HONGERA ULANGA COMMUNITY RESOURCE CENTRE

photos

Welcome to UCRC

About Me

Ulanga Community Resource Centre is a not-for-profit company limited by guarantee which was initiated with the aim of capacitating the resident peoples of Ulanga and Kilombero Districts and Tanzania in general to secure the right information and hold their duty bearers accountable in a bid to promote sustainable community development. UCRC as well aims at promoting educational activities in Ulanga District through facilitation of necessary educational resources in the area which include well equipped libraries and study centers. UCRC also works on land and natural resource rights for the marginalized rural people in Tanzania which also include sustainable use of such resources. It also provides legal aid and assistance to the poor, particularly women, children, the disabled and other disadvantaged groups in the society on different themes including land and gender.

Tuesday, November 27, 2012

SUALA LA ARDHI BADO LAFUKUTA KILOMBERO


Na Senior Libonge,Kilombero

SERIKALI wilayani Kilombero imesema kuwa itafuta mpaka wa kugawa ardhi ya kijiji na hifadhi bila kujali gharama iliyotumika kama ikibainika kuwa mpaka huo umekosema.

Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Miwangani kata ya Idete baada ya wananchi hao kulalamika mbele ya mkuu huyo wa wilaya kuwa mpaka uliowekwa hivi karibuni kutenganisha kijiji na eneo la hifadhi umemega sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji.

Hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Kilombero iliweka mpaka wa kutenganisha vijiji na eneo la hifadhi la lengo ni kuyatenganisha maeneo hayo ni kutekeleza azimio la Ramsar lililotaka kutunza maeneo ya ardhi oevu ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

Hata hivyo zoezi hilo lililofanywa na wataalamu wa mazingira na ardhi wa wilaya lililalamikiwa na baadhi ya wananchi ambapo mpaka huo umepita kuwa wataalamu hao walikuwa wakifanya kazi bila kushirikisha serikali za vijiji ambazo zinajuwa mipaka halisi ya vijiji vyao na eneo la hifadhi.

Masala amesema kuwa ameamua kufika katika kijiji hicho ili kupata ukweli kuhusu tatizo la mipaka baada ya kupata barua na kupigiwa simu kutoka kwa viongozi wa kijiji na wananchi kuwa wataalamu walikwenda kuweka mpaka wamemega sehemu kubwa ya kijiji na kufanya wananchi wa kijiji hicho kukosa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.

Na alipotoa nafasi kwa wananchi ili kutoa kero zao wananchi wote waliosimama walilalamikia suala la mpaka na kusema kuwa kama serikali isipochukua hatua za haraka kurekebisha mpaka huo kuna hatari ya kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji kwani hivi sasa mifugo iliyopo katika kijiji hicho inalishiwa katika mashamba ya wakulima kwa kukosa sehemu za malisho ambazo mwanzo zilitengwa eneo lililomegwa.

Ilibidi mkuu wa wilaya aingilie kati kupunguza hasira baada ya kutokea hali ya kutupiana maneno makali waliokuwa wakirushiana kati ya wataalamu wa ardhi na maliasili na mwenyekiti wa kijiji cha Miwangani Abdul Mtilangondo ambapo kila mmoja alikuwa akijitetea kuwa yupo sawa katika suala hilo.

Baada ya wataalamu kusema kuwa mpaka uliowekwa ni halali kwani wametumia kifaa maalum cha kupimia GPS na wakati wanaendesha zoezi hilo walishirikisha serikali ya kijiji lakini wakati zoezi linaendelea mwenyekiti wa kijiji aliwashawishi wajumbe wa serikali ya kijiji kususia zoezi hilo.

Naye mwenyekiti wa kijiji Mtilangondo alisema kuwa wakati zoezi linafanyika aliamua kugoma kutokana na wataalamu hao kupindisha mipaka wakati ramani halali inaonyesha mipaka inapotakiwa kupita lakini wataalamu hao wanagoma na kuweka mipaka wanayotaka wao na hali hiyo ndiyo ilipelekea yeye na wajumbe wake kususia zoezi hilo.

