......TUNALENGA Kujenga uwezo wa jamii kushiriki katika utawala na kuwajibisha viongozi wao, kuwezesha jamii kufuatilia matumizi ya fedha za umma kupitia PETS, kutoa elimu ya ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi, utunzaji wa mazingira, kukuza kipato cha jamii hasa wanawake kupitia VICOBA na kuwawezesha wanafunzi kwa kurahisisha upatikanaji wa vitabu katika vituo vya elimu (student centres) PAMOJA TUNAWEZA......TUSHIRIKIANE..
photos
Welcome to UCRC
About Me
- Ulanga Community Resource Centre
- Ulanga Community Resource Centre is a not-for-profit company limited by guarantee which was initiated with the aim of capacitating the resident peoples of Ulanga and Kilombero Districts and Tanzania in general to secure the right information and hold their duty bearers accountable in a bid to promote sustainable community development. UCRC as well aims at promoting educational activities in Ulanga District through facilitation of necessary educational resources in the area which include well equipped libraries and study centers. UCRC also works on land and natural resource rights for the marginalized rural people in Tanzania which also include sustainable use of such resources. It also provides legal aid and assistance to the poor, particularly women, children, the disabled and other disadvantaged groups in the society on different themes including land and gender.
Monday, December 31, 2012
TANZIA- MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero afariki dunia
Na Senior
Libonge,Kilombero
MWENYEKITI
wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero Ramadhani Kiombile amefariki katika
hospitali ya taifa ya Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Taarifa
ambazo zimethibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero
Jackson Mpankuli zimesema kwamba Kiombile amefariki jana (leo) saa 6 mchana
katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mpankuli
alisema Mwenyekiti huyo alikuwa anaumwa huku akikataa kueleza ugongwa uliokuwa
ukimsumbua na kwamba sababu zilizopelekea kifo chake zitaelezwa baadaye
baada ya madaktari wa hospitali hiyo kuufanyia uchunguzi mwili huo.
Taarifa
za kifo cha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero kimestua wakazi
wengi wa wilaya hiyo ambao wengi wao wamekaa katika makundi makundi na
wakijadili baada ya kupata taarifa hiyo huku wengi wao wakiwa hawaamini.
Baada
ya kupata taarifa za msiba huo kila mwananchi wa wilaya ya Kilombero amekuwa
akimpigia simu mwenzie ili kupata ukweli wa kifo hicho na baada ya kupatwa
ukweli kila mmoja amekuwa na majonzi hasa kutokana na uwajibikaji wa mwenyekiti
huyo kijana.
Marehemu
Kiombile licha ya kuwa mwenyekiti wa kwanza mdogo kuongoza
halmashauri hiyo pia alikuwa diwani wa kata ya Ifakara kupitia tiketi ya Chama
cha Mapinduzi(CCM).
Atakumbukwa
kwa mengi hasa ushirikiano kati yake na vijana katika kata yake na wilaya yote
kiujumla pia msimamo wake ambapo alikuwa ahofii kumwambia mtu ukweli pale
anapopata taarifa fulani ambayo inataka kurudisha nyumba maendeleo ya wilaya ya
Kilombero.
Pia
Kiombile anaheshimiwa baada ya kusimamia utengenezaji wa barabara za mitaa ya
kata nzima ya Ifakara ambayo kwa hivi sasa zinapitika kwa msimu mzima na pia
zinarahisisha mgeni yeyote anaeingia katika mji mdogo wa Ifakara kufika popote
atakapo punde atakapoulizia.
Licha
ya hayo pia marehemu alikuwa akisaidia watu wa aina mbalimbali wanaofika katika
ofisi yake wakihitaji msaada wa fedha kwa ajili ya matibabu,shule na shida
mbalimbali ambapo yeye alitoa fedha zake mfukoni na kuweza kuwasaidia.
Wakizungumza
na gazeti hili wakazi wa mji wa Ifakara wamesema kuwa wilaya imempoteza kijana
mchapakazi ambaye uwezo wake ulikuwa unahitajika zaidi hasa baada ya kufanya
mambo makubwa punde alipopata vyeo hivyo vya uwenyekiti na udiwani.
Hiyari
Bohari mkazi wa Ifakara amesema yeye baada ya kupata taarifa ilibidi akae kimya
na kutoamini hasa kutokana na ukaribu alionao kati yake na mwenyekiti huyo hata
kabla hajawa diwani na nafasi ya uwenyekiti.
“Unajuwa
huwezi amini unapopata taarifa za ghafla kama hizi hasa kutokana na ukaribu wa
mtu mwenyewe kwani marehemu nilikuwa nae karibu sana wakati tukiwa pamoja
katika shughuli za usambazaji wa pembejeo na yeye kusema kuwa anaamua kuingia
katika siasa na kweli dhamira yake ilifanikiwa kwa kupata udiwani na
uwenyekiti,”alisema Hiyari.
