Na Senior Libonge, Ifakara
WAKATI familia ya aliyekuwa mbunge wa viti maalum
jimbo la Kilombero marehemu Regia Mtema ikiandaa tarehe 14 Januari mwaka huu
kuwa ni siku ya Regia kwa kuandaa hafla kubwa jijini Dar es Salaam,pia shughuli
maalum zitafanyika wilayani Kilombero ambapo ndiko marehemu alipokuwa
akitumikia wananchi wa jimbo hilo.
Aliyekuwa Mbunge wa Kilombero (Viti Maalum CHADEMA) Marehemu Regia Mtema |
Akizungumza na Blog blog hii mjini Ifakara,mratibu
wa shughuli hizo wilaya ya Kilombero Antony Kamonalelo amesema kuwa amepewa
jukumu hilo kutoka kwa famila ya marehemu ambao wameanzisha Regia Mtema
Foundation na shughuli kubwa zitakayofanyika wilayani hapa ni zoezi la upandaji
miti,usafi wa mazingira na matembezi ya mshikamano.
Kamonalelo amesema kuwa shughuli hizo zitaanza
tarehe 16 mwezi huu kwa wananchi kupanda miti na shughuli itaanza katika shule
ya msingi Maendeleo na siku inayofuata litafuatia zoezi la usafi wa mazingira
katika maeneo mbalimbali ya mji wa Ifakara na viunga vyake hasa katika vituo
vya kuhudumia watoto wenye matatizo mbalimbali,hospitali ya rufaa ya Mt.Francis
na soko kuu la Ifakara.
Kwa mujibu wa Kamonalelo tarehe 18 ndio itakuwa mwisho
wa shughuli hiyo ambapo kutakuwa na matembezi ya mshikamano yatakayoanzia
katika mzunguko wa Kibaoni na kuelekea katika makabuli ya kwa Mkuya katika
kijiji cha Lipangalala ambako ndiko alipozikwa na wakishafika hapo shughu
itakayofuatia ni kufanya usafina kisha kuwasha mishumaa ikiwa ni ishara ya
kumkumbuka kipenzi cha wana Kilombero.
Amesema shughuli zote hizo zitaongozwa na mkuu wa
wilaya ya Kilombero Hassan Masala hivyo kutoa wito kwa wananchi wote wilayani
Kilombero bila kujadi itikadi za kisiasa na kidini kujitokeza kwa wingi katika
shughuli zote za siku tatu kutokana na marehemu alikuwa mtu wa watu.
Huku shughuli za kumkumbuka marehemu Regia Mtema
zikitarajia kufanyika hivyo wilayani Kilombero jijini Dar es Salaam shughuli
maalum itafanyika Januari 14 katika hoteli ya Peacock ambapo Regia Mtema
Foundation wamesema kuwa kutakuwa na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na
kujadiliwa kama alivyozisimamia marehemu.
Taarifa zilizosambazwa kwa vyombo vya habari na
familia ya marehemu zimeeleza kuwa katika siku hiyo maalum wageni na wadau
mbalimbali wamethibitisha kushiriki na hafla itaanza saa 9 alasiri na
kumalizika saa 2 usiku katika hoteli ya Peacock na kisha kufuatiwa na chakula
cha usiku.
Kwa mujibu wa famila ya marehemu ratiba kamili
itahusisha matukio kadhaa yakiwemo historia ya Regia itakayowasilishwa na
Mbunge David Kafulila,mada juu ya rushwa itakayowasilishwa na Takukuru na
Ulemavu sio kutoweza itakayowasilishwa na Shida Salum mwenyekiti wa CHAWATA.
Pia Mh January Makamba atawasilisha mada ya nafasi
ya kijana katika kuchochea maendeleo na demokrasia,makala za Regia na pia
nasaha kutoka kwa wabunge Mh Zito Kabwe na John Mnyika,Hussen Bashe na
mzee Mtema zitatolewa.
Marehemu Regia Mtema alifariki kwa ajali ya gari
katika eneo la Ruvu Januari 14 mwaka jana baada ya gari alilokuwa akiliendesha
kupinduka na kusababisha kifo chake na baadaye kuzikwa mjini Ifakara katika
mazishi yaliyokusanya watu wengi yaliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
No comments:
Post a Comment