HONGERA ULANGA COMMUNITY RESOURCE CENTRE

photos

Welcome to UCRC

About Me

Ulanga Community Resource Centre is a not-for-profit company limited by guarantee which was initiated with the aim of capacitating the resident peoples of Ulanga and Kilombero Districts and Tanzania in general to secure the right information and hold their duty bearers accountable in a bid to promote sustainable community development. UCRC as well aims at promoting educational activities in Ulanga District through facilitation of necessary educational resources in the area which include well equipped libraries and study centers. UCRC also works on land and natural resource rights for the marginalized rural people in Tanzania which also include sustainable use of such resources. It also provides legal aid and assistance to the poor, particularly women, children, the disabled and other disadvantaged groups in the society on different themes including land and gender.

Monday, December 31, 2012

TANZIA- MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero afariki dunia


Na Senior Libonge,Kilombero

MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero Ramadhani Kiombile amefariki katika hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Taarifa ambazo zimethibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Jackson Mpankuli zimesema kwamba Kiombile amefariki jana (leo) saa 6 mchana katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mpankuli alisema Mwenyekiti huyo alikuwa anaumwa huku akikataa kueleza ugongwa uliokuwa ukimsumbua na kwamba sababu zilizopelekea  kifo chake zitaelezwa baadaye baada ya madaktari wa hospitali hiyo kuufanyia uchunguzi mwili huo.

Mkurugenzi huyo alisema kwa upande wa suala la maziko bado ni mapema kulizungumzia na kwamba watalitolea ufumbuzi baada ya kumalizika kwa kikao cha pamoja kati ya viongozi wa serikali na halmashauro.

Taarifa za kifo cha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero kimestua wakazi wengi wa wilaya hiyo ambao wengi wao wamekaa katika makundi makundi na wakijadili baada ya kupata taarifa hiyo huku wengi wao wakiwa hawaamini.

Baada ya kupata taarifa za msiba huo kila mwananchi wa wilaya ya Kilombero amekuwa akimpigia simu mwenzie ili kupata ukweli wa kifo hicho na baada ya kupatwa ukweli kila mmoja amekuwa na majonzi hasa kutokana na uwajibikaji wa mwenyekiti huyo kijana.

 

Marehemu Kiombile licha ya kuwa mwenyekiti  wa kwanza mdogo kuongoza halmashauri hiyo pia alikuwa diwani wa kata ya Ifakara kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).

Atakumbukwa kwa mengi hasa ushirikiano kati yake na vijana katika kata yake na wilaya yote kiujumla pia msimamo wake ambapo alikuwa ahofii kumwambia mtu ukweli pale anapopata taarifa fulani ambayo inataka kurudisha nyumba maendeleo ya wilaya ya Kilombero.

Pia Kiombile anaheshimiwa baada ya kusimamia utengenezaji wa barabara za mitaa ya kata nzima ya Ifakara ambayo kwa hivi sasa zinapitika kwa msimu mzima na pia zinarahisisha mgeni yeyote anaeingia katika mji mdogo wa Ifakara kufika popote atakapo punde atakapoulizia.

Licha ya hayo pia marehemu alikuwa akisaidia watu wa aina mbalimbali wanaofika katika ofisi yake wakihitaji msaada wa fedha kwa ajili ya matibabu,shule na shida mbalimbali ambapo yeye alitoa fedha zake mfukoni na kuweza kuwasaidia.

Wakizungumza na gazeti hili wakazi wa mji wa Ifakara wamesema kuwa wilaya imempoteza kijana mchapakazi ambaye uwezo wake ulikuwa unahitajika zaidi hasa baada ya kufanya mambo makubwa punde alipopata vyeo hivyo vya uwenyekiti na udiwani.

Hiyari Bohari mkazi wa Ifakara amesema yeye baada ya kupata taarifa ilibidi akae kimya na kutoamini hasa kutokana na ukaribu alionao kati yake na mwenyekiti huyo hata kabla hajawa diwani na nafasi ya uwenyekiti.

 

“Unajuwa huwezi amini unapopata taarifa za ghafla kama hizi hasa kutokana na ukaribu wa mtu mwenyewe kwani marehemu nilikuwa nae karibu sana wakati tukiwa pamoja katika shughuli za usambazaji wa pembejeo na yeye kusema kuwa anaamua kuingia katika siasa na kweli dhamira yake ilifanikiwa kwa kupata udiwani na uwenyekiti,”alisema Hiyari.