Naye
John Torogo mkazi wa Kidatu wilayani hapa alisema kuwa kifo cha Kiombile ni
pigo kwa vijana wote wa wilaya hiyo kwani alikuwa mpiganaji wa kweli bila
kuhofia mtu wala chama kwani alikuwa akisimamia haki katika kutatua matatizo
mbalimbali ya wananchi katika wilaya ya Kilombero.
Kwa
upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo David Ligazio alisema kuwa
aamini mwenyekiti wake amefariki dunia kwani mara kwa mara alikuwa akiwasiliana
na mtu wa karibu aliyekuwa akimuhudumia na kumuelezea kuwa afya yake inaimarika
ila alipopigiwa simu na kaimu mkurugenzi pamoja na mkuu wa wilaya nguvu zote
zilimuishia.
Naye
mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilombero Abdallah Kambangwa amesema kuwa naye
ameshtushwa na habari za msiba huo kwani marehemu alikuwa akishirikiana nae
vizuri ndani ya kazi za chama na za nje ya chama akimchukulia kuwa ni mdogo
wake hivyo asingekubali apotosheke wakati yeye yupo
Monday, December 17, 2012
JKT Chita wapewa somo
Na
Senior Libonge,Kilombero
WITO umetolewa kwa askari wa kambi
ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT Chita) kujiwekea malengo yao hasa katika suala la
elimu ili kuweza kutimiza ndoto zao pamoja na za familia zao.
Akizungumza
na askari hao katika tafrija ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya
sambamba na kumpongeza mkuu wa kikosi hicho Meja Msabaha Yamawe kwa kupata
shahada ya pili ya uzamili ya uhasibu na fedha,mkuu wa wilaya ya Kilombero
Hassan Masala amesema kuwa moja ya majukumu ya kutimiza malengo yako ni kupata
elimu.
Masala
amesema kinachofanyika hivi sasa kwa askari nchini ni kubweteka baada ya kupata
ajira bila kufahamu kuwa kujiendeleza kwa elimu ni kupiga hatua moja zaidi ya
maisha hasa katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia.
Amempongeza
mkuu wa kikosi hicho kwa kujiendeleza na kupata shahada ya pili bila kuridhika
na mamlaka makubwa ya kuwaongoza wenzie na kusema kuwa kiongozi huyo amekuwa
mfano mzuri kwa wenzie hivyo na askari waliopo chini yake pia waige mfano huo.
Masala
amemtaka mkuu huyo wa kikosi kunufaisha wenzake kwa elimu aliyoipata na kuwa
mfano bora kwa wafanyakazi wenzie na familia yake na hasa kuwaruhusu wale wote
wanaotaka kujiendeleza ili mradi wafuate sheria za kijeshi.
Naye
meja Yamawe amemuhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa elimu aliyoipata ataitumia
kwa faida ya jeshi na taifa kiujumla na kusema kuwa alikwisha anza na
anaendelea na mwenendo wa kuruhusu askari wengine wajiendeleze kwani faida ya
elimu atakayoipata itamsaidia yeye,jeshi na taifa.
Meja
Yamawe amesema yeyote anaetaka kwenda kusoma amjulishe nay eye atahakikisha
anafanikisha dhamira hiyo ila atakapomaliza lazima alete cheti chake na
asiyeleta cheti atamfungulia mashtaka na kumfukuza jeshi kwani atakuwa amepoteza
fedha za bure za serikali wakati kuna watu wengine wanahitaji huduma kama hiyo.
Hata
hivyo mkuu huyo wa kikosi amesema kuwa licha ya kupata shahada ya pili bado ana
kiu ya kusoma kwani anategemea kusomea shahada ya tatu ya uchumi hivi karibuni.
CCM Moro wakemea makundi
Na
Senior Libonge,Kilombero
MWENYEKITI wa Chama cha
Mapinduzi(CCM) mkoa wa Morogoro Inocent Kalogeris amesema kuwa atakula nae
sahani moja mwanachama yeyote atakaebainika kuwa ni kinara wa makundi ndani ya
chama hicho.
Kauli
hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Ifakara katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Kiungani wenye lengo la
kuimarisha na kukijenga chama.
Kalogeris
amesema kinachoichafua chama hivi sasa ni makundi yaliyopo ndani ya chama hicho
nayayoendelezwa na wanachama wenye uchu wa madaraka na wao wana kina kila
sababu za kuvunja makundi ndani ya chama kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Amewaagiza
viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya matawi kuwachunguza wale wote
wanaoendeleza makundi na watakaobainika watimuliwe ndani ya chama hicho nay eye
lengo lake ni kupigana na kuhakikisha kuwa CCM hakiyumbi katika mkoa wa
Morogoro.
Kuhusu
baadhi ya viongozi wa vijiji kutosoma taarifa za mapato na matumizi,mwenyekiti
huyo wa CCM mkoa amewataka wahusika kufuata taratibu za kusoma
taarifa hizo na atakaeshindwa kufuata taratibu hatua za kisheria zichukuliwe
dhidi yake.
