HONGERA ULANGA COMMUNITY RESOURCE CENTRE

photos

Welcome to UCRC

About Me

Ulanga Community Resource Centre is a not-for-profit company limited by guarantee which was initiated with the aim of capacitating the resident peoples of Ulanga and Kilombero Districts and Tanzania in general to secure the right information and hold their duty bearers accountable in a bid to promote sustainable community development. UCRC as well aims at promoting educational activities in Ulanga District through facilitation of necessary educational resources in the area which include well equipped libraries and study centers. UCRC also works on land and natural resource rights for the marginalized rural people in Tanzania which also include sustainable use of such resources. It also provides legal aid and assistance to the poor, particularly women, children, the disabled and other disadvantaged groups in the society on different themes including land and gender.

Monday, November 12, 2012

Operesheni Okoa Bonde la Mto Kilombero yasababisha Kifo


Na Senior Libonge,Kilombero

WAKATI zoezi la kuondoa mifugo vamizi katika bonde tengefu la Kilombero likiendelea,zoezi hilo limeingia dosari baada ya mfugaji mmoja kudaiwa kuuawa na polisi wanaoendesha zoezi hilo .

Tukio la kuuawa kwa mfugaji huyo limetokea juzi katika kijiji cha Udagaji kata ya Chita wilayani Kilombero baada ya kundi la wafugaji kuwavamia askari na kuanza kuwapiga lengo lao ni kuwanyang’anya mifugo iliyokamatwa katika operesheni hiyo.

Akizungumza na gazeti hili diwani wa kata ya Chita Hassan Kidapa amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea juzi majira ya jioni katika kijiji hicho cha Udagaji baada ya kundi la wafugaji kuwavamia askari waliokamata kundi la ng’ombe wanaofikia 300 walioingia katika kijiji hicho kinyemela ili kuficha mifugo yao .

Kidapa amesema siku ya tukio baada ya askari kukamata mifugo hiyo iliyokuwa imefichwa katika moja ya msitu katika kijiji hicho waliikusanya katika kundi moja ili kuipeleka katika kambi maalum za kuhifadhi mifugo iliyokamatwa mara wakatokea jamii ya wafugaji wachache na kumpiga askari mmoja aliye na silaha kwa kutumia fimbo na alipoanguka chini waliamua kuondoka na kwenda kuita wenzao ili wachukue mifugo hiyo.

Amesema baada ya kupeana taarifa liliibuka kundi kubwa la wafugaji huku wakiwa na silaha za jadi lengo ni kupora ng’ombe hao waliokamatwa lakini walipofika katika uwanja wa mpira wa shule ya Udagaji walikutana na askari walioongezeka na walipewa tahadhari kwamba wasisogee eneo hilo lakini wafugaji hao walikaidi amri ya polisi na kusogelea mifugo na ndipo askari waliporusha risasi hewani ili kuwatawanya lakini waliendelea kukaidi.

Diwani huyo amesema kuwa baada ya kuona kuwa wafugaji hao wamekaidi amri halali ya polisi ya kutosogelea eneo la mifugo hiyo mmojawapo alipigwa risasi ya mguuni lakini bado walikaidi na kuendelea kuwasogelea askari na ndipo marehemu alipopigwa risasi ya kiunoni na kufariki dunia.

Hata hivyo diwani huyo amesema kuwa hadi jana jioni jina na mahali alipotokea marehemu bado havijajulikana kwani ni wafugaji wageni walioingia na kujificha katika kijiji hicho kwa lengo la kukimbia operesheni inayoendeshwa kwa nguvu ya kuondoa mifugo katika bonde lote la Kilombero na kijiji hicho hakina historia ya kuwepo kwa mifugo.

Kidapa amesema mifugo iliyokamatwa imepelekwa katika kambi maalum ya kuhifadhi mifugo iliyopo Mngeta na hivi sasa katika kata ya Chita hali sio shwari kwani jamii ya wafugaji wanaendelea kuwatisha viongozi akiwemo afisa mtendaji wa kata kwa madai kuwa ndio waliosababisha mwenzao kuuawa.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na yeye yupo katika operesheni hiyo akifuatilia zoezi linavyoendelea na kusema kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakaidi kutekeleza maagizo ya askari punde wanapotakiwa kufanya hivyo.

Shilogile amewataka wafugaji na wananchi wote kiujumla katika operesheni hiyo kutii sheria punde wanapoagizwa na kueleza kuwa wao kama askari toka ianze operesheni hiyo wanaiendesha kiustaarabu ila kuna watu wachache wanaotaka kulipaka matope jeshi hilo kwa kukaidi amri halali za kipolisi.

No comments:

Post a Comment