Ndipo mkuu wa wilaya alipoamua kuingilia kati na kusema kuwa itabidi zoezi hilo liangaliwe upya kati ya wataalamu wa halmashauri na viongozi wa serikali ya kijiji na ikibainika kuwa mipaka imekosewa itafutwa na kuwekwa upya bila kujali gharama iliyotumika ila ikionekana na halali itabidi mipaka hiyo iheshimiwe.

Masala alisema cha msingi ni kulinganisha mipaka halali kwa kufuata ramami za vijiji husika na ramani za wilaya kwani zoezi hilo sio la kuwakomoa wananchi bali ni kuyahifadhi maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibika baada ya kuvamiwa na kusema kuwa kama mipaka ipo halali yeye hana mamlaka ya ubadilishaji wa mpaka huo.

LUPIRO KUNUFAIKA NA MRADI MKUBWA WA MAJI


Na Senior Libonge,Ulanga

Wananchi wa kijiji cha  Lupiro  chenye wakazi zaidi 4000 wilayani Ulanga mkoani Morogoro wanategemea kunufaika na mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na benki ya Dunia.

Akiongea wakati wa ziara ya Madiwani wa kamati ya Fedha Utawala na Mipango kutembelea miradi ya maendeleo Mhandisi wa Maji Wilaya ya Ulanga  Patrice Jerome amesema benki ya dunia imetoa kiasi cha Tshs milioni 233 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Lupiro ambapo miundombinu ya maji ,tanki la kuhifadhia maji na ujenzi wa vituo 20 vya maji vya  jumuiya ,ufungaji wa mabomba ya maji , ujenzi wa pampu house na ufungaji wa pampu ya kusukuma maji .

Jerome amesema kuwa tanki linalojengwa litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 90 za maji (sawa na lita 90,000) na kuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa tarafa hiyo kwani eneo hilo lina uhaba mkubwa wa maji kwa muda mrefu.

Amesema mradi huu ni miongoni wa miradi ya vijiji 10 vinavyotarajiwa kujengwa kupitia pragramu  hii ya maji na usafi wa mazingira.

Nao wajumbe wa kamati waliwashukuru benki ya dunia kupitia program ya maendeleo ya sekta ya maji kwa kufadhili mradi huo kwani itawasaidia wananchi na kuwasihi wananchi  kutunza na kuhifadhi vizuri mradi huo pindi utakapokamilika ili uwe endelevu na kufikia lengo la kuanzishwa kwa mradi huo.

 Kamati imesisitiza kuanzishwa  na kusajiliwa kwa jumuiya hiyo ya watumiaji maji sambamba na kuwa na mfuko wa maji kwa ajili ya kuendesha mradi huo.Pia miradi mingine kama Igota kichangani  na Gombe ifuatiliwe kwani taratibu za manunuzi  zilishakamilika ili ianze kujengwa .

Akizitaja changamoto zinazojitokeza katika ujenzi wa mradi huo mshauri wa mradi Bw Raymundi wa kampuni ya ushauri ya Interconsult  ya Dar  es salaam amesema kuwa ni ugumu wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na uhaba wa upatikanaji wa vibarua ambapo wengi wao wanadai maslahi makubwa kuliko fedha iliyopangwa.

Ziara ya kamati ya Fedha Utawala na Mipango pia ilitembelea miradi mbalimbali katika tarafa za Vigoi,Lupiro na mradi mkubwa wa umwagiliaji unaoanza kujengwa katika kata ya Minepa.

Monday, November 12, 2012

VIONGOZI WATAKAOBAINIKA KUWAKUMBATIA WAVAMIZI KUKIONA


Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero.

MKUU wa Wilaya ya Kilombero Bwana Hassan Masala amesema kiongozi yoyote atakayewaficha Wavamizi wa Bonde la Kilombero atachukuliwa hatua za Kisheria.

Amesema kuna taarifa kutoka kwa Wananchi kuwa kuna baadhi ya Viongozi wa Vijiji wamekuwa wakiwakingia Kifua Wafugaji kwa kuwapa taarifa za siku ambayo zoezi litafanyika katika maeneo yao na kuwaficha Wavamizi na Wakulima walioingia katika mipaka ya Bonde Tengefu la Kilombero.