Naye John Torogo mkazi wa Kidatu wilayani hapa alisema kuwa kifo cha Kiombile ni pigo kwa vijana wote wa wilaya hiyo kwani alikuwa mpiganaji wa kweli bila kuhofia mtu wala chama kwani alikuwa akisimamia haki katika kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi katika wilaya ya Kilombero.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo David Ligazio alisema kuwa aamini mwenyekiti wake amefariki dunia kwani mara kwa mara alikuwa akiwasiliana na mtu wa karibu aliyekuwa akimuhudumia na kumuelezea kuwa afya yake inaimarika ila alipopigiwa simu na kaimu mkurugenzi pamoja na mkuu wa wilaya nguvu zote zilimuishia.

Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilombero Abdallah Kambangwa amesema kuwa naye ameshtushwa na habari za msiba huo kwani marehemu alikuwa akishirikiana nae vizuri ndani ya kazi za chama na za nje ya chama akimchukulia kuwa ni mdogo wake hivyo asingekubali apotosheke wakati yeye yupo

 

Monday, December 17, 2012

JKT Chita wapewa somo


Na Senior Libonge,Kilombero

WITO umetolewa kwa askari wa kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT Chita) kujiwekea malengo yao hasa katika suala la elimu ili kuweza kutimiza ndoto zao pamoja na za familia zao.

Akizungumza na askari hao katika tafrija ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya sambamba na kumpongeza mkuu wa kikosi hicho Meja Msabaha Yamawe kwa kupata shahada ya pili ya uzamili ya uhasibu na fedha,mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala amesema kuwa moja ya majukumu ya kutimiza malengo yako ni kupata elimu.

Masala amesema kinachofanyika hivi sasa kwa askari nchini ni kubweteka baada ya kupata ajira bila kufahamu kuwa kujiendeleza kwa elimu ni kupiga hatua moja zaidi ya maisha hasa katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia.

Amempongeza mkuu wa kikosi hicho kwa kujiendeleza na kupata shahada ya pili bila kuridhika na mamlaka makubwa ya kuwaongoza wenzie na kusema kuwa kiongozi huyo amekuwa mfano mzuri kwa wenzie hivyo na askari waliopo chini yake pia waige mfano huo.

Masala amemtaka mkuu huyo wa kikosi kunufaisha wenzake kwa elimu aliyoipata na kuwa mfano bora kwa wafanyakazi wenzie na familia yake na hasa kuwaruhusu wale wote wanaotaka kujiendeleza ili mradi wafuate sheria za kijeshi.

Naye meja Yamawe amemuhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa elimu aliyoipata ataitumia kwa faida ya jeshi na taifa kiujumla na kusema kuwa alikwisha anza na anaendelea na mwenendo wa kuruhusu askari wengine wajiendeleze kwani faida ya elimu atakayoipata itamsaidia yeye,jeshi na taifa.

Meja Yamawe amesema yeyote anaetaka kwenda kusoma amjulishe nay eye atahakikisha anafanikisha dhamira hiyo ila atakapomaliza lazima alete cheti chake na asiyeleta cheti atamfungulia mashtaka na kumfukuza jeshi kwani atakuwa amepoteza fedha za bure za serikali wakati kuna watu wengine wanahitaji huduma kama hiyo.

Hata hivyo mkuu huyo wa kikosi amesema kuwa licha ya kupata shahada ya pili bado ana kiu ya kusoma kwani anategemea kusomea shahada ya tatu ya uchumi hivi karibuni.

CCM Moro wakemea makundi


Na Senior Libonge,Kilombero

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Morogoro Inocent Kalogeris amesema kuwa atakula nae sahani moja mwanachama yeyote atakaebainika kuwa ni kinara wa makundi ndani ya chama hicho.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Kiungani wenye lengo la kuimarisha na kukijenga chama.

Kalogeris amesema kinachoichafua chama hivi sasa ni makundi yaliyopo ndani ya chama hicho nayayoendelezwa na wanachama wenye uchu wa madaraka na wao wana kina kila sababu za kuvunja makundi ndani ya chama kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Amewaagiza viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya matawi kuwachunguza wale wote wanaoendeleza makundi na watakaobainika watimuliwe ndani ya chama hicho nay eye lengo lake ni kupigana na kuhakikisha kuwa CCM hakiyumbi katika mkoa wa Morogoro.

