Na Senior Libonge,Kilombero
HALI ya upatikanaji wa nishati ya mafuta katika
wilaya ya Kilombero imerudi kama kawaida kwa bidhaa hiyo kuanza kupatikana
baada ya kuadimika kwa wiki moja sasa.
Kukosekana kwa nishati hiyo muhimu ikiwemo
Petrol,Diseli na mafuta ya taa kulisababisha walanguzi kupandisha bei ya mafuta
kwa bei wanayotaka wao na ilipelekea bei ya petrol kufikia shilingi 5000 badala
ya bei halisi ya shilingi 2360.
Bei ya petrol ilikuwa juu zaidi hasa baada ya
kutumiwa na wananchi wengi hasa waendesha pikipiki maarufu Bodaboda ambapo na
wao ilipelekea kupandisha nauli ya safari kutoka shilingi 1000 hadi kufikia
shilingi 2000.
Licha ya kupanda kwa bei huko na bidhaa hizo
kuuzwa kwa kificho jeshi la polisi liliendelea na msako wa kuwakamata walanguzi
hao ambao wengi wao walificha bidhaa hiyo kwenye nyumba zao bila kuhofia hatari
ya kulipuka na kusababisha moto katika nyumba hizo.
Kutokana na tatizo hilo wengi wa wananchi wilayani
hapo waliwalaumu wamiliki wa vituo vya mafuta kuwa walikuwa wanakataa kwa
makusudi kuyatoa mafuta ambayo yalikuwemo kwenye matanki yao kwa kutaka
yapandishwe bei na wao wayatoe huku wengine wakisema kuwa pia wamiliki hao
walikuwa wakiwatumia walanguzi kwa kuwapa mafuta nyakati za usiku ili asubuhi
wayauze kwa bei ya juu.
Kwa upande wao wamiliki wa vituo vya mafuta wote
kwa pamoja baada ya kuhojiwa walisema kuwa kukosekana kwa bidhaa hiyo Dar es
Salaam ndiko kulikofanya wao wakose nishati hiyo na pia kukanusha kuwa hawakuwa
wakitoa mafuta kinyemela kwa ajili ya kuwapatia walanguzi ili wawauzie kwa bei
ya juu.
Hata hivyo huduma hiyo imerudi katika hali ya
kawaida tokea Novemba 3 ambapo mafuta yameanza kuuzwa katika vituo vya mafuta
katika mji wa Ifakara na katika tarafa ya Kidatu huduma hiyo ilianza kupatikana
tokea Novemba 1 mwaka huu.
Mwandishi wa habari hii alishuhudia misururu
mirefu wa magari na pikipiki katika moja ya kituo cha mafuta Ifakara na wengi
wao walisema kuwa licha ya kujaza matenki ya vyombo vyao vya moto pia wataweka
akiba kwani hawawaamini tena wamiliki wa vituo vya mafuta na kuhofia kuwa
watawadanganya na kuwaeleza kuwa yamekwisha kumbe wamehifadhi kwenye matanki
yao.
No comments:
Post a Comment