 Ameomba ushirikiano kutoka kwa Wananchi ili kuweza kuwabaini wale wote wanaokwamisha zoezi hili la Uhifadhi wa Bonde hili huku akitilia mkazo kuwa Zoezi si la Mkuu wa Wilaya.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa Mifugo mingi kwa kiasi kikubwa imeanza kuondoka Wilayani Kilombero.
Ametilia mkazo kuwa si mifugo yote inatarajiwa kuondolewa Wialayani humo bali ile isiyo na Chapa na iliyozidi kulingana na Eneo lililotengwa kwa malisho.

Operesheni okoa Bonde la Mto Kilombero iliyopangwa kuisha baada ya siku Nne itaendelea mpaka Viji vyote vyenye Mifugo mingi kubainika na ni zoezi endelevu.

Operesheni Okoa Bonde Tengefu la Kilombero yakabiliwa na changamoto


Henry Bernard Mwakifuna, Mchombe-Kilombero

KUTOKUWAPO kwa utaratibu mzuri unaotumika kuwasimamia ili kuhakikisha Wafugaji Wavamizi wanatoka nje ya Wilaya ya Kilombero imekuwa Changamoto mojawapo katika Operesheni Okoa Bonde la Kilombero.

Bwana Madaraka Amani, AfIsa Wanyamapori Wilaya ya Kilombero amewambia waandishi wa Habari waliotembelea operesheni hiyo kuwa wavamizi wanaotozwa faini na kuamriwa kuondoka nje ya Wilaya hii wamekuwa wanazunguka zunguka ndani ya Wilaya hiyo na kisha kurudi kufuatia kutokuwapo Utaratibu mzuri.

Amesema kuna tetezi za suala hilo na Watakaobainika watapelekwa moja kwa moja Mahakamani kwani watakuwa wamevunja Sheria na kukiuka maagizo ya Serikali.

Ameongeza kuwa Wafugaji Wavamizi awali waliekezwa waende Lindi  ambapo walitengewa maeneo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bwana Said Mecky Sadiq kwa zaidi ya Ng’ombe Laki moja ambapo Takwimu zinaonesha ni N’gombe Elfu Ishirini na mbili tu ndiyo walioenda huko.

Sababu kubwa anabainisha Bwana Madaraka ni kuwa Bonde la Kilombero lina malisho bora yenye Virutubisho kwa Mifugo inayopelekea Mifugo kama N’gombe kuzaa kila Mwaka hivyo kupelekea Wafugaji kukahidi kuondoka.

Wakati huo huo, Bwana Madaraka Amani amesema kuwa Sheria Tisa zinatumika katika operesheni okoa Bonde Tengefu la Kilombero.

Amezitaji Sheria hizo kuwa ni  Sheria ya Mazingira, Sheria ya Wanyamapori, Sheria ya Misitu na Sheria ya Ardhi ya Vijiji.
Nyingine ni Sheria ya Uhamishaji wa Mifugo, Sheria ya Kuweka Alama Mifugo na Sheria ya Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi.

Operesheni Okoa Bonde Tengefu la Kilombero lenye Ukubwa wa Kilometa 7,697 likihusisha Vijiji 228 limeanza Tangu Mwishoni mwa Mwezi Uliopita na katika Wilaya ya Kilombero ilianzia katika Tarafa ya Mlimba na kwa sasa ipo Kata ya Mchombe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana Elias Masala amesema kuwa Sheria kuu zinazotumika katika Operesheni hii ni ile ya Wanyamapori kipengele cha 116 (2) kisemacho Afisa amepewa kutoza faini ya kiwango kisichopungua Elfu 20 na kisichozidi shilingi Milioni 10 kwa kosa moja.

Sheria ndogondogo za Kilimo na Mifugo chini ya Halmashauri za mwaka 2007 sheria kifungu cha 10 kinachosema faini isizidi shilingi Laki Tatu ni sheria ya pili inayotumika katika operesheni Okoa Bonde la Kilombero.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa sasa wanatoza Faini ya Kati ya Shilingi Elfu 10 na Elfu 40 kwa kosa moja.