Kuhusu baadhi ya viongozi wa vijiji kutosoma taarifa za mapato na matumizi,mwenyekiti huyo wa CCM mkoa amewataka wahusika kufuata taratibu  za kusoma taarifa hizo na atakaeshindwa kufuata taratibu hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Aidha Kalogeris alizungumzia zoezi la uondoaji mifugo katika bonde la Kilombero na kusema kuwa lengo la zoezi hilo ni kulinusuru bonde hilo na kutaka dola ifanye kazi yake bila kuhofia mtu na serikali ihakikishe inawapatia maeneo mbadala wale wote wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo katika eneo la Ramsar ili kuendeleza shughuli zao za kilimo.

Pia kiongozi huyo alitoa miezi 6 kwa halmashauri ya wilaya kuhakikisha kero ya maji ya maji katika mji wa Ifakara inakwisha na pia kutoa miezi 9 kwa halmashauri hiyo kufanikisha mpango wa wilaya kuwa na hospitali ya wilaya.

Awali mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala alitaja miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa kama ilani ya chama hicho na kikubwa zaidi kukanusha upotoshaji unaofanyika juu ya operesheni ya okoa bonde la Kilombero.

Masala amesema mpaka sasa ni mifugo laki 3 imeondolewa toka zoezi hilo lianze na linazingatia sheria na kusema kuwa wapo viongozi wanaoendesha kampeni za kupotosha wananchi wasiondoe mifugo na kusema kuwa wao hawatawaachia viongozi hao.

Amesema athari za kuwepo mifugo kwenye bonde hilo ni kubwa na wameongeza wiki 2na mwisho itakuwa Disema 24 mwaka huu ili kupitia upya kila eneo ili kukagua tena mifugo na hivi karibuni watatumia tena Helkopta katika ukamilishaji wa zoezi hilo.

Hata hivyo Masala alibainisha kuwa hata kama mifugo inayoendelea kukamatwa hivi sasa ikibainika kuwa ya kiongozi Fulani wao hawatasita kuikamata na kuipiga faini nay eye atakaechukizwa aende popote nayeye yupo tayari kupambana nae kwani yeye anafuata sheria bali hafanyi kazi ya kuropoka kwenye vyombo vya habari.

Saturday, December 15, 2012

Tulinde Misitu yetu na rasilimali adhimu, wananchi waaswa


Henry Bernard Mwakifuna, Ifakara-Kilombero.

Serikali imeahidi kwa dhati kabisa kusimamia Sheria za Uhifadhi wa Misitu .

Akifunga Warsha ya Siku Moja ya Uwasilishaji wa Hali Halisi ya Hifadhi ya Misitu ya Udzungwa, Bi Hawa Mposi Lumuli, Afisa Tarafa ya Ifakara amesema kwa Watumishi wa Idara ya Misitu wanaolegalega na kutosimamia ipasavyo Sheria, Kanuni na Taratibu na kukiuka maadili watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Amesema kuwa tegemeo kubwa la Serikali ni kuona wafanyakazi wa Idara hiyo wanazingatia maadili na kusaidia kuokoa, kuhifadhi na kutunza misitu.

Kwa upande wao watafiti kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) wamesema kuwa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa imeonekana ya Kipekee kwa Uhifadhi wa Wanyama muhimu na Adimu kama Swala waitwao Vinde na Vyura wa Kihansi.

Vinde, aina ya Swala adimu Misitu ya Asili ya Udzungwa.

Akiwasilisha Matokeo ya Utafiti wa Hali ya Msitu wa Udzungwa, Bwana Justine Gwegine ,Afisa Mtafiti  na Mtathimini wa Hali ya Misitu kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) amesema kuwa  Matokeo ya  ya utafiti wao yameorodhesha Jumla  ya aina za ndege 79 zilionekana na katika maeneo  ya Ikule, Chita Wilayani Kilombero na Illutila na Idegenda katika Wilaya ya Kilolo.

Amesema kuwa kati ya  aina 79  zilizoorodheshwa, aina 14  ambayo  ni asilimia 17 ni wale ndege adimu na pengine wanapatikana katika  tao la  mashariki pekee.


Mbega mweupe, kiumbe adimu anyepatikana katika msitu wa Udzungwa
Lengo la Uwasilishaji huo ni kufahamu hali ya Misitu na Bioanuai yake kwa ujumla ili kuisaidia Serikali Kupanga Mipango ya Kuisimamia Vizuri kutokana na Matokeo ya Tafiti.

