Na Senior Libonge,Ulanga
WANANCHI wilayani Ulanga wamedai kuwa licha pembejeo za ruzuku za kilimo kuchelewa kufika kwa wakati pia pembejeo hizo zimekuwa bei ghali na hali hiyo umfanya mkulima wa chini kushindwa kuipata na kutimiza malengo yake katika kilimo..
Wakizungumza katika mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma sekta ya kilimo wilaya ya Ulanga yanayotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya kikundi cha wanawake wa St.Maria Magdalena ya Ifakara wananchi hao wamesema kuwa serikali inatakiwa kushirikisha viongozi wa vitongoji katika ugawaji na sio kamati ya vocha.
Wamesema kuwa kutokana na kuchelewa kufika kwa wakati kwa mbolea hizo imepelekea wananchi kulima bila kutumia mbolea na punde mbolea ikifika ulundikana katika ofisi za serikali kwani zinakuwa hazina kazi tena.
Julius Mwere mkazi wa Kivukoni amesema kuwa gharama ya mfuko mmoja wa mbolea ya minjingu uuziwa mkulima hadi kiasi cha shilingi 80,000 na hali hiyom umfanya mkulima kushindwa kununua mbolea hiyo kutokana na gharama kuwa kubwa.
Naye Hassan Mkamla mkazi wa Lupiro ambaye ni mlemvu amesema kuwa hata wao hawapatiwi mbolea hizo na wakifuatilia kwa watendaji wa vijiji uambiwa kuwa wakaonana na wakala wao na hata wakienda huko huwa wanazungushwa na hakuna wanachopata.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji cha Kivukoni Josephat Masanyoni alikiri kweli kuwa malalamiko ya wananchi hao ni ya msingi na kuelezea suala la mbolea kuwa kweli ilichelewa kufika na licha ya kufika baadhi ya wananchi walikosa na tatizo kubwa ni uchangiaji wa fedha toka kwa wananchi.
Masanyoni alisema uchelewaji wa mbolea hizo umepelekea mifuko kadhaa ya mbolea kulundikana katika ofisi yake baada ya wakulima kukataa kuipokea kwa madai kuwa imefika muda ambao sio wa kwake kwani wakulima walikuwa wamekwisha panda na wanasubiria kuvuna.
Mratibu wa mafunzo hayo Bi Christina Kulunge amesema mafunzo yameendeshwa katika kata za Kivukoni,Minepa na Lupiro huku lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wananchi kuhusu ufuatiliaji wa pembejeo za ruzuku katika sekta ya kilimo na mradi huo ni wa mwaka mmoja na una gharama ya shilingi milioni 43 ambazo zimefadhiliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya The Foundation for civil society.
No comments:
Post a Comment