Operesheni Okoa Bonde Tengefu la Kilombero yakabiliwa na changamoto


Henry Bernard Mwakifuna, Mchombe-Kilombero

KUTOKUWAPO kwa utaratibu mzuri unaotumika kuwasimamia ili kuhakikisha Wafugaji Wavamizi wanatoka nje ya Wilaya ya Kilombero imekuwa Changamoto mojawapo katika Operesheni Okoa Bonde la Kilombero.

Bwana Madaraka Amani, AfIsa Wanyamapori Wilaya ya Kilombero amewambia waandishi wa Habari waliotembelea operesheni hiyo kuwa wavamizi wanaotozwa faini na kuamriwa kuondoka nje ya Wilaya hii wamekuwa wanazunguka zunguka ndani ya Wilaya hiyo na kisha kurudi kufuatia kutokuwapo Utaratibu mzuri.

Amesema kuna tetezi za suala hilo na Watakaobainika watapelekwa moja kwa moja Mahakamani kwani watakuwa wamevunja Sheria na kukiuka maagizo ya Serikali.

Ameongeza kuwa Wafugaji Wavamizi awali waliekezwa waende Lindi  ambapo walitengewa maeneo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bwana Said Mecky Sadiq kwa zaidi ya Ng’ombe Laki moja ambapo Takwimu zinaonesha ni N’gombe Elfu Ishirini na mbili tu ndiyo walioenda huko.

Sababu kubwa anabainisha Bwana Madaraka ni kuwa Bonde la Kilombero lina malisho bora yenye Virutubisho kwa Mifugo inayopelekea Mifugo kama N’gombe kuzaa kila Mwaka hivyo kupelekea Wafugaji kukahidi kuondoka.

Wakati huo huo, Bwana Madaraka Amani amesema kuwa Sheria Tisa zinatumika katika operesheni okoa Bonde Tengefu la Kilombero.

Amezitaji Sheria hizo kuwa ni  Sheria ya Mazingira, Sheria ya Wanyamapori, Sheria ya Misitu na Sheria ya Ardhi ya Vijiji.
Nyingine ni Sheria ya Uhamishaji wa Mifugo, Sheria ya Kuweka Alama Mifugo na Sheria ya Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi.

Operesheni Okoa Bonde Tengefu la Kilombero lenye Ukubwa wa Kilometa 7,697 likihusisha Vijiji 228 limeanza Tangu Mwishoni mwa Mwezi Uliopita na katika Wilaya ya Kilombero ilianzia katika Tarafa ya Mlimba na kwa sasa ipo Kata ya Mchombe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana Elias Masala amesema kuwa Sheria kuu zinazotumika katika Operesheni hii ni ile ya Wanyamapori kipengele cha 116 (2) kisemacho Afisa amepewa kutoza faini ya kiwango kisichopungua Elfu 20 na kisichozidi shilingi Milioni 10 kwa kosa moja.

Sheria ndogondogo za Kilimo na Mifugo chini ya Halmashauri za mwaka 2007 sheria kifungu cha 10 kinachosema faini isizidi shilingi Laki Tatu ni sheria ya pili inayotumika katika operesheni Okoa Bonde la Kilombero.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa sasa wanatoza Faini ya Kati ya Shilingi Elfu 10 na Elfu 40 kwa kosa moja.

Operesheni Okoa Bonde la Mto Kilombero yasababisha Kifo


Na Senior Libonge,Kilombero

WAKATI zoezi la kuondoa mifugo vamizi katika bonde tengefu la Kilombero likiendelea,zoezi hilo limeingia dosari baada ya mfugaji mmoja kudaiwa kuuawa na polisi wanaoendesha zoezi hilo .

Tukio la kuuawa kwa mfugaji huyo limetokea juzi katika kijiji cha Udagaji kata ya Chita wilayani Kilombero baada ya kundi la wafugaji kuwavamia askari na kuanza kuwapiga lengo lao ni kuwanyang’anya mifugo iliyokamatwa katika operesheni hiyo.

