Na Senior Libonge,Kilombero
KITUO cha Utafiti wa Kilimo(KATRIN) kilichopo wilayani Kilombero mkoani
Morogoro kimeamua kuboresha mbegu ya mpunga aina ya Saro 5 kutokana
na mbegu hiyo kupendwa zaidi na wakulima wengi nchini hasa kutokana na mchele
wake kunukia vizuri.
Akizungumza na mkuu wa wilaya ya Kilombero baada ya kutembelea kituo
hicho,Kaimu afisa mfawidhi wa kituo Dk Jerome Mghase amesema wakulima wengi wa
mpunga nchini wanapendelea mbegu za Saro 5 kutokana na mchele wake kuwa na
uhakika wa soko na wao kwa kutambua hilo wameamua kuboresha mbegu hiyo.
AKINA MAMA WAKIPALIA MPUNGA KATIKA ENEO LA IGAWA, Picha kwa Hisani ya Juma Mtanda Blog Archieve |
Dk Mghase amesema hiyo yote inatokana na mafanikio ya utafiti wa zao la
mpunga ambapo licha ya kuboresha mbegu aina ya Saro 5 pia kituo kimewezesha
upatikanaji wa mbegu nyingine zilizoboreshwa zikiwemo TXD 85,TXD 88 na NERICA
za ukanda wa juu na milima zikiwemo Nerica 1 hadi 7 na pia WAB 450-12-2BL1-DV4.
Amesema pia kituo kimefanikiwa katika upatikanaji wa mbegu zenye
ukinzani dhidi ya ugonjwa wa kimyanga ambazo ni Kalalu na Mwangaza huku pia
teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa mpunga zimetolewa kwa wakulima zikiwemo
kupanda kwa nafasi,matumizi bora ya mbolea,kiwango cha mbegu za
kupanda,udhibiti wa magugu na muda muafaka baada ya kuvuna.
Kaimu afisa mfawidhi huyo ameendelea kusema kuwa kituo hicho kwa sasa
ni taasisi mahiri ya mpunga kwa ukanda wa afrika mashariki baada ya kuteuliwa
mwaka 2008 kupitia mpango ujulikanao kama Eastern Africa Agriculture
Productivity Program(EAAPP) na mradi huu unafadhiliwa na benki ya dunia.
Amesema katika mradi huo nchi ya Tanzania unahusisha zao la
mpunga,Kenya(Maziwa),Uganda(Mihogo) na Ethiopia(Ngano) na mradi huu
ulizinduliwa rasmi April 2010 na hadi sasa zaidi ya tafii 20 za kikanda
zinaratibiwa na KATRIN.
Kwa mujibu wa afisa huyo amesema kuwa kituo hicho kwa sasa kinazalisha
mbegu za mpunga ambazo huuzwa kwa wakala wa mbegu wa Taifa(ASA) ambao
huzizalisha kwa wingi na kuuza kwa wakulima nchi nzima na pia kituo kinawapatia
wakulima mmoja mmoja au kupitia vikundi kadri ya mahitaji yao.
Aidha kituo mbali ya utafiti wa zao la mpunga pia wamepewa jukumu la
kutafiti aimba mbalimbali za mazao ya viungo kama vile
Vanila,Tangawizi,Pilipili manga,Iliki,Mdalasini na Kokoa na utafii huo
utawezesha wakulima kupata mazao mbadala ya biashara mbali na mpunga ambao
hautoshelezi mahitaji yao ya kiuchumi.
Hata hivyo Dk Mghase amesema licha mafanikio hayo pia kituo hicho kina
changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ambazo ni idadi ndogo ya watafiti na
watumishi wengine,uchakavu wa miundombinu na vifaa,uvamizi wa maeneo ya kituo
na wanajamii wanaokizunguka na ukosefu wa huduma muhimu hasa afya.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala amesema kuwa
nchi nyingi zimeendelea kutokana na utafiti na wao kama serikali wana jukumu
kubwa la kuzalisha katika kilimo ila hawataweza kufanikiwa bila kuona wataalamu
wanashughulikiaje kilimo hicho.
Masala amesema serikali bado ina mkakati wa kuboresha taasisi zake
ikiwemo Katrin na kwa kuona hilo wameamua kukiteua kituo hicho ili kufanya
utafiti na kuzalisha mbegu bora zaidi ili kufanikisha mipango ya Famoghata na
Sagcot huku pia akiwataka wataalamu hao kuwapatia elimu wakulima ili waweze
kuzalisha mazao bora zaidi na kukuza vipato vyao.
No comments:
Post a Comment