Na
Senior Libonge,Ulanga
SERIKALI imetakiwa
kuhakikisha inafanyia marekebisho sheria za ardhi zilizopo, ili mashauri
yanayohusu migogoro ya ardhi yaweze kushughulikiwa kwenye ngazi za vijiji na
kata ardhi hizo zilipo badala ya kupeleka mashauri hayo ngazi za wilaya,
mahakama kuu ama za rufaa, ambapo wakati mwingine imewafanya wananchi kupoteza
haki zao kwa kushindwa kumudu gharama kubwa za uendeshaji.
Ushauri
huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na Wananchi na viongozi wa Tarafa za Malinyi
na Ruaha wilayani Ulanga Mkoani Morogoro, wakati wakichangia kwenye midahalo
kuhusu uwazi na Uwajibikaji katika sekta ya ardhi, iliyoandaliwa na Umoja wa
Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani Ulanga (UNGOKI) kwa ufadhili wa shirika
la Foundation For Civil Society ambapo walitolea mfano iwapo ardhi hiyo itakuwa
ikigombewa baina ya mwananchi wa kawaida na mwekezaji mkubwa, ni rahisi
kwa mwekezaji kushinda shauri husika kutokana na uwezo mdogo wa mwananchi
kufuatilia shauri husika kama inavyotakiwa na kukosa wazi haki zake stahili.
Wananchi
hao pia walilalamikia mabaraza ya adrhi ya vijiji na kata kukosa nguvu za
kisheria katika kushughulikia migogoro, hivyo kudharaulika katika maeneo yao,
ambapo iwapo mlalamikiwa ataitwa na baraza hilo na kushindwa kufika, mabaraza
hayo yamekosa nguvu kuwachukulia watuhumiwa hatua.
Katika
midahalo hiyo ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ni “Uwazi na Uwajibikaji ni msingi
wa maendeleo,wananchi hao walilalamikia mashauri ya ardhi kuandikwa kwa lugha
ya kiingereza katika baraza la ardhi na nyumba, changamoto za mipaka katika vijiji
vyao, wananchi kushindwa kushirikishwa katika masuala ya ardhi ikiwemo
kupitisha majina ya watu wanaoomba maeneo, na gharama kubwa ya kufuatilia
mashauri hasa yale yanayofikishwa ngazi za juu kama baraza la wilaya, mahakama
kuu na mahakama ya rufaa.
Baadhi
ya wananchi hao Omary Ibrahim, Stephen Kasasi,Dvodius Mlungachuma,Edward Lupogo
na Agnes Mpangule walilalamikia wageni kupewa ardhi tena maeneo makubwa katika
maeneo yao, bila kushirikisha ugawaji huo katika mikutano ya vijiji, jambo
linalowanyima haki wakazi husika,na viongozi wengine kutumia nyadhifa zao
kujimilikisha maeneo makubwa, jambo linalochochea migogoro miongoni mwa
wananchi.
Aidha
Stephen Kasasi Lugumey na wenzake kutoka Kijiji cha Makelele walilalamikia eneo
lao la kijiji kuwa dogo na hivyo kushindwakufanya matumii bora ya ardhi,
ikilinganishwa na vijiji vidogo, hivyo kuhoji ukubwa wa eneo la kijiji unapaswa
kuwa vipi na kwamba ni vyema vijiji vikapimwa upya na kugawanywa kwa mlingano
ulio sawa. .
Nao
wanavijiji wa Tarafa ya Ruaha, Kanusian Nkasi,Medist Zimani,Todros
Katanda,Ezekiel Maridadi,Renfrida Pesa na Williama Kologati, pamoja na
kulalamikia madai kama yalivyojitokeza Malinyi, walihoji mpango wa matumizi
bora ya ardhi kuchelewa kufanywa sasa, kutokana na kuwa tayari wananchi wameshajimilisha
maeneo na kutishia ubora wa mpango huo.
Chami
aliwashauri kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali kuwezesha kufanya matumizi
bora ya ardhi kufikia vijiji 38 kati ya 91 vya wilaya ya Ulanga, ni vyema
vijiji vingine vikapitisha maamuzi ya kutaka mpango huo kwenye mikutano yao ya
vijiji na hata kuomba wahisani na mashirika mbalimbali kusaidia uwekaji wa
mipango hiyo, badala ya kuisubiri Serikali, huku akihimiza ushirikishwaji kuwa
ni njia pekee na kubwa ya kutatua migogoro ya ardhi.
“Migogoro
hii ya ardhi ikitatuliwa vijijini ni jambo zuri na jepesi kutatulika, kwa
sababu ardhi ipo kwenu, kuliko kupeleka migogoro hii ngazi za juu, ni kweli
bado kuna changamoto ya sheria za ardhi, kama kushindwa kutoa nguvu kisheria
kwenye mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata, ambapo mlalamikiwa asipotokea
kwenye shauri, baraza limekuwa likikosa nguvu kisheria kumchukulia hatua,lakini
bado wanaharakati wanalipigia kelele”Alisema Mratibu huyo wa UNGOKI akijibu
madai mbalimbali ya wananchi hao.
Nguku
alisema halmashauri za vijiji hazina Mamlaka kisheria kugawa maeneo, na
wanaopaswa kufanya hivyo ni wananchi kupitia mikutano ya vijiji huku
akiwatahadharisha kuwa makini na ugawaji wa maeneo makubwa kwa wawekezaji,
kwani wana hatari ya kukosa haki mbeleni iwapo wanaopewa maeneo watapata hati
miliki na kutumia sheria hizo hizo za ardhi kuwalinda.
Wananchi
walipitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo sheria za ardi namba nne na tano za
mwaka 2004, sheria ya kijiji ya mwaka 1999, historia ya uwepo wa sheria za
ardhi,migogoro inayojitokeza vijijini na mifumo inayotumika katika utatuzi na
mpango wa usimamizi na matumizi bora ya ardhi.
No comments:
Post a Comment