Na Igamba Libonge,Kilombero
KATIKA
kuonyesha kukerwa na uchafu uliokithiri katika vizimba vya madampo madogo
matatu yaliyopo katikati ya mamlaka ya mji mdogo wa Ifakara,mkuu wa wilaya ya
Kilombero Hassan Masala ametoa masaa 24 kwa viongozi wa mamlaka huo kuondoa
uchafu huo la sivyo wahusika wote watawajibishwa kisheria.
Masala ametoa agizo hilo jana wakati alipotembelea
na kujionea lundo kubwa la takataka zikiwa zimelundikana katika vizimba hivyo
hivyo vitatu ambavyo ni vya stendi ya mabasi,stendi ya zamani na soko kuu la
Ifakara.
Katika ziara hiyo sehemu ya kwanza kutembelea
ilikuwa stendi ya mabasi ambapo wananchi walimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa
licha ya wao kuchangia lakini wanashangaa taka hizo kuendelea kujaa na
wanaosababisha kujaa huko ni majirani ambao utoa taka zao majumbani na kuzileta
katika dampo hilo.
Sehemu ya pili kutembelea ilikuwa stendi ya zamani
ambapo hapo alikuta takataka zimelundikana hadi barabarani na wakazi wa maeneo
hayo walimweleza mkuu huyo kuwa wanashindwa kukaa katika maeneo yao hasa
kutokana na harufu kali inayotoka katika dampo hilo.
Alipofika sokoni ndipo alipopata malalamiko mengi
kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambapo wamedai kuwa licha ya kulipia
ushuru kwa kila siku wanashangaa takataka hizo kuendelea kuwepo eneo hilo na
malalamiko yao pamoja na kukosekana kw walinzi wenye silaha na geti walikwisha
ueleza uongozi wa halmashauri kwa muda mrefu lakini hakuna mabadiliko.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa
wafanyabiashara wa soko hilo Shabani Gwazai ambaye alisema kuwa licha ya
kukutana mara kadhaa na uongozi wa halmashauri kuhusu kutatua matatizo hayo
hakuna jipya lililojitokeza na kusema kuwa kama ukiwepo ushirikiano wa pamoja
kati ya wao kama wafanyabiashara na halmashauri tatizo la uchafu halitakuwepo
sokoni hapo.
Awali kabla ya kutoa fursa ya maswali kwa
wafanyabiashara taarifa ya afya ya kata ilisomwa na kueleza changamoto
wanazokabiliana nazo ikiwemo kutokuwa na vyombo vya usafirishaji taka vya
uhakika,matumizi mabaya ya vizimba ikiwemo jamii kutupa vinyesi na mimba zilizotolewa
mitaani na jamii kutumia watu wenye mtindio wa ubongo kutupa taka kwenye
vizimba.
Changamoto nyinngine ni mwitikio mdogo wa jamii
juu ya usafi wa mazingira na baadhi ya wanajamii kukaidi uondoaji wa takataka
kwenye misingi ya barabara kwa madai kuwa shughuli hiyo ni ya halmashauri hata
hivyo wamesema matumizi ya sheria ndogo za mamlaka ya mji mdogo itakuwa
ufumbuzi mkubwa na suluhisho la tatizo hilo sugu.
Ndipo ilipofika zamu ya mkuu wa wilaya kuongeza na
kutoa masaa 24 kwa taka zote zilizopo katika vizimba hivyo vitatu kuzolewa
haraka na kama akiendelea kuziona wahusika wote watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Masala amesema ameaumua kufanya ziara ya
kutembelea vizimba hivyo baada ya kupata malalamiko ya kukithiri kwa uchafu
ukizingatia kuwa vizimba hivyo vipo katikati ya mji wa Ifakara ambao ndio kioo
cha wilaya ya Kilombero kwani alikwisha toa agizo kwa watendaji wa mji huo
wahakikishe kuwa uchafu usiwepo tena katika vizimba hivyo.
Amesema kuwa aimuingii akilini kuwa uchafu huo
unaendelea kulundikana katika vizimba hivyo wakati wananchi na wafanyabiashara
wanalipa ushuru hivyo kuutaka uongozi wa kata kubuni njia nyingine
itakayosaidia kupunguza taka katika vizimba hivyo ikiwemo kuweka sheria za
utupaji wa taka.
Hata hivyo Masala amemtaka mtendaji wa kata ya
Ifakara kumkamata kisha kumfikisha kwenye vyombo vya sheria mtu yeyote
atakaebainika kuwa anatupa taka nje ya vizimba vilivyowekwa na halmashauri.
Kwa upande wake bwana afya wa wilaya Mbonja
Kasemba alisema kuwa katika bajeti ya mwaka huu idara ya afya imetenga fedha
kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika dampo kubwa la Kiogosi ili kuzuia wananchi
kuzitoa taka punde zinapomwagwa na pia wanategemea kujenga kibanda kwa ajili ya
walinzi eneo hilohilo la Dampo.
No comments:
Post a Comment