Utafiti huo umefanyika kwa Siku 25 Mwezi Septemba na Oktoba mwaka jana ambapo Vijiji Vinne vya Wilaya za Kilolo na Kilombero zimehusika.







Msitu wa Hifadhi Asili wa Udzungwa wenye ukubwa wa Hekta  20,720 na ulianzishwa Mwaka 1929, unasimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania.



Tuesday, December 11, 2012

Mkuu wa Wilaya apania kuweka safi mji wa Ifakara


Na Igamba Libonge,Kilombero

KATIKA kuonyesha kukerwa na uchafu uliokithiri katika vizimba vya madampo madogo matatu yaliyopo katikati ya mamlaka ya mji mdogo wa Ifakara,mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala ametoa masaa 24 kwa viongozi wa mamlaka huo kuondoa uchafu huo la sivyo wahusika wote watawajibishwa kisheria.

Masala ametoa agizo hilo jana wakati alipotembelea na kujionea lundo kubwa la takataka zikiwa zimelundikana katika vizimba hivyo hivyo vitatu ambavyo ni vya stendi ya mabasi,stendi ya zamani na soko kuu la Ifakara.

Katika ziara hiyo sehemu ya kwanza kutembelea ilikuwa stendi ya mabasi ambapo wananchi walimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa licha ya wao kuchangia lakini wanashangaa taka hizo kuendelea kujaa na wanaosababisha kujaa huko ni majirani ambao utoa taka zao majumbani na kuzileta katika dampo hilo.

Sehemu ya pili kutembelea ilikuwa stendi ya zamani ambapo hapo alikuta takataka zimelundikana hadi barabarani na wakazi wa maeneo hayo walimweleza mkuu huyo kuwa wanashindwa kukaa katika maeneo yao hasa kutokana na harufu kali inayotoka katika dampo hilo.

Alipofika sokoni ndipo alipopata malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambapo wamedai kuwa licha ya kulipia ushuru kwa kila siku wanashangaa takataka hizo kuendelea kuwepo eneo hilo na malalamiko yao pamoja na kukosekana kw walinzi wenye silaha na geti walikwisha ueleza uongozi wa halmashauri kwa muda mrefu lakini hakuna mabadiliko.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo Shabani Gwazai ambaye alisema kuwa licha ya kukutana mara kadhaa na uongozi wa halmashauri kuhusu kutatua matatizo hayo hakuna jipya lililojitokeza na kusema kuwa kama ukiwepo ushirikiano wa pamoja kati ya wao kama wafanyabiashara na halmashauri tatizo la uchafu halitakuwepo sokoni hapo.

Awali kabla ya kutoa fursa ya maswali kwa wafanyabiashara taarifa ya afya ya kata ilisomwa na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo kutokuwa na vyombo vya usafirishaji taka vya uhakika,matumizi mabaya ya vizimba ikiwemo jamii kutupa vinyesi na mimba zilizotolewa mitaani na jamii kutumia watu wenye mtindio wa ubongo kutupa taka kwenye vizimba.

Changamoto nyinngine ni mwitikio mdogo wa jamii juu ya usafi wa mazingira na baadhi ya wanajamii kukaidi uondoaji wa takataka kwenye misingi ya barabara kwa madai kuwa shughuli hiyo ni ya halmashauri hata hivyo wamesema matumizi ya sheria ndogo za mamlaka ya mji mdogo itakuwa ufumbuzi mkubwa na suluhisho la tatizo hilo sugu.


Ndipo ilipofika zamu ya mkuu wa wilaya kuongeza na kutoa masaa 24 kwa taka zote zilizopo katika vizimba hivyo vitatu kuzolewa haraka na kama akiendelea kuziona wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Masala amesema ameaumua kufanya ziara ya kutembelea vizimba hivyo baada ya kupata malalamiko ya kukithiri kwa uchafu ukizingatia kuwa vizimba hivyo vipo katikati ya mji wa Ifakara ambao ndio kioo cha wilaya ya Kilombero kwani alikwisha toa agizo kwa watendaji wa mji huo wahakikishe kuwa uchafu usiwepo tena katika vizimba hivyo.

