Na Senior Libonge,Kilombero
JUMLA ya zana za uvuvi haramu yakiwemo makokoro 35 na nyavu ndogo 4
vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 28.6 zimekamatwa katika doria
zilizofanyika katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2012 katika mamlaka ya mji
mdogo wa Ifakara.
Kwa mujibu wa afisa mtendaji wa
mamlaka ya mji mdogo wa Ifakara Mercy Minja amesema mpaka sasa kesi
zilizopelekwa mahakamani ni tano ambazo ni za kukamatwa na kokoro,kutishia kwa
njia ya simu baada ya kukamatwa,kumiliki kokoro,kumiliki kokoro na kujeruhi kwa
panga baada ya kukamatwa.
Mercy amesema lakini cha kushangaza
hakuna mtuhumiwa aliyefungwa hadi sasa licha ya serikali kupitia mkuu wa mkoa
wa Morogoro Joel Bendera wakati akifungua miezi ya karibuni kuagiza jeshi la
polisi na mahakama kutowachelewesha kuwahukumu wale wote watakaopatikana na
hatia ya uvuvi haramu katika mto Kilombero.
Hata hivyo wajumbe wa baraza la
mamlaka ya mji mdogo wameiomba halmashauri ya wilaya kusimamia kwa umakini
zoezi la doria kwa kushirikiana nao na hatimaye kuhakikisha vyombo vya sheria
vinawahukumu haraka iwezekanavyo watuhumiwa ili kuwapa moyo wale wote
wanaoendeleza doria katika mto huo.
Aidha mtendaji huyo wa mamlaka ya
mji mdogo alizungumzia suala la ujenzi holela katika maeneo mbalimbali ya
mamlaka ya mji mdogo Ifakara na kusema kuwa kumekuwepo na uvmizi wa ujenzi wa
nyumba za makazi au za biashara katika maeneo hasa ya hifadhi ya barabara.
Amesema ujenzi huo unasababisha
kushindikana kuwepo miundombinu ambayo inatakiwa kuwekwa pembezoni mwa barabara
na kuitaja kuwa ni mifereji ya maji taka,upitishaji wa mkongo wa mawasiliano wa
Taifa na nguzo za umeme.
Mercy amesema pia kumekuwepo na
ubadilishaji wa matumizi ya ardhi bila ya kuwa na kibali cha kubadili matumizi
ya ardhi hiyo kwa mfano kupewa eneo kwa ajili ya kujenga nyumba ya makazi
lakini mtu anabadilisha na kujenga nyumba ya kulala wageni ama kiwanda bila
kuwasiliana na mamlaka husika yenye jukumu hilo.
Amewaomba wajumbe wa baraza la
mamlaka ya mji mdogo kulisimamia na kuzuia watu kujichukulia sheria mkononi
mwao kwa kuwazuia na kuwaelekeza nini cha kufanya ili waweze kuepuka kuendelea
kubomolewa nyumba zao walizojenga bila kufuata kanuni,sheria na taratibu za
ujenzi katika mamlaka ya mji mdogo.
No comments:
Post a Comment