Na Senior Libonge,Ulanga
WANANCHI wa tarafa ya Lupiro wilayani Ulanga wamesema kuwa tabia ya watu kunywa pombe kupita kiasi ndiyo sababu kubwa ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi katika tarafa hiyo.
Kauli hiyo wameitoa hivi karibuni wakati wa tamasha la Ukimwi lililoandaliwa na kampuni ya Mitiki ya bonde la Kilombero(KVTC) lililofanyika katika kata ya Mavimba wilayani humo ambapo imebainika kuwa wapo wagonjwa 462 wanaoishi na virusi vya ukimwi na kupata huduma katika kituo cha Afya Lupiro.
Wamesema kuwa wengi wa wananchi katika tarafa hiyo wanakunywa sana pombe za kienyeji na wakishalewa huwa wanafanya matendo yanayochangia maambukizi ya ukimwi bila kinga ya aina yeyote na hali ndiyo uongeza maambukizi.
Licha ya ulevi pia wamesema kuwa hali ya uchumi kwa wananchi ,kuingia kwa kasi kwa wingi kwa wageni na mila za kurithishana wanawake nazo uchangia kuenea kwa maambukizi hayo.
Akitoa taarifa ya maambukizi katika tarafa hiyo,afisa tabibu wa kitengo cha kuhudumia wagonjwa wa ukimwi katika kituo cha afya Lupiro Wadugu Wadugu amesema wapo wagonjwa 462 wanaohudumiwa katika kituo hicho na wanatoka sehemu mbalimbali ndani ya tarafa hiyo.
Wadugu amebainisha kuwa kata ya Lupiro inaongoza kwa kuwa na watu 124 wanaoishi na virusi vya ukimwi,kata ya Iragua watu 115,kata ya Mavimba watu 110,kata ya Kichangani watu 51 na kata ya Minepa ina watu 62.
Amesema kati ya wagonjwa hao wanawake ni 311,wanaume 125 na watoto wa kike 12 huku watoto wa kiume ni 14 na kwa hivi sasa wanaendelea kupata huduma endelevu katika kituo hicho cha Afya hivyo kuomba watu wengine kujitokeza na kupima afya zao kisha kupata matibabu kwa wakati.
Hata hivyo Wadugu amesema kwa hivi sasa tarafa hiyo imeandaa mikakati ili kupinguza maambukizi katika tarafa hiyo kwa kutoa elimu zaidi kuhusu athari za ugonjwa huo na hatua gain zinazotakiwa kuchukuliwa punde mtu anapopata ugonjwa huo.
Kwa upande wake meneja jamii wa KVTC Kennedy Haule amesema tamasha hilo ni la pili kufanyika toka waanzishe kiwanda cha mbao katika tarafa hiyo na hiyo yote ni kutokana na tathmini ya mazingira hasa baada ya kuonekana kwamba kutakuwa na ongezeko la watu hivyo kuweka mkakati wa kudhibiti maambukizi ya ukimwi.
Haule amesema tamasha limekuwa na mafanikio mwaka hadi mwaka hasa baada ya watu kujitokeza kwa wingi na hiyo inatokana na kuongezeka kwa michezo ikiwemo soka,netball,draft na bao na washindi wa michezo hiyo licha ya kupata zawadi pia wamekuwa mabalozi wa kampuni katika kuzuia maambukizi kwa jamii inayozunguka kiwanda.
Aidha Haule amesema mkakati wa kampuni ya KVTC ni kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja kati ya jamii na kampuni katika kuhakikisha wananchi na sehemu za kazi kutokuwepo maambukizi mapya ya ukimwi.
No comments:
Post a Comment