Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana Hassani Masala amewataka wakazi wa Kilombero kuacha kutoa taarifa zisizo na ukweli kuhusu uhamaji wa maeneo Tengefu ya Bonde la Kilombero na atakaye kamatwa anatoa taarifa za uongo kuhusiana na kuhama kwa wavamizi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Bwana Masala amesema hayo wakati akifunga Mdahalo wakukuza uwajibikaji wa Viongozi na Wawakilishi wa Wananchi kwa Jamii ulioandaliwa na Mtandao wa Azaki Mkoa wa Morogoro {UNGO}kwa kushirikiana na The Foundation for Civil Society uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Vijana(John Paul II ) uliopo mjini Ifakara.
Ametoa tahadhari hiyo kwa baadhi ya wananchi na viongozi wanaowapotosha wananchi juu ya zoezi la kuhama kwa wavamizi wa maeneo ya hifadhi na kuondolewa kwa mifugo vamizi.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilombero amewapongeza UNGO kwa kutoa Elimu kupitia mdahalo huo na amewaomba kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kuleta maendeleo na kutoa Elimu kuhusu utawala bora kwa viongozi na wananchi.
Wakitoa mada ya utawala wa uwajibikaji katika Usimamizi na Menejimenti ya Rasilimali katika sekta ya Maliasili Bwana Masanja Joram na Christer Njovu wamesema kuwa katika utawala na uwajibikaji kiongozi anatakiwa kuwa mvumulivu wakati watu wanatoa maoni katika mkutano au vikao na pia anatakiwa kukosoa au kukosolewa bila ya kuoneana aibu. Wawezeshaji hao pia wamewataka wananchi kujihusisha kusimamia maeneo ya Uvuvi ili kuzuia uvuvi haramu katika sekta ya maliasili.
No comments:
Post a Comment