Akizungumza na gazeti hili diwani wa kata ya Chita Hassan Kidapa amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea juzi majira ya jioni katika kijiji hicho cha Udagaji baada ya kundi la wafugaji kuwavamia askari waliokamata kundi la ng’ombe wanaofikia 300 walioingia katika kijiji hicho kinyemela ili kuficha mifugo yao .

Kidapa amesema siku ya tukio baada ya askari kukamata mifugo hiyo iliyokuwa imefichwa katika moja ya msitu katika kijiji hicho waliikusanya katika kundi moja ili kuipeleka katika kambi maalum za kuhifadhi mifugo iliyokamatwa mara wakatokea jamii ya wafugaji wachache na kumpiga askari mmoja aliye na silaha kwa kutumia fimbo na alipoanguka chini waliamua kuondoka na kwenda kuita wenzao ili wachukue mifugo hiyo.

Amesema baada ya kupeana taarifa liliibuka kundi kubwa la wafugaji huku wakiwa na silaha za jadi lengo ni kupora ng’ombe hao waliokamatwa lakini walipofika katika uwanja wa mpira wa shule ya Udagaji walikutana na askari walioongezeka na walipewa tahadhari kwamba wasisogee eneo hilo lakini wafugaji hao walikaidi amri ya polisi na kusogelea mifugo na ndipo askari waliporusha risasi hewani ili kuwatawanya lakini waliendelea kukaidi.

Diwani huyo amesema kuwa baada ya kuona kuwa wafugaji hao wamekaidi amri halali ya polisi ya kutosogelea eneo la mifugo hiyo mmojawapo alipigwa risasi ya mguuni lakini bado walikaidi na kuendelea kuwasogelea askari na ndipo marehemu alipopigwa risasi ya kiunoni na kufariki dunia.

Hata hivyo diwani huyo amesema kuwa hadi jana jioni jina na mahali alipotokea marehemu bado havijajulikana kwani ni wafugaji wageni walioingia na kujificha katika kijiji hicho kwa lengo la kukimbia operesheni inayoendeshwa kwa nguvu ya kuondoa mifugo katika bonde lote la Kilombero na kijiji hicho hakina historia ya kuwepo kwa mifugo.

Kidapa amesema mifugo iliyokamatwa imepelekwa katika kambi maalum ya kuhifadhi mifugo iliyopo Mngeta na hivi sasa katika kata ya Chita hali sio shwari kwani jamii ya wafugaji wanaendelea kuwatisha viongozi akiwemo afisa mtendaji wa kata kwa madai kuwa ndio waliosababisha mwenzao kuuawa.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na yeye yupo katika operesheni hiyo akifuatilia zoezi linavyoendelea na kusema kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakaidi kutekeleza maagizo ya askari punde wanapotakiwa kufanya hivyo.

Shilogile amewataka wafugaji na wananchi wote kiujumla katika operesheni hiyo kutii sheria punde wanapoagizwa na kueleza kuwa wao kama askari toka ianze operesheni hiyo wanaiendesha kiustaarabu ila kuna watu wachache wanaotaka kulipaka matope jeshi hilo kwa kukaidi amri halali za kipolisi.

Wednesday, November 7, 2012

Wananchi na Mizigo wakiwa kwenye Canter
Wananchi wakivuka katika Kivuko cha mto Kilombero
Mifugo ikiwa imeifadhiwa katika eneo la kiwanja cha mpira jirani na Ofisi ya Kata ya Mngeta



MIFUGO ELFU 52 KUONDOLEWA WILAYANI KILOMBERO


Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero.




Ng'ombe wakiwa wanaondoka kutoka maeneo ya Bonde Tengefu la Kilombero, pichani Mfugaji akiwa ametangulia mbele eneo la KIjiji cha Njage, Wilayani Kilombero.


JUMLA ya Mifugo Elfu Hamsini(52,000) na Mbili inatarajiwa kuondolewa katika Bonde la Hifadhi la Kilombero.

Akizungumza Ofisini kwake  na Wanahabari waliokuwa wakitembelea Zoezi la Operesheni Okoa Bonde la Kilombero, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana Hassan Masala amesema kuwa mpaka kufikia sasa Mifugo Elfu 21,375 imeuzwa na wenye mifugo katika Minada ya maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa kuhifadhia mifugo iliyokamatwa.

