WAKULIMA Wilayani Kilombero wameshauriwa kufuata kanuni Bora za Kilimo wanazokuwa wanazipata kutoka kwa Maafisa Ugani ili kuweza kuzalisha mazao yao kwa Tija.
Bi Hawa Ndapanya,Mtaalamu wa Kilimo Kitengo cha Huduma za Ugani upande wa Shamba Darasa Wilayani Kilombero amesema katika kuzalisha mazao bora mkulima lazima azingatie kulima kwa wakati,kuchagua Mbegu bora, kupanda kwa wakati na kuwa na matumizi sahihi ya pembejeo ndipo mavuno bora yawezekana.
Amesema kuwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo kwa wakati na msimu ukiwa mzuri kwa wakulima wa Mpunga wanaotumia Mbegu ya Salo au TXD 306 waweza kupata Magunia 35 kwa Hekari moja ya zao hilo.
Wakulima wakizingatia kanuni hizo na kuacha nafasi kati ya mimea kwa senimita 20 kwa 20 wilaya ya Kilombero itakuwa imefanikiwa kwa asilimia kubwa kutekeleza maagizo ya kilimo kwanza na dhamana kubwa ya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa.
Kwa kuzingatia kanuni zote za kilimo bora uzalishaji wa mazao Utaongezeka na kuweza kujitosheleza kwa Chakula na ziada kuweza kukidhi mahitaji mengine ya Wakulima.
Wakati huo huo,Bi Hawa amewashauri Wakulima kuendelea Kulima mazao yanayostahimili ukame kwani nayo ni mkombozi pindi hali ya Hewa inapokuwa si nzuri.
Amesema kwa Mkulima wa kawaida anapolima Hekari 3 anashauriwa kuwa na hekari moja ya zao la Biashara na Hekari mbili za Mazao ya Chakula zinazoweza kuhimili ukame.
Bi Hawa Ndapanya, ambaye pia ni Mwezeshaji Mkuu katika Mafunzo kwa Wataalamu wa Kilimo kuhusu dhana ya Shamba Darasa alikuwa akitoa mada ya Dhana ya Shamba Darasa kwa Washiriki wa Mafunzo ya Siku Nne kwa Wataalamu hao, mafunzo yanayosimamiwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na Uhifadhi wa Mazingira katika Bonde la Kilombero (KIVEDO) chini ya Ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Plan International.
No comments:
Post a Comment