Aidha
Kalogeris alizungumzia zoezi la uondoaji mifugo katika bonde la Kilombero na
kusema kuwa lengo la zoezi hilo ni kulinusuru bonde hilo na kutaka dola ifanye
kazi yake bila kuhofia mtu na serikali ihakikishe inawapatia maeneo mbadala
wale wote wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo katika eneo la Ramsar
ili kuendeleza shughuli zao za kilimo.
Pia
kiongozi huyo alitoa miezi 6 kwa halmashauri ya wilaya kuhakikisha kero ya maji
ya maji katika mji wa Ifakara inakwisha na pia kutoa miezi 9 kwa halmashauri
hiyo kufanikisha mpango wa wilaya kuwa na hospitali ya wilaya.
Awali
mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala alitaja miradi mbalimbali ambayo
imetekelezwa kama ilani ya chama hicho na kikubwa zaidi kukanusha upotoshaji
unaofanyika juu ya operesheni ya okoa bonde la Kilombero.
Masala
amesema mpaka sasa ni mifugo laki 3 imeondolewa toka zoezi hilo lianze na
linazingatia sheria na kusema kuwa wapo viongozi wanaoendesha kampeni za
kupotosha wananchi wasiondoe mifugo na kusema kuwa wao hawatawaachia viongozi
hao.
Amesema
athari za kuwepo mifugo kwenye bonde hilo ni kubwa na wameongeza wiki 2na
mwisho itakuwa Disema 24 mwaka huu ili kupitia upya kila eneo ili kukagua tena
mifugo na hivi karibuni watatumia tena Helkopta katika ukamilishaji wa zoezi
hilo.
Hata
hivyo Masala alibainisha kuwa hata kama mifugo inayoendelea kukamatwa hivi sasa
ikibainika kuwa ya kiongozi Fulani wao hawatasita kuikamata na kuipiga faini
nay eye atakaechukizwa aende popote nayeye yupo tayari kupambana nae kwani yeye
anafuata sheria bali hafanyi kazi ya kuropoka kwenye vyombo vya habari.
Saturday, December 15, 2012
Tulinde Misitu yetu na rasilimali adhimu, wananchi waaswa
Henry Bernard Mwakifuna,
Ifakara-Kilombero.
Serikali
imeahidi kwa dhati kabisa kusimamia Sheria za Uhifadhi wa Misitu .
Akifunga
Warsha ya Siku Moja ya Uwasilishaji wa Hali Halisi ya Hifadhi ya Misitu ya
Udzungwa, Bi Hawa Mposi Lumuli, Afisa Tarafa ya Ifakara amesema kwa Watumishi
wa Idara ya Misitu wanaolegalega na kutosimamia ipasavyo Sheria, Kanuni na
Taratibu na kukiuka maadili watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Amesema
kuwa tegemeo kubwa la Serikali ni kuona wafanyakazi wa Idara hiyo wanazingatia
maadili na kusaidia kuokoa, kuhifadhi na kutunza misitu.
Kwa
upande wao watafiti kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG)
wamesema kuwa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa imeonekana ya Kipekee kwa Uhifadhi
wa Wanyama muhimu na Adimu kama Swala waitwao Vinde na Vyura wa Kihansi.
Vinde, aina ya Swala adimu Misitu ya Asili ya Udzungwa. |
Akiwasilisha
Matokeo ya Utafiti wa Hali ya Msitu wa Udzungwa, Bwana Justine Gwegine ,Afisa
Mtafiti na Mtathimini wa Hali ya Misitu
kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) amesema kuwa Matokeo ya
ya utafiti wao yameorodhesha Jumla
ya aina za ndege 79 zilionekana na katika maeneo ya Ikule, Chita Wilayani Kilombero na Illutila
na Idegenda katika Wilaya ya Kilolo.
Amesema
kuwa kati ya aina 79 zilizoorodheshwa, aina 14 ambayo
ni asilimia 17 ni wale ndege adimu na pengine wanapatikana katika tao la
mashariki pekee.
Mbega mweupe, kiumbe adimu anyepatikana katika msitu wa Udzungwa |
Lengo la Uwasilishaji
huo ni kufahamu hali ya Misitu na Bioanuai yake kwa ujumla ili kuisaidia
Serikali Kupanga Mipango ya Kuisimamia Vizuri kutokana na Matokeo ya Tafiti.
Utafiti huo umefanyika
kwa Siku 25 Mwezi Septemba na Oktoba mwaka jana ambapo Vijiji Vinne vya Wilaya
za Kilolo na Kilombero zimehusika.
Msitu wa Hifadhi Asili
wa Udzungwa wenye ukubwa wa Hekta 20,720 na ulianzishwa Mwaka 1929,
unasimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania.