Amesema kuwa aimuingii akilini kuwa uchafu huo unaendelea kulundikana katika vizimba hivyo wakati wananchi na wafanyabiashara wanalipa ushuru hivyo kuutaka uongozi wa kata kubuni njia nyingine itakayosaidia kupunguza taka katika vizimba hivyo ikiwemo kuweka sheria za utupaji wa taka.

Hata hivyo Masala amemtaka mtendaji wa kata ya Ifakara kumkamata kisha kumfikisha kwenye vyombo vya sheria mtu yeyote atakaebainika kuwa anatupa taka nje ya vizimba vilivyowekwa na halmashauri.

Kwa upande wake bwana afya wa wilaya Mbonja Kasemba alisema kuwa katika bajeti ya mwaka huu idara ya afya imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika dampo kubwa la Kiogosi ili kuzuia wananchi kuzitoa taka punde zinapomwagwa na pia wanategemea kujenga kibanda kwa ajili ya walinzi eneo hilohilo la Dampo.

Tuesday, December 4, 2012

Utunzaji wa Mazingira sawa, Haki za Binadamu Je?


Na Senior Libonge,Ulanga

SERIKALI  imetakiwa kuhakikisha inafanyia marekebisho sheria za ardhi zilizopo, ili mashauri yanayohusu migogoro ya ardhi yaweze kushughulikiwa kwenye ngazi za vijiji na kata ardhi hizo zilipo badala ya kupeleka mashauri hayo ngazi za wilaya, mahakama kuu ama za rufaa, ambapo wakati mwingine imewafanya wananchi kupoteza haki zao kwa kushindwa kumudu gharama kubwa za uendeshaji.





Ushauri huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na Wananchi na viongozi wa Tarafa za Malinyi na Ruaha wilayani Ulanga Mkoani Morogoro, wakati wakichangia kwenye midahalo kuhusu uwazi na Uwajibikaji katika sekta ya ardhi, iliyoandaliwa na Umoja wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani Ulanga (UNGOKI) kwa ufadhili wa shirika la Foundation For Civil Society ambapo walitolea mfano iwapo ardhi hiyo itakuwa ikigombewa baina ya mwananchi wa kawaida na mwekezaji mkubwa, ni rahisi kwa mwekezaji kushinda shauri husika kutokana na uwezo mdogo wa mwananchi kufuatilia shauri husika kama inavyotakiwa na kukosa wazi haki zake stahili.



Wananchi hao pia walilalamikia mabaraza ya adrhi ya vijiji na kata kukosa nguvu za kisheria katika kushughulikia migogoro, hivyo kudharaulika katika maeneo yao, ambapo iwapo mlalamikiwa ataitwa na baraza hilo na kushindwa kufika, mabaraza hayo yamekosa nguvu kuwachukulia watuhumiwa hatua.

Katika midahalo hiyo ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ni “Uwazi na Uwajibikaji ni msingi wa maendeleo,wananchi hao walilalamikia mashauri ya ardhi kuandikwa kwa lugha ya kiingereza katika baraza la ardhi na nyumba, changamoto za mipaka katika vijiji vyao, wananchi kushindwa kushirikishwa katika masuala ya ardhi ikiwemo kupitisha majina ya watu wanaoomba maeneo, na gharama kubwa ya kufuatilia mashauri hasa yale yanayofikishwa ngazi za juu kama baraza la wilaya, mahakama kuu na mahakama ya rufaa.





Baadhi ya wananchi hao Omary Ibrahim, Stephen Kasasi,Dvodius Mlungachuma,Edward Lupogo na Agnes Mpangule walilalamikia wageni kupewa ardhi tena maeneo makubwa katika maeneo yao, bila kushirikisha ugawaji huo katika mikutano ya vijiji, jambo linalowanyima haki wakazi husika,na viongozi wengine kutumia nyadhifa zao kujimilikisha maeneo makubwa, jambo linalochochea migogoro miongoni mwa wananchi.

Aidha Stephen Kasasi Lugumey na wenzake kutoka Kijiji cha Makelele walilalamikia eneo lao la kijiji kuwa dogo na hivyo kushindwakufanya matumii bora ya ardhi, ikilinganishwa na vijiji vidogo, hivyo kuhoji ukubwa wa eneo la kijiji unapaswa kuwa vipi na kwamba ni vyema vijiji vikapimwa upya na kugawanywa kwa mlingano ulio sawa. .