Mifugo 3,546 imetozwa Faini, kila mfugo umetozwa shilingi Elfu 10 huku Mifugo 2,565 imesafirishwa nje ya Wilaya ya Kilombero.

Lengo kubwa la Operesheni Okoa Bonde la Kilombero ni kuhakikisha Mifugo yote iliyozidi kuondoka katika Bonde Tengefu la Kilombero.

Amesema Changamoto kubwa inalolikumba zoezi hili  ni faini kuonekana si Tatizo kwa Wafugaji na Halmashauri kupitia Sheria ndogo ndogo imepandisha  Faini mpaka kufikia shilingi Elfu 20 kwa Ng’ombe.

Ameongeza kuwa operesheni ilipangwa kufanyika kwa siku 4 lakini kutokana na Ugumu wa kazi yenyewe imeongezwa siku  mpaka vijiji vyote vyenye idadi kubwa ya Mifugo vitakapopitiwa.

Operesheni okoa bonde la Kilombero ilifunguliwa Tarehe 30 mwezi Oktoba Rasmi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bwana Said Mecky Sadiq na ukamataji Rasmi ulianza Oktoba 31.

Sunday, November 4, 2012

MILIONI 81 KUWANUFAISHA WAKAZI WA KILOMBERO


Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero.

WANACHAMA 927 wa Mfuko wa Mzunguko wa Shirika lisilo la Kiserikali la Camfed wana akiba ya  jumla ya Shilingi 81,964,000 ambazo zipo kwa ajili ya kukopeshana.

Bi.Tukaeje Habibu, Afisa Mradi Camfed Tanzania, akitoa Taarifa ya Mwaka ya Mfuko wa Mzunguko amesema Wanachama hao wana Jumla ya Shilingi Milioni 32.4 na Camfed imewapatia msaada wa Shilingi milioni 49,520,000.

Amesema kuwa mfuko huo umeweza kuwanufaisha Wanachama kutoka Wilaya Kumi nchini Tanzania na tayari wanachama wameanza kuchukua Mikopo kutoka  kwenye Mfuko huo.

Ameongeza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni baadhi ya Viongozi wa Vikundi vinavyofadhiliwa na Shirika hilo kula fedha huku akizitaja Wilaya za Kilolo, Kilosa na Kilombero zikiongoza kwa Utafunaji wa Fedha hizo.

Kwa upande wa Kilolo Viongozi Watatu wametafuna Jumla ya Shilingi Milioni 2,140,000, kwa upande wa Kilombero kiongozi mmoja ametafuna 453,000 na  Kilosa kiongozi mmoja ametafuna Laki 190,000. 

Kwa upande wake Nasikiwa Duke, Afisa Mradi wa Young Women wa Shirika la Camfed akitoa Ripoti ya Mwaka amesema kuwa Shirika hilo mpaka sasa linafanya kazi na Shule 540 likiwa na Miradi aina mbili ambayo ni kumsaidia Mtoto wa Kike na kumwendeleza kiuchumi.

Viongozi hao wa Camfed Shirika lenye Makao Makuu Nchini Uingereza linalofanya kazi na Nchi Tano kwa sasa ikiwemo Tanzania waliyasema hayo walipokuwa katika Mkutano wa Mwaka uliofanyika Ifakara, Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na Wanachama kutoka Wilaya Kumi nchini Tanzania.

MILIONI 544 ZAKUSANYWA KAMA USHURU JULAI-SEPTEMBA WILAYANI KILOMBERO


Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero.

JUMLA ya Shilingi Milioni 544 sawa na Asilimia 84.8 ya lengo zimekusanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero  kutokana na Ushuru katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu huku lengo likiwa ni kukusanya Shilingi Milioni 647.

Taarifa ya Kamati ya Fedha iliyotolewa katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi hivi Karibuni imeeleza kuwa ukusanyaji wa ushuru katika wilaya hiyo umeshuka .

Katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, Halmashauri hiyo imekusanya ushuru kutoka kampuni ya Kilombero Plantation Limited (KPL)  iliyopo kata ya Mngeta shs. milion 16 tu wakati lengo lilikuwa kukusanya shs. milion 30 kila mwezi.

Taarifa hiyo imezidi kueleza kwa upande wa Minada katika kipindi hicho Halmashauri hiyo imekusanya ushuru shs. milion 2 tu, lengo lilikuwa kukusanya shs. milion 7, ushuru wa Soko imekusanya shs. milion 3 wakati lengo ilikuwa kukusanya shs. milion 23, ushuru wanyumba za kulala wageni imekusanya shs. milion 17,748,050 ni sawa na asililimia 17 lengo lilikuwa kukusanya shs. milion 98,776,000|= na ushuru wa miwa imekusanya shs. milion 18 ni sawa na asilimia 14 lengo lilikuwa kukusanya shs milion 127.

Wakati huo huo Wajumbe wa Baraza hilo wamewataka Maafisa Watendaji wa Kata 21 waliopo katika Wilaya ya Kilombero kufanya kazi ya ziada ya kukusanya ushuru ili kuiletea mapato makubwa Halmashauri hiyo ili iweze kuleta maendeleo kutokana na miradi inayopangwa kutekelezwa.

Wamesema Watendaji wa Kata mwishoni mwa mwaka jana wamepewa Pikipiki ili kufuatilia ukusanyaji wa ushuru katika kata zao lakini matokeo yake mapato yatokanayo na ushuru yameshuka.

Kati ya Kata 21, Kata za Idete na Mofu kwa muujibu wa Taarifa ya Kamati ya Fedha  hazikufanya Vizuri katika Zoezi la Ukusanyaji Ushuru katika Kipindi hicho cha Julai hadi Septemba.

Mbali ya hilo Wajumbe wa Kamati ya Fedha wametakiwa kubuni mbinu mbadala ya kuingizia mapato Halmashauri ya Wilaya, huku kamati hiyo ya Fedha ikitoa Pendekezo la  kulirudisha geti la Idete ili mapato yaweze kuongezeka, lakini wajumbe wa Baraza hilo wamekataa pendekezo hilo.

KITONGOJI CHA IFAKARA CHAVUKA LENGO MICHANGO YA MAENDELEO


Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero

Kitongoji cha Ifakara mjini katika Kipindi cha Julai hadi Oktoba kimevuka lengo kwa ukusanyaji wa michango ya maendeleo kutoka kwa jamii kwa muujibu wa Taarifa ya Kamati ya Maendeleo ya Kata.

Taarifa ya Michango ya Maendeleo ya Kata ya Ifakara Mjini kwa mwaka huu, iliyotolewa katika kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata(KMK) cha Hivi Karibuni, imeeleza kuwa kitongoji cha Ifakara mjini Kimepangiwa kukusanya michango ya maendeleo kutoka kwa Jamii shs.4,776,000/= kutoka nguvu kazi 1,592 iliyopo, lakini iimekusanya jumla ya shs.4,974,000/=na kuvuka lengo la shs.198,000/=.

Taarifa hiyo imezidi kueleza kuwa kitongoji cha Mkuya kimekusanya mchango  wa maendeleo kutoka kwa jamii shs. 1,806,000/= wakati lengo walilopangiwa ni kukusanya shs.1,812,000/= kutoka nguvu kazi 604 iliyopo katika kitongoji hicho.

Kitongoji cha Nduna kwa Muujibu wa Tarifa,hakijafanya vizuri katika zoezi la ukusanyaji wa Michango ya Maendeleo, ambapo lengo wamepangiwa kukusanya shs.5,235,000/= kutoka nguvu kazi 1745 iliyopo katika kitongoji hicho, lakini imekusanya jumla ya shs.2,766,000/= na inadaiwa shs.2,469,000/= ambazo bado hazijachangwa.

Taarifa inaonesha Kitongoji cha Nduna kina nguvu kazi 823 ambayo bado haijachangia michango yao ya Maendeleo hadi kufikia Oktoba 15 mwaka huu.

