Na Senior Libonge,Kilombero
MKUU wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala amesema kuwa atamlipia gharama ya masomo na malazi kwa muhula wa kwanza mwanafunzi yeyote atakaemaliza kidato cha nne mwaka huu na kufaulu kwa kupata daraja la 2 ama 3 kutoka katika shule ya sekondari ya kata ya Uchindile.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo ya sekondari ambayo ipo pembezoni mwa wilaya ya Kilombero ambayo kwa kiasi kikubwa ukimbiwa na walimu pamoja na wanafunzi kutokana umbali wake.
Masala ameamua kujitolea kumsaidia mwanafunzi yeyote atakaefaulu baada ya kusomewa risala ya shule hiyo na kuelezwa kuwa kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana ni mwanafunzi mmoja tu ndiye aliyefaulu kwa kupata daraja la 4.
Katika kuwatia moyo wanafunzi watakaomaliza mwaka huu Masala amesema yeyote atakaepata daraja hilo yupo tayari kumlipia ada na malazi kwa muhula wa kwanza ili mradi mwanafunzi huyo amletee barua ya mahitaji ya shule(Join Instruction).
Amesema ameamua kutoa ofa kwa shule hiyo kutokana na mazingira ya shule yenyewe hasa baada ya kuona wanafunzi wake wakijitahidi kusoma licha ya mazingira yake kuwa pembezoni mwa kata hata wilaya na pia wengi wa wanafunzi wakiwa wametoka nje ya kata hiyo.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewataka wanafunzi wengine kusoma kwa bidii na kuheshimu walimu wao huku pia akiwataka walimu kuwafundisha wanafunzi hao kwa bidii licha ya kuwa na changamoto mbalimbali ambazo ameahidi kuzishughulikia baadhi yake.
Awali akisoma risala ya shule hiyo mkuu wa shule Januari Mkoba amesema shule iliponzishwa ilikuwa na wanafunzi 59 ila sasa ina wanafunzi 120 na walimu 8 huku wanafunzi wengi wakitoka katika tarafa ya Ifakara baada ya shule za msingi katika kata hiyo kushindwa kufaulisha wanafunzi wake.
Mkoba amesema changamoto kubwa ni wakati wa likizo wanafunzi wengi kuchelewa kurudi shule kutokana na umbali wanapotoka huku pia ushindwa kukutana na wazazi kutokana na tatizo hilohilo la umbali na hali hiyo upelekea wanafunzi kushindwa kusoma masomo yote kwa wakati unaotakiwa.
Pia mwalimu huyo alisema shule hiyo haina mwalimu wa masomo ya hisabati na fizikia na hali hiyo upelekea wanafunzi kutaka kuhama kwa kukosa masomo hayo na pia shule kukosa usafiri ambao ungesaidia walimu kurahisisha kudurufu hata karatasi za masomo mbalimbali.
Akijibu hoja za jumla,Masala alisema atakutana na mkurugenzi mtendaji wa wilaya ili kufanikisha shule hiyo kuwa na walimu wa masomo ya fizikia na hisabati na pia atajitahidi kupigania ili shule hiyo ipate pikipiki moja ambayo itawasaidia walimu waliopo kurahisisha shughuli mbalimbali ukizingatia lengo la halmashauri ni kusaidia walimu wote waliopo pembezoni mwa wilaya.