Nao wanavijiji wa Tarafa ya Ruaha, Kanusian Nkasi,Medist Zimani,Todros Katanda,Ezekiel Maridadi,Renfrida Pesa na Williama Kologati, pamoja na kulalamikia madai kama yalivyojitokeza Malinyi, walihoji mpango wa matumizi bora ya ardhi kuchelewa kufanywa sasa, kutokana na kuwa tayari wananchi wameshajimilisha maeneo na kutishia ubora wa mpango huo.




Wakitoa mada kwa nyakati tofauti katika midahalo hiyo, Mratibu wa UNGOKI, Maiko Chami,mjumbe wa umoja huo Ansagar Kwanja na mtoa mada Mohamed Nguku,waliwaasa wananchi kushiriki mikutano ya vijiji ili kutoa mapendekezo, maoni na ushauri juu ya bajeti za vijiji, mpango wa matumizi bora ya ardhi na changamoto na mahitaji mengine muhimu yanayoyakabili maeneo yao.

Chami aliwashauri kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali kuwezesha kufanya matumizi bora ya ardhi kufikia vijiji 38 kati ya 91 vya wilaya ya Ulanga, ni vyema vijiji vingine vikapitisha maamuzi ya kutaka mpango huo kwenye mikutano yao ya vijiji na hata kuomba wahisani na mashirika mbalimbali kusaidia uwekaji wa mipango hiyo, badala ya kuisubiri Serikali, huku akihimiza ushirikishwaji kuwa ni njia pekee na kubwa ya kutatua migogoro ya ardhi.

“Migogoro hii ya ardhi ikitatuliwa vijijini ni jambo zuri na jepesi kutatulika, kwa sababu ardhi ipo kwenu, kuliko kupeleka migogoro hii ngazi za juu, ni kweli bado kuna changamoto ya sheria za ardhi, kama kushindwa kutoa nguvu kisheria kwenye mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata, ambapo mlalamikiwa asipotokea kwenye shauri, baraza limekuwa likikosa nguvu kisheria kumchukulia hatua,lakini bado wanaharakati wanalipigia kelele”Alisema Mratibu huyo wa UNGOKI akijibu madai mbalimbali ya wananchi hao.

Nguku alisema halmashauri za vijiji hazina Mamlaka kisheria kugawa maeneo, na wanaopaswa kufanya hivyo ni wananchi kupitia mikutano ya vijiji huku akiwatahadharisha kuwa makini na ugawaji wa maeneo makubwa kwa wawekezaji, kwani wana hatari ya kukosa haki mbeleni iwapo wanaopewa maeneo watapata hati miliki na kutumia sheria hizo hizo za ardhi kuwalinda.

Wananchi walipitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo sheria za ardi namba nne na tano za mwaka 2004, sheria ya kijiji ya mwaka 1999, historia ya uwepo wa sheria za ardhi,migogoro inayojitokeza vijijini na mifumo inayotumika katika utatuzi na mpango wa usimamizi na matumizi bora ya ardhi.

Saturday, December 1, 2012

Jumla ya shilingi milioni 212,886,000 zakusanywa katika zoezi la kuondoa mifugo Bonde la Mto Kilombero


Na Senior Libonge- Ifakara

JUMLA ya shilingi milioni 212,886,000 zimepatikana ikiwa ni mapato ya uwekaji alama mifugo na faini katika zoezi la uondoaji mifuko katika bonde tengefu la Kilombero kwa wilaya ya Kilombero.

Akizungumza jana katika kikao cha kamati ya uashauri ya wilaya(DCC)Mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala amesema kuwa fedha hizo zimepatikana baada ya kuanza kwa zoezi la uwekaji alama lilianza Agosti 21 na kumalizika Septemba 30 mwaka huu na pia zoezi la faini kwa wafugaji waliokaidi amri halali lililoanza Oktoba 30 mwaka huu.

Masala amesema zoezi la kuweka alama mifugo inayostahili kubaki kulingana na ukubwa wa eneo husika lilihusisha vijiji vilivyopo ndani ya eneo la Ramsar na vilevile nje ya eneo hilo kwa kufanya mikutano mikuu ya hadhara kwa ajili ya utambuzi wa wafugaji halali na wanaotakiwa kubaki katika kila kijiji.

Alisema jumla ya ng’ombe 52,780 waliwekwa alama kwa gharama ya shilingi 1000 kwa kila ng’ombe na kupata jumla ya shilingi milioni 52,780,000 kama makusanyo ya zoezi hilo na kati ya hizo shilingi milioni 27,940,300 zilitumika kuendelea na zoezi hilo.

