Na Senior Libonge,Ulanga
WAKAZI wa kijiji cha Kivukoni wilayani Ulanga wameiomba halmashauri ya wilaya kukipa upendeleo kijiji hicho kwa kuwapatia asilimia ya mapato ya kizuizi cha wilaya kilichopo katika kijiji chao ili kufanyia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Rai hiyo wameitoa juzi wakati wa mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma sekta ya kilimo wilaya ya Ulanga yanayotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya kikundi cha wanawake wa St.Maria Magdalena ya mjini Ifakara.
Wananchi hao wamesema kuwa hivi sasa kijiji hicho kinapata asilimia chache ya mapato licha ya kizuizi hicho kuwepo kwenye kijiji chao na wao kuendelea kuwa maskini huku wakishindwa kujiendesha ikiwemo wenyeviti wa vitongoji kukosa fedha za shajala.
Wamesema kwa hivi sasa hawaoni faida ya kuwepo kizuizi hicho katika kijiji chao kwani wamekuwa wakijichangisha wao wenyewe michango mbalimbali ya maendeleo bila kupata msaada wa kutosha katika halmashauri ukizingatia kuwa sehemu nyingine zenye kitegauchumi cha wilaya kijiji husika upata mafanikio ya mradi uliopo.
Aidha wananchi hao wamewaomba wabunge wa majimbo yote ya Ulanga mashariki na magharibi kufanya mikutano kwenye kijiji chao kwani wao ukipita tu kijiji hicho punde waingiapo katika ziara zao kwenye majimbo yao ukizingatia kuwa kijiji hicho ndiyo mlango wa wilaya ya Ulanga.
Kuhusu pembejeo za ruzuku za kilimo wananchi hao wamesema kuwa licha ya kuchelewa kufika kwa wakati pia pembejeo hizo zimekuwa bei ghali na hali hiyo umfanya mkulima wa chini kushindwa kuipata na kutimiza malengo yake katika kilimo..
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw Josephat Masanyoni ili kupata ukweli kuhusu malalamiko ya wananchi ambapo alikiri kweli kuwa malalamiko ya wananchi hao ni ya msingi na kuelezea suala la mbolea kuwa kweli ilichelewa kufika na licha ya kufika baadhi ya wananchi walikosa na tatizo kubwa ni uchangiaji wa fedha toka kwa wananchi.
Masanyoni akielezea suala la mapato ya kizuizi alisema kweli hawana asilimia wanayopata kutoka kwenye kizuizi hicho licha ya wao kupeleka malalamiko kwa viongozi wa wilaya na hata wananchi kutoa malalamiko yao punde wanapokuja viongozi mbalimbali.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Christina Kulunge amesema mafunzo hayo ni ya siku 5 yanafanyika katika kata za Kivukoni,Minepa na Lupiro na lengo lake ni kuwajengea uwezo wananchi kuhusu ufuatiliaji wa pembejeo za ruzuku katika sekta ya kilimo.
Amesema pia wananchi wanatakiwa kuwa na ufahamu wa uchangiaji wa serikali katika mbolea za ruzuku na maadili ya utawala bora.
Christina amesema mradi huo ni wa mwaka mmoja na una gharama ya shilingi milioni 43 ambazo zimefadhiliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya The Foundation for civil society
No comments:
Post a Comment