Na Senior Libonge,Ulanga
KATIKA kuonyesha kuwa amekerwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kwa ukataji na uchomaji ovyo misitu ya asili mwananchi wa kijji cha kituti tarafa ya Ruaha wilayani Ulanga,Metrucy Albert,ameangua kilio mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Menejamenti ya Utumishi wa Umma,Celina Kombani wakati akimuelezea kukithiri kwa vitendo hivyo katika kijiji chao .
Albert aliangua kilio hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho baada ya kumalizika kwa hotuba Waziri Kombani ambaye ni mbunge wa jimbo la Ulanga mashariki (CCM) baadaye na kuruhusu wananchi wa kijiji hicho kutoa kero zao mbalimbali zinazowakabili .
Baada ya kupewa nafasi hiyo kutoa kero hiyo,Albert alieleza kuwa hivi sasa kijiji hicho kimevamiwa na maharamia mbalimbali ambao wamekuwa wakikata misitu na kuchoma moto ovyo kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya kijiji hali ambayo imekuwa ikitishi ukame na kuathiri upatikanaji wa mvua.
Alisema licha ya jitihada mbalimbali wanazofanya za kuhakikisha wanadhibiti uharibifu wa maliasili hizo ikiwemo uvunaji wa mbao na wanyama wanaotoka pembezoni ya mbuga ya Serue zimeshindikana kutokana na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mahalamia hao kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya kijiji hicho.
Naye Lucas Talimo,alisema kuwa maliasili hizo ambazo ni pamoja na madini wao kama wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakishindwa kufaidika nazo licha ya kuzilinda na badala yake wageni ndio wamekuwa wakijinufaisha nazo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa vijiji hivyo.
Aliomba Serikali kuingilia kati vinginevyo malisili hizo zinaweza kutoweka wakati wowote kutokana na vitendo vinavyofanywa na mahalamia hao katika kata hiyo .
Akizungumzia hilo,Waziri Kombani aliagiza Uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Ulanga kupitia ofisi ya Maliasili wilaya kulishughulikia suala hilo mara moja ili kuzuia kutoweka kwa maliasili hizo zinazockuliwa kinyemela na mahalamia hao.
No comments:
Post a Comment