAFISA UGANI


Na Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero

MBINU ya Shamba Darasa inatarajiwa kusaidia kupunguza tatizo la Uhaba wa Maafisa Ugani Vijijini.

Juliana Njombo,Mwezeshaji wa Shamba Darasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero amewaambia Washiriki wa Mafunzo kwa Wataalamu wa Kilimo kuhusu Dhana ya Shamba Darasa kuwa Mkulima aliyeshiriki ipasavyo katika mafunzo ya Shamba Darasa anakuwa Mtaalamu na anauwezo wa kusaidia Wakulima Wengine.

Amesema Kuwa pindi mkulima anapowezeshwa na mwezeshaji wa Mafunzo ya Shamba Darasa anakuwa Mtaalamu baada ya Kuhitimu naye anawafundisha wenzake na kutanua wigo kwa wakulima wengine katika kila kipindi cha msimu wa Kilimo na hivyo kusaidia kupunguza tatizo la Maafisa Ugani katika baadhi ya Vijiji.

Lengo kuu la Mafunzo hayo ya Siku Nne yanayoshirikisha Maafisa Ugani wa Vijiji Saba,Wataalamu kutoka Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Kilombero Wawili,wawezeshaji Wawili na watu wa Kada nyingine Jumla yao 15 ni washiriki kuweza kupata ujuzi wa kuanzisha na kuendesha shamba Darasa katika Maeneo husika.

Mafunzo hayo yanayoendeshwa na Wawezeshaji kutoka Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Kilombero inasimamiwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojihushisha na Mazingira katika Bonde la Kilombero (KIVEDO) chini ya Ufadhili Serikali ya Ujerumani kupitia Wizara ya Uchumi na Maendeleo kupitia Plan International.

 

MIFUGO ZAIDI YA 20 YAFA KWA KUKOSA MAJI NAMHANGA

Henry Bernard Mwakifuna, Namhanga Ulanga
 
ZAIDI ya Ngombe na Mbuzi 20 wamekufa kwa kukosa maji katika Kitongoji cha Mbenja, kijiji cha Namuhanga Wilayani Ulanga.
 
Nkuba Ngwandu, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wafugaji cha Mbenja Livestock cooperative amesema Mifugo hiyo imekufa kutokan na  Serikali Wilayani Ulanga kukataza kunywesha Maji mifugo yao katika Mto Mnjeta.
 
Mbali ya Tatizo hilo Wafugaji hao wamelalamikia Mipaka iliyowekwa na Serikali kuwa ipo ndani ya makazi yao.
 
Baadhi ya Wafugaji wamesema kuwa  wameingia katia eneo  la Mbenja kihalali baada ya kuomba maombi yao kwa serikali ya kijiji cha Namuhanga na kukubaliwa kuishi katika eneo hilo.
 
Mwenyekiti wa kijiji cha Namuhanga Bwana Iddi Lihogoya amekiri serikali kuwakataza Wafugaji kunywesha  mifugo kyao katika Mto Mnjeta na Kuongeza kuwa Wafugaji hao wameingia kihalali katika kijiji hicho baada ya kuandika barua ya kuomba kuishi katika eneo la Mbenja na wananchi wa kijiji hicho kukubali.
 
Kwa upande wake Bwana Francis Miti , Mkuu wa Wilaya ya Ulanga amekiri Serikali kuwakataza Jamii ya Wafugaji wa eneo la Mbenja, kunywesha Mifugo yao katika Mto Mnjeta kwa kuwa tayari Maeneo hayo yapo katika Eneo la Hifadhi ambapo Shughuli zozote za Kuichumi ikiwa pamoja na Ufugaji  hairuhusiwi kuingia katika Eneo hilo.
 
Amewataka Wafugaji kuchimba Mabwawa ya kunyweshea mifugo yao ili kuokoa mifugo yao inayokufa kwa kukosa maji ambapo hapo awali wamekuwa wakitegemea kunywesha mifugo yao katika mto mnjetwa.
 
Amesema wafugaji wajitokeze kuchimba mabwawa ya maji na serikali inaweza kuwasaidia katika kuchimba mabwawa ya maji baada ya nguvu zao kuonyesha kwanza.