Amebainisha kuwa katika zoezi la uondoaji wa mifugo ambalo zoezi hilo bado linaendelea mpaka sasa jumla ya wafugaji 2,428 wenye ng’ombe wapatao 9,248 walitozwa faini kwa viwango mbalimbali kulingana na makosa waliyopatikana nayo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema jumla ya ng’ombe 3,482 walitozwa shilingi 10,000 na kupatikana shilingi milioni 34.8 huku ng’ombe 5,379 walitozwa shilingi 20,000 na kupatikana shilingi milioni 107.5,ng’ombe 264 walitozwa shilingi 40,000 na kupatikana shilingi milioni 10.5 na hiyo inafanya shilingi milioni 152.9 kuwa jumla ya mapato yaliyotokana na faini.

Masala amesema hata hivyo zoezi utoaji wa vibali vya kusafiria lilienda sambamba na zoezi hilo ambapo idadi ya ng’ombe 4764 walipatiwa vibali kwa gharama ya shilingi 1500 na shilingi milioni 7.1 zimekusanywa kama ruzuku ya serikali kuu.

Amesema fedha zilizoidhinishwa katika zoezi la uwekaji wa alama ng’ombe na uondoaji wa mifugo katika bonde tengefu la Kilombero ni shilingi milioni 152.7 na fedha iliyotumika hadi sasa ni shilingi milioni 94 na kufanya salio la shilingi milioni 14.1.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya amesema zoezi la kuondoa mifugo linaendelea japokuwa linakabiliana na changamoto mbalimbali ambazo wataalamu wanaendelea kukabiliana nazo

Gharama za Afya zapanda katika Hospitali ya St. Francis Ifakara


Na Senior Libonge,Kilombero

KUTOPATA fedha kwa wakati kutoka mfuko wa pamoja(basket fund)na mgawanyo mdogo toka bohari ya madawa nchini(MSD)ndiko kunakosababisha hospitali ya rufaa ya Mt.Francis iliyopo mjini Ifakara wilayani Kilombero kupandisha gharama ya matibabu.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya,mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk,Angelo Nyamtema amesema licha ya kutopata fedha kwa wakati na mgawanyo mdogo pia suala la ulipaji wa mishahara kwa wataalamu mbalimbali nayo uchangia hospitali hiyo kukosa fedha.
                
Dk,Nyamtema amesema licha ya changamoto hizo alizozitaja mkakati uliopo hivi sasa ni kuboresha huduma katika hospitali hiyo ili kuweza kufikia hadhi ya hospitali ya rufaa baada ya kupandishwa hadhi.

Amesema ni mwezi wa tano hivi sasa hawajapata fedha ya basket fund huku pia wakiwa hawajapata fedha toka serikalini tokea mwezi Julai mwaka huu ili kuweza kuagiza madawa na vifaa mbalimbali vya tiba kutoka bohari ya madawa nchini(MSD).

Mkurugenzi huyo wa hospitali ameiomba halmashauri ya wilaya na serikali kiujumla kushirikiana nao ili kutatua changamoto zinazowakabili hatimaye kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wanaotumia hospitali hiyo kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Amesema suala la mishahara limekuwa tatizo kwani kwa kipindi cha karibuni wametumia kiasi cha shilingi milioni 42 kwa ajili ya kulipa mishahara watumishi wake na fedha hizo zimetokana na fedha zinazotokana na gharama za uchangiaji zinazotozwa kwa wagonjwa.

Dk,Nyamtema ameiomba serikali kuwapatia wataalamu walioajiriwa na serikali ili wao waweze kupunguza mzigo mkubwa wa kuwalipa mishahara na hali hiyo itapelekea kupunguza gharama kwa wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo.

Hata hivyo mkurugenzi huyo amekanusha taarifa kuwa menejimenti ya hospitali uamua kupandisha gharama za matibabu wanapojisikia na kusema kuwa mawazo ya kupandisha gharama za matibabu sio ufanywa na uongozi wa hospitali bali ni kamati nzima inayowashirikisha watu kutoka serikalini,halmashauri ya wilaya na wadau mbalimbali.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilombero aliuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya chini ya mwenyekiti wake na mkurugenzi mtendaji kukaa pamoja na menejimenti ya hospitali hiyo ili kutatua matatizo mbalimbali hatimaye kuweza kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama za matibabu.