Na
Senior Libonge,Kilombero
SERIKALI wilayani Kilombero imesema kuwa itafuta
mpaka wa kugawa ardhi ya kijiji na hifadhi bila kujali gharama iliyotumika kama ikibainika kuwa mpaka huo umekosema.
Kauli hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya ya
Kilombero Hassan Masala wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha
Miwangani kata ya Idete baada ya wananchi hao kulalamika mbele ya mkuu huyo wa
wilaya kuwa mpaka uliowekwa hivi karibuni kutenganisha kijiji na eneo la
hifadhi umemega sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji.
Hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Kilombero
iliweka mpaka wa kutenganisha vijiji na eneo la hifadhi la lengo ni
kuyatenganisha maeneo hayo ni kutekeleza azimio la Ramsar lililotaka kutunza
maeneo ya ardhi oevu ambayo yana umuhimu wa pekee duniani katika suala zima la
utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo zoezi hilo lililofanywa na wataalamu wa mazingira na ardhi wa
wilaya lililalamikiwa na baadhi ya wananchi ambapo mpaka huo umepita kuwa
wataalamu hao walikuwa wakifanya kazi bila kushirikisha serikali za vijiji
ambazo zinajuwa mipaka halisi ya vijiji vyao na eneo la hifadhi.
Masala amesema kuwa ameamua kufika katika kijiji
hicho ili kupata ukweli kuhusu tatizo la mipaka baada ya kupata barua na
kupigiwa simu kutoka kwa viongozi wa kijiji na wananchi kuwa wataalamu
walikwenda kuweka mpaka wamemega sehemu kubwa ya kijiji na kufanya wananchi wa
kijiji hicho kukosa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.
Na alipotoa nafasi kwa wananchi ili kutoa kero zao
wananchi wote waliosimama walilalamikia suala la mpaka na kusema kuwa kama
serikali isipochukua hatua za haraka kurekebisha mpaka huo kuna hatari ya
kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji kwani hivi sasa mifugo
iliyopo katika kijiji hicho inalishiwa katika mashamba ya wakulima kwa kukosa
sehemu za malisho ambazo mwanzo zilitengwa eneo lililomegwa.
Ilibidi mkuu wa wilaya aingilie kati kupunguza
hasira baada ya kutokea hali ya kutupiana maneno makali waliokuwa wakirushiana
kati ya wataalamu wa ardhi na maliasili na mwenyekiti wa kijiji cha Miwangani
Abdul Mtilangondo ambapo kila mmoja alikuwa akijitetea kuwa yupo sawa katika
suala hilo.
Baada ya wataalamu kusema kuwa mpaka uliowekwa ni
halali kwani wametumia kifaa maalum cha kupimia GPS na wakati wanaendesha zoezi hilo walishirikisha serikali ya kijiji lakini wakati
zoezi linaendelea mwenyekiti wa kijiji aliwashawishi wajumbe wa serikali ya
kijiji kususia zoezi hilo.
Naye mwenyekiti wa kijiji Mtilangondo alisema kuwa
wakati zoezi linafanyika aliamua kugoma kutokana na wataalamu hao kupindisha
mipaka wakati ramani halali inaonyesha mipaka inapotakiwa kupita lakini
wataalamu hao wanagoma na kuweka mipaka wanayotaka wao na hali hiyo ndiyo
ilipelekea yeye na wajumbe wake kususia zoezi hilo.
Ndipo mkuu wa wilaya alipoamua kuingilia kati na
kusema kuwa itabidi zoezi hilo liangaliwe upya kati ya wataalamu wa halmashauri
na viongozi wa serikali ya kijiji na ikibainika kuwa mipaka imekosewa itafutwa
na kuwekwa upya bila kujali gharama iliyotumika ila ikionekana na halali
itabidi mipaka hiyo iheshimiwe.
Masala alisema cha msingi ni kulinganisha mipaka
halali kwa kufuata ramami za vijiji husika na ramani za wilaya kwani zoezi hilo
sio la kuwakomoa wananchi bali ni kuyahifadhi maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa
yameharibika baada ya kuvamiwa na kusema kuwa kama mipaka ipo halali yeye hana
mamlaka ya ubadilishaji wa mpaka huo.