Na Senior Libonge