Na
Senior Libonge,Kilombero
WAKATI zoezi la kuondoa mifugo
vamizi katika bonde tengefu la Kilombero likiendelea,zoezi hilo limeingia
dosari baada ya mfugaji mmoja kudaiwa kuuawa na polisi wanaoendesha zoezi hilo
.
Tukio la kuuawa kwa mfugaji huyo
limetokea juzi katika kijiji cha Udagaji kata ya Chita wilayani Kilombero baada
ya kundi la wafugaji kuwavamia askari na kuanza kuwapiga lengo lao ni
kuwanyang’anya mifugo iliyokamatwa katika operesheni hiyo.
Akizungumza na gazeti hili diwani wa
kata ya Chita Hassan Kidapa amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa
limetokea juzi majira ya jioni katika kijiji hicho cha Udagaji baada ya kundi
la wafugaji kuwavamia askari waliokamata kundi la ng’ombe wanaofikia 300
walioingia katika kijiji hicho kinyemela ili kuficha mifugo yao .
Kidapa amesema siku ya tukio baada
ya askari kukamata mifugo hiyo iliyokuwa imefichwa katika moja ya msitu katika
kijiji hicho waliikusanya katika kundi moja ili kuipeleka katika kambi maalum
za kuhifadhi mifugo iliyokamatwa mara wakatokea jamii ya wafugaji wachache na
kumpiga askari mmoja aliye na silaha kwa kutumia fimbo na alipoanguka chini
waliamua kuondoka na kwenda kuita wenzao ili wachukue mifugo hiyo.
Amesema baada ya kupeana taarifa
liliibuka kundi kubwa la wafugaji huku wakiwa na silaha za jadi lengo ni kupora
ng’ombe hao waliokamatwa lakini walipofika katika uwanja wa mpira wa shule ya
Udagaji walikutana na askari walioongezeka na walipewa tahadhari kwamba
wasisogee eneo hilo lakini wafugaji hao walikaidi amri ya polisi na kusogelea
mifugo na ndipo askari waliporusha risasi hewani ili kuwatawanya lakini
waliendelea kukaidi.
Diwani huyo amesema kuwa baada ya
kuona kuwa wafugaji hao wamekaidi amri halali ya polisi ya kutosogelea eneo la
mifugo hiyo mmojawapo alipigwa risasi ya mguuni lakini bado walikaidi na
kuendelea kuwasogelea askari na ndipo marehemu alipopigwa risasi ya kiunoni na
kufariki dunia.
Hata hivyo diwani huyo amesema kuwa
hadi jana jioni jina na mahali alipotokea marehemu bado havijajulikana kwani ni
wafugaji wageni walioingia na kujificha katika kijiji hicho kwa lengo la
kukimbia operesheni inayoendeshwa kwa nguvu ya kuondoa mifugo katika bonde lote
la Kilombero na kijiji hicho hakina historia ya kuwepo kwa mifugo.
Kidapa amesema mifugo iliyokamatwa
imepelekwa katika kambi maalum ya kuhifadhi mifugo iliyopo Mngeta na hivi sasa
katika kata ya Chita hali sio shwari kwani jamii ya wafugaji wanaendelea
kuwatisha viongozi akiwemo afisa mtendaji wa kata kwa madai kuwa ndio
waliosababisha mwenzao kuuawa.
Kwa upande wake kamanda wa polisi
mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
yeye yupo katika operesheni hiyo akifuatilia zoezi linavyoendelea na kusema
kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakaidi kutekeleza maagizo ya askari punde wanapotakiwa
kufanya hivyo.
Shilogile amewataka wafugaji na
wananchi wote kiujumla katika operesheni hiyo kutii sheria punde wanapoagizwa
na kueleza kuwa wao kama askari toka ianze operesheni hiyo wanaiendesha
kiustaarabu ila kuna watu wachache wanaotaka kulipaka matope jeshi hilo kwa
kukaidi amri halali za kipolisi.
No comments:
Post a Comment