ZAIDI YA MILIONI 6 ZAHITAJIKA KUMALIZA MADARASA SEKONDARI LUPIRO


Henry Bernard Mwakifuna, Lupiro-Ulanga

JUMLA ya Shilingi Milioni  6,900,000/ zinahitajika kwa ajili ya umaliziaji wa Madarasa Mawili katika shule ya Sekondari Lupiro iliyopo katika kata ya Lupiro Wilayani Ulanga.

Diwani wa Kata hiyo Bwana Nassoro Mchalange, amesema kuwa fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya umaliziaji wa madarasa mawili ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Amesema kuwa kukamilika kwa Madarasa hayo kutatoa fursa kwa Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza ambao wanatarajiwa kujiunga mwezi Januari mwaka 2013 .

Kutokana na kuishiwa kwa fedha za umaliziaji wa Madarasa hayo Bwana Mchalange ameiomba Halmashauri ya Wilaya kuwasaidia fedha hizo ili waweze kukamilisha lengo hilo kwani hatua iliyobakia ni kupiga lipu ili madarasa yaweze kuwa tayari kutumika.

Saturday, November 3, 2012

Hali ya upatikanaji wa Mafuta yawa shwari Kilombero


Na Senior Libonge,Kilombero

HALI ya upatikanaji wa nishati ya mafuta katika wilaya ya Kilombero imerudi kama kawaida kwa bidhaa hiyo kuanza kupatikana baada ya kuadimika kwa wiki moja sasa.

Kukosekana kwa nishati hiyo muhimu ikiwemo Petrol,Diseli na mafuta ya taa kulisababisha walanguzi kupandisha bei ya mafuta kwa bei wanayotaka wao na ilipelekea bei ya petrol kufikia shilingi 5000 badala ya bei halisi ya shilingi 2360.

Bei ya petrol ilikuwa juu zaidi hasa baada ya kutumiwa na wananchi wengi hasa waendesha pikipiki maarufu Bodaboda ambapo na wao ilipelekea kupandisha nauli ya safari kutoka shilingi 1000 hadi kufikia shilingi 2000.

Licha ya kupanda kwa bei huko na bidhaa hizo kuuzwa kwa kificho jeshi la polisi liliendelea na msako wa kuwakamata walanguzi hao ambao wengi wao walificha bidhaa hiyo kwenye nyumba zao bila kuhofia hatari ya kulipuka na kusababisha moto katika nyumba hizo.

Kutokana na tatizo hilo wengi wa wananchi wilayani hapo waliwalaumu wamiliki wa vituo vya mafuta kuwa walikuwa wanakataa kwa makusudi kuyatoa mafuta ambayo yalikuwemo kwenye matanki yao kwa kutaka yapandishwe bei na wao wayatoe huku wengine wakisema kuwa pia wamiliki hao walikuwa wakiwatumia walanguzi kwa kuwapa mafuta nyakati za usiku ili asubuhi wayauze kwa bei ya juu.

Kwa upande wao wamiliki wa vituo vya mafuta wote kwa pamoja baada ya kuhojiwa walisema kuwa kukosekana kwa bidhaa hiyo Dar es Salaam ndiko kulikofanya wao wakose nishati hiyo na pia kukanusha kuwa hawakuwa wakitoa mafuta kinyemela kwa ajili ya kuwapatia walanguzi ili wawauzie kwa bei ya juu.

Hata hivyo huduma hiyo imerudi katika hali ya kawaida tokea Novemba 3 ambapo mafuta yameanza kuuzwa katika vituo vya mafuta katika mji wa Ifakara na katika tarafa ya Kidatu huduma hiyo ilianza kupatikana tokea Novemba 1 mwaka huu.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia misururu mirefu wa magari na pikipiki katika moja ya kituo cha mafuta Ifakara na wengi wao walisema kuwa licha ya kujaza matenki ya vyombo vyao vya moto pia wataweka akiba kwani hawawaamini tena wamiliki wa vituo vya mafuta na kuhofia kuwa watawadanganya na kuwaeleza kuwa yamekwisha kumbe wamehifadhi kwenye matanki yao.