Tuesday, December 11, 2012
Mkuu wa Wilaya apania kuweka safi mji wa Ifakara
Na Igamba Libonge,Kilombero
KATIKA
kuonyesha kukerwa na uchafu uliokithiri katika vizimba vya madampo madogo
matatu yaliyopo katikati ya mamlaka ya mji mdogo wa Ifakara,mkuu wa wilaya ya
Kilombero Hassan Masala ametoa masaa 24 kwa viongozi wa mamlaka huo kuondoa
uchafu huo la sivyo wahusika wote watawajibishwa kisheria.
Masala ametoa agizo hilo jana wakati alipotembelea
na kujionea lundo kubwa la takataka zikiwa zimelundikana katika vizimba hivyo
hivyo vitatu ambavyo ni vya stendi ya mabasi,stendi ya zamani na soko kuu la
Ifakara.
Katika ziara hiyo sehemu ya kwanza kutembelea
ilikuwa stendi ya mabasi ambapo wananchi walimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa
licha ya wao kuchangia lakini wanashangaa taka hizo kuendelea kujaa na
wanaosababisha kujaa huko ni majirani ambao utoa taka zao majumbani na kuzileta
katika dampo hilo.
Sehemu ya pili kutembelea ilikuwa stendi ya zamani
ambapo hapo alikuta takataka zimelundikana hadi barabarani na wakazi wa maeneo
hayo walimweleza mkuu huyo kuwa wanashindwa kukaa katika maeneo yao hasa
kutokana na harufu kali inayotoka katika dampo hilo.
Alipofika sokoni ndipo alipopata malalamiko mengi
kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hilo ambapo wamedai kuwa licha ya kulipia
ushuru kwa kila siku wanashangaa takataka hizo kuendelea kuwepo eneo hilo na
malalamiko yao pamoja na kukosekana kw walinzi wenye silaha na geti walikwisha
ueleza uongozi wa halmashauri kwa muda mrefu lakini hakuna mabadiliko.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa
wafanyabiashara wa soko hilo Shabani Gwazai ambaye alisema kuwa licha ya
kukutana mara kadhaa na uongozi wa halmashauri kuhusu kutatua matatizo hayo
hakuna jipya lililojitokeza na kusema kuwa kama ukiwepo ushirikiano wa pamoja
kati ya wao kama wafanyabiashara na halmashauri tatizo la uchafu halitakuwepo
sokoni hapo.
Awali kabla ya kutoa fursa ya maswali kwa
wafanyabiashara taarifa ya afya ya kata ilisomwa na kueleza changamoto
wanazokabiliana nazo ikiwemo kutokuwa na vyombo vya usafirishaji taka vya
uhakika,matumizi mabaya ya vizimba ikiwemo jamii kutupa vinyesi na mimba zilizotolewa
mitaani na jamii kutumia watu wenye mtindio wa ubongo kutupa taka kwenye
vizimba.
Changamoto nyinngine ni mwitikio mdogo wa jamii
juu ya usafi wa mazingira na baadhi ya wanajamii kukaidi uondoaji wa takataka
kwenye misingi ya barabara kwa madai kuwa shughuli hiyo ni ya halmashauri hata
hivyo wamesema matumizi ya sheria ndogo za mamlaka ya mji mdogo itakuwa
ufumbuzi mkubwa na suluhisho la tatizo hilo sugu.
Ndipo ilipofika zamu ya mkuu wa wilaya kuongeza na
kutoa masaa 24 kwa taka zote zilizopo katika vizimba hivyo vitatu kuzolewa
haraka na kama akiendelea kuziona wahusika wote watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Masala amesema ameaumua kufanya ziara ya
kutembelea vizimba hivyo baada ya kupata malalamiko ya kukithiri kwa uchafu
ukizingatia kuwa vizimba hivyo vipo katikati ya mji wa Ifakara ambao ndio kioo
cha wilaya ya Kilombero kwani alikwisha toa agizo kwa watendaji wa mji huo
wahakikishe kuwa uchafu usiwepo tena katika vizimba hivyo.
Amesema kuwa aimuingii akilini kuwa uchafu huo
unaendelea kulundikana katika vizimba hivyo wakati wananchi na wafanyabiashara
wanalipa ushuru hivyo kuutaka uongozi wa kata kubuni njia nyingine
itakayosaidia kupunguza taka katika vizimba hivyo ikiwemo kuweka sheria za
utupaji wa taka.
Hata hivyo Masala amemtaka mtendaji wa kata ya
Ifakara kumkamata kisha kumfikisha kwenye vyombo vya sheria mtu yeyote
atakaebainika kuwa anatupa taka nje ya vizimba vilivyowekwa na halmashauri.
Kwa upande wake bwana afya wa wilaya Mbonja
Kasemba alisema kuwa katika bajeti ya mwaka huu idara ya afya imetenga fedha
kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika dampo kubwa la Kiogosi ili kuzuia wananchi
kuzitoa taka punde zinapomwagwa na pia wanategemea kujenga kibanda kwa ajili ya
walinzi eneo hilohilo la Dampo.
Tuesday, December 4, 2012
Utunzaji wa Mazingira sawa, Haki za Binadamu Je?
Na
Senior Libonge,Ulanga
SERIKALI imetakiwa
kuhakikisha inafanyia marekebisho sheria za ardhi zilizopo, ili mashauri
yanayohusu migogoro ya ardhi yaweze kushughulikiwa kwenye ngazi za vijiji na
kata ardhi hizo zilipo badala ya kupeleka mashauri hayo ngazi za wilaya,
mahakama kuu ama za rufaa, ambapo wakati mwingine imewafanya wananchi kupoteza
haki zao kwa kushindwa kumudu gharama kubwa za uendeshaji.
Ushauri
huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na Wananchi na viongozi wa Tarafa za Malinyi
na Ruaha wilayani Ulanga Mkoani Morogoro, wakati wakichangia kwenye midahalo
kuhusu uwazi na Uwajibikaji katika sekta ya ardhi, iliyoandaliwa na Umoja wa
Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani Ulanga (UNGOKI) kwa ufadhili wa shirika
la Foundation For Civil Society ambapo walitolea mfano iwapo ardhi hiyo itakuwa
ikigombewa baina ya mwananchi wa kawaida na mwekezaji mkubwa, ni rahisi
kwa mwekezaji kushinda shauri husika kutokana na uwezo mdogo wa mwananchi
kufuatilia shauri husika kama inavyotakiwa na kukosa wazi haki zake stahili.
Wananchi
hao pia walilalamikia mabaraza ya adrhi ya vijiji na kata kukosa nguvu za
kisheria katika kushughulikia migogoro, hivyo kudharaulika katika maeneo yao,
ambapo iwapo mlalamikiwa ataitwa na baraza hilo na kushindwa kufika, mabaraza
hayo yamekosa nguvu kuwachukulia watuhumiwa hatua.
Katika
midahalo hiyo ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ni “Uwazi na Uwajibikaji ni msingi
wa maendeleo,wananchi hao walilalamikia mashauri ya ardhi kuandikwa kwa lugha
ya kiingereza katika baraza la ardhi na nyumba, changamoto za mipaka katika vijiji
vyao, wananchi kushindwa kushirikishwa katika masuala ya ardhi ikiwemo
kupitisha majina ya watu wanaoomba maeneo, na gharama kubwa ya kufuatilia
mashauri hasa yale yanayofikishwa ngazi za juu kama baraza la wilaya, mahakama
kuu na mahakama ya rufaa.
Baadhi
ya wananchi hao Omary Ibrahim, Stephen Kasasi,Dvodius Mlungachuma,Edward Lupogo
na Agnes Mpangule walilalamikia wageni kupewa ardhi tena maeneo makubwa katika
maeneo yao, bila kushirikisha ugawaji huo katika mikutano ya vijiji, jambo
linalowanyima haki wakazi husika,na viongozi wengine kutumia nyadhifa zao
kujimilikisha maeneo makubwa, jambo linalochochea migogoro miongoni mwa
wananchi.
Aidha
Stephen Kasasi Lugumey na wenzake kutoka Kijiji cha Makelele walilalamikia eneo
lao la kijiji kuwa dogo na hivyo kushindwakufanya matumii bora ya ardhi,
ikilinganishwa na vijiji vidogo, hivyo kuhoji ukubwa wa eneo la kijiji unapaswa
kuwa vipi na kwamba ni vyema vijiji vikapimwa upya na kugawanywa kwa mlingano
ulio sawa. .
Nao
wanavijiji wa Tarafa ya Ruaha, Kanusian Nkasi,Medist Zimani,Todros
Katanda,Ezekiel Maridadi,Renfrida Pesa na Williama Kologati, pamoja na
kulalamikia madai kama yalivyojitokeza Malinyi, walihoji mpango wa matumizi
bora ya ardhi kuchelewa kufanywa sasa, kutokana na kuwa tayari wananchi wameshajimilisha
maeneo na kutishia ubora wa mpango huo.
Chami
aliwashauri kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali kuwezesha kufanya matumizi
bora ya ardhi kufikia vijiji 38 kati ya 91 vya wilaya ya Ulanga, ni vyema
vijiji vingine vikapitisha maamuzi ya kutaka mpango huo kwenye mikutano yao ya
vijiji na hata kuomba wahisani na mashirika mbalimbali kusaidia uwekaji wa
mipango hiyo, badala ya kuisubiri Serikali, huku akihimiza ushirikishwaji kuwa
ni njia pekee na kubwa ya kutatua migogoro ya ardhi.
“Migogoro
hii ya ardhi ikitatuliwa vijijini ni jambo zuri na jepesi kutatulika, kwa
sababu ardhi ipo kwenu, kuliko kupeleka migogoro hii ngazi za juu, ni kweli
bado kuna changamoto ya sheria za ardhi, kama kushindwa kutoa nguvu kisheria
kwenye mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata, ambapo mlalamikiwa asipotokea
kwenye shauri, baraza limekuwa likikosa nguvu kisheria kumchukulia hatua,lakini
bado wanaharakati wanalipigia kelele”Alisema Mratibu huyo wa UNGOKI akijibu
madai mbalimbali ya wananchi hao.
Nguku
alisema halmashauri za vijiji hazina Mamlaka kisheria kugawa maeneo, na
wanaopaswa kufanya hivyo ni wananchi kupitia mikutano ya vijiji huku
akiwatahadharisha kuwa makini na ugawaji wa maeneo makubwa kwa wawekezaji,
kwani wana hatari ya kukosa haki mbeleni iwapo wanaopewa maeneo watapata hati
miliki na kutumia sheria hizo hizo za ardhi kuwalinda.
Wananchi
walipitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo sheria za ardi namba nne na tano za
mwaka 2004, sheria ya kijiji ya mwaka 1999, historia ya uwepo wa sheria za
ardhi,migogoro inayojitokeza vijijini na mifumo inayotumika katika utatuzi na
mpango wa usimamizi na matumizi bora ya ardhi.
Saturday, December 1, 2012
Jumla ya shilingi milioni 212,886,000 zakusanywa katika zoezi la kuondoa mifugo Bonde la Mto Kilombero
Na Senior Libonge- Ifakara
JUMLA ya shilingi milioni 212,886,000 zimepatikana
ikiwa ni mapato ya uwekaji alama mifugo na faini katika zoezi la uondoaji
mifuko katika bonde tengefu la Kilombero kwa wilaya ya Kilombero.
Akizungumza jana katika kikao cha kamati ya
uashauri ya wilaya(DCC)Mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala amesema kuwa
fedha hizo zimepatikana baada ya kuanza kwa zoezi la uwekaji alama lilianza
Agosti 21 na kumalizika Septemba 30 mwaka huu na pia zoezi la faini kwa
wafugaji waliokaidi amri halali lililoanza Oktoba 30 mwaka huu.
Masala amesema zoezi la kuweka alama mifugo
inayostahili kubaki kulingana na ukubwa wa eneo husika lilihusisha vijiji
vilivyopo ndani ya eneo la Ramsar na vilevile nje ya eneo hilo kwa kufanya
mikutano mikuu ya hadhara kwa ajili ya utambuzi wa wafugaji halali na
wanaotakiwa kubaki katika kila kijiji.
Alisema jumla ya ng’ombe 52,780 waliwekwa alama
kwa gharama ya shilingi 1000 kwa kila ng’ombe na kupata jumla ya shilingi
milioni 52,780,000 kama makusanyo ya zoezi hilo na kati ya hizo shilingi
milioni 27,940,300 zilitumika kuendelea na zoezi hilo.
Amebainisha kuwa katika zoezi la uondoaji wa
mifugo ambalo zoezi hilo bado linaendelea mpaka sasa jumla ya wafugaji 2,428
wenye ng’ombe wapatao 9,248 walitozwa faini kwa viwango mbalimbali kulingana na
makosa waliyopatikana nayo.
Mkuu huyo wa wilaya amesema jumla ya ng’ombe 3,482
walitozwa shilingi 10,000 na kupatikana shilingi milioni 34.8 huku ng’ombe
5,379 walitozwa shilingi 20,000 na kupatikana shilingi milioni 107.5,ng’ombe
264 walitozwa shilingi 40,000 na kupatikana shilingi milioni 10.5 na hiyo inafanya
shilingi milioni 152.9 kuwa jumla ya mapato yaliyotokana na faini.
Masala amesema hata hivyo zoezi utoaji wa vibali
vya kusafiria lilienda sambamba na zoezi hilo ambapo idadi ya ng’ombe 4764
walipatiwa vibali kwa gharama ya shilingi 1500 na shilingi milioni 7.1
zimekusanywa kama ruzuku ya serikali kuu.
Amesema fedha zilizoidhinishwa katika zoezi la
uwekaji wa alama ng’ombe na uondoaji wa mifugo katika bonde tengefu la
Kilombero ni shilingi milioni 152.7 na fedha iliyotumika hadi sasa ni shilingi
milioni 94 na kufanya salio la shilingi milioni 14.1.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya amesema zoezi la
kuondoa mifugo linaendelea japokuwa linakabiliana na changamoto mbalimbali
ambazo wataalamu wanaendelea kukabiliana nazo
Gharama za Afya zapanda katika Hospitali ya St. Francis Ifakara
Na Senior
Libonge,Kilombero
KUTOPATA fedha kwa wakati
kutoka mfuko wa pamoja(basket fund)na mgawanyo mdogo toka bohari ya madawa
nchini(MSD)ndiko kunakosababisha hospitali ya rufaa ya Mt.Francis iliyopo mjini
Ifakara wilayani Kilombero kupandisha gharama ya matibabu.
Akizungumza katika kikao
cha kamati ya ushauri ya wilaya,mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk,Angelo Nyamtema
amesema licha ya kutopata fedha kwa wakati na mgawanyo mdogo pia suala la
ulipaji wa mishahara kwa wataalamu mbalimbali nayo uchangia hospitali hiyo
kukosa fedha.
Dk,Nyamtema amesema licha
ya changamoto hizo alizozitaja mkakati uliopo hivi sasa ni kuboresha huduma
katika hospitali hiyo ili kuweza kufikia hadhi ya hospitali ya rufaa baada ya
kupandishwa hadhi.
Amesema ni mwezi wa tano hivi sasa hawajapata
fedha ya basket fund huku pia wakiwa hawajapata fedha toka serikalini tokea
mwezi Julai mwaka huu ili kuweza kuagiza madawa na vifaa mbalimbali vya tiba
kutoka bohari ya madawa nchini(MSD).
Mkurugenzi huyo wa hospitali ameiomba halmashauri
ya wilaya na serikali kiujumla kushirikiana nao ili kutatua changamoto
zinazowakabili hatimaye kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wanaotumia
hospitali hiyo kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Amesema suala la mishahara limekuwa tatizo kwani
kwa kipindi cha karibuni wametumia kiasi cha shilingi milioni 42 kwa ajili ya
kulipa mishahara watumishi wake na fedha hizo zimetokana na fedha zinazotokana
na gharama za uchangiaji zinazotozwa kwa wagonjwa.
Dk,Nyamtema ameiomba serikali kuwapatia wataalamu
walioajiriwa na serikali ili wao waweze kupunguza mzigo mkubwa wa kuwalipa
mishahara na hali hiyo itapelekea kupunguza gharama kwa wananchi wanaopata
huduma katika hospitali hiyo.
Hata hivyo mkurugenzi huyo amekanusha taarifa kuwa
menejimenti ya hospitali uamua kupandisha gharama za matibabu wanapojisikia na
kusema kuwa mawazo ya kupandisha gharama za matibabu sio ufanywa na uongozi wa
hospitali bali ni kamati nzima inayowashirikisha watu kutoka
serikalini,halmashauri ya wilaya na wadau mbalimbali.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilombero
aliuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya chini ya mwenyekiti wake na
mkurugenzi mtendaji kukaa pamoja na menejimenti ya hospitali hiyo ili kutatua
matatizo mbalimbali hatimaye kuweza kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama za matibabu.
Tuesday, November 27, 2012
SUALA LA ARDHI BADO LAFUKUTA KILOMBERO
Na
Senior Libonge,Kilombero
SERIKALI wilayani Kilombero imesema kuwa itafuta
mpaka wa kugawa ardhi ya kijiji na hifadhi bila kujali gharama iliyotumika kama ikibainika kuwa mpaka huo umekosema.
Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya ya
Kilombero Hassan Masala wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha
Miwangani kata ya Idete baada ya wananchi hao kulalamika mbele ya mkuu huyo wa
wilaya kuwa mpaka uliowekwa hivi karibuni kutenganisha kijiji na eneo la
hifadhi umemega sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji.
Hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Kilombero
iliweka mpaka wa kutenganisha vijiji na eneo la hifadhi la lengo ni
kuyatenganisha maeneo hayo ni kutekeleza azimio la Ramsar lililotaka kutunza
maeneo ya ardhi oevu ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la
utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo zoezi hilo lililofanywa na wataalamu wa mazingira na ardhi wa
wilaya lililalamikiwa na baadhi ya wananchi ambapo mpaka huo umepita kuwa
wataalamu hao walikuwa wakifanya kazi bila kushirikisha serikali za vijiji
ambazo zinajuwa mipaka halisi ya vijiji vyao na eneo la hifadhi.
Masala amesema kuwa ameamua kufika katika kijiji
hicho ili kupata ukweli kuhusu tatizo la mipaka baada ya kupata barua na
kupigiwa simu kutoka kwa viongozi wa kijiji na wananchi kuwa wataalamu
walikwenda kuweka mpaka wamemega sehemu kubwa ya kijiji na kufanya wananchi wa
kijiji hicho kukosa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.
Na alipotoa nafasi kwa wananchi ili kutoa kero zao
wananchi wote waliosimama walilalamikia suala la mpaka na kusema kuwa kama
serikali isipochukua hatua za haraka kurekebisha mpaka huo kuna hatari ya
kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji kwani hivi sasa mifugo
iliyopo katika kijiji hicho inalishiwa katika mashamba ya wakulima kwa kukosa
sehemu za malisho ambazo mwanzo zilitengwa eneo lililomegwa.
Ilibidi mkuu wa wilaya aingilie kati kupunguza
hasira baada ya kutokea hali ya kutupiana maneno makali waliokuwa wakirushiana
kati ya wataalamu wa ardhi na maliasili na mwenyekiti wa kijiji cha Miwangani
Abdul Mtilangondo ambapo kila mmoja alikuwa akijitetea kuwa yupo sawa katika
suala hilo.
Baada ya wataalamu kusema kuwa mpaka uliowekwa ni
halali kwani wametumia kifaa maalum cha kupimia GPS na wakati wanaendesha zoezi hilo walishirikisha serikali ya kijiji lakini wakati
zoezi linaendelea mwenyekiti wa kijiji aliwashawishi wajumbe wa serikali ya
kijiji kususia zoezi hilo.
Naye mwenyekiti wa kijiji Mtilangondo alisema kuwa
wakati zoezi linafanyika aliamua kugoma kutokana na wataalamu hao kupindisha
mipaka wakati ramani halali inaonyesha mipaka inapotakiwa kupita lakini
wataalamu hao wanagoma na kuweka mipaka wanayotaka wao na hali hiyo ndiyo
ilipelekea yeye na wajumbe wake kususia zoezi hilo.
Ndipo mkuu wa wilaya alipoamua kuingilia kati na
kusema kuwa itabidi zoezi hilo liangaliwe upya kati ya wataalamu wa halmashauri
na viongozi wa serikali ya kijiji na ikibainika kuwa mipaka imekosewa itafutwa
na kuwekwa upya bila kujali gharama iliyotumika ila ikionekana na halali
itabidi mipaka hiyo iheshimiwe.
Masala alisema cha msingi ni kulinganisha mipaka
halali kwa kufuata ramami za vijiji husika na ramani za wilaya kwani zoezi hilo
sio la kuwakomoa wananchi bali ni kuyahifadhi maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa
yameharibika baada ya kuvamiwa na kusema kuwa kama mipaka ipo halali yeye hana
mamlaka ya ubadilishaji wa mpaka huo.
LUPIRO KUNUFAIKA NA MRADI MKUBWA WA MAJI
Na
Senior Libonge,Ulanga
Wananchi
wa kijiji cha Lupiro chenye wakazi zaidi 4000 wilayani
Ulanga mkoani Morogoro wanategemea kunufaika na mradi mkubwa wa maji
unaofadhiliwa na benki ya Dunia.
Akiongea wakati wa ziara ya Madiwani wa kamati ya
Fedha Utawala na Mipango kutembelea miradi ya maendeleo Mhandisi wa Maji Wilaya
ya Ulanga Patrice Jerome amesema benki ya dunia imetoa kiasi cha
Tshs milioni 233 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Lupiro ambapo miundombinu
ya maji ,tanki la kuhifadhia maji na ujenzi wa vituo 20 vya maji
vya jumuiya ,ufungaji wa mabomba ya maji , ujenzi wa pampu house na
ufungaji wa pampu ya kusukuma maji .
Jerome amesema kuwa tanki linalojengwa litakuwa na
uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 90 za maji (sawa na lita 90,000) na kuwa
msaada mkubwa kwa wakazi wa tarafa hiyo kwani eneo hilo lina uhaba mkubwa wa
maji kwa muda mrefu.
Amesema mradi huu ni miongoni wa miradi ya vijiji
10 vinavyotarajiwa kujengwa kupitia pragramu hii ya maji na usafi wa
mazingira.
Nao wajumbe wa kamati waliwashukuru benki ya dunia
kupitia program ya maendeleo ya sekta ya maji kwa kufadhili mradi huo kwani
itawasaidia wananchi na kuwasihi wananchi kutunza na kuhifadhi
vizuri mradi huo pindi utakapokamilika ili uwe endelevu na kufikia lengo la
kuanzishwa kwa mradi huo.
Kamati imesisitiza kuanzishwa na
kusajiliwa kwa jumuiya hiyo ya watumiaji maji sambamba na kuwa na mfuko wa maji
kwa ajili ya kuendesha mradi huo.Pia miradi mingine kama Igota kichangani na
Gombe ifuatiliwe kwani taratibu za manunuzi zilishakamilika ili
ianze kujengwa .
Akizitaja changamoto zinazojitokeza katika ujenzi
wa mradi huo mshauri wa mradi Bw Raymundi wa kampuni ya ushauri ya
Interconsult ya Dar es salaam amesema kuwa ni ugumu wa
upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na uhaba wa upatikanaji wa vibarua ambapo wengi
wao wanadai maslahi makubwa kuliko fedha iliyopangwa.
Ziara ya kamati ya Fedha Utawala na Mipango pia
ilitembelea miradi mbalimbali katika tarafa za Vigoi,Lupiro na mradi mkubwa wa
umwagiliaji unaoanza kujengwa katika kata ya Minepa.
Subscribe to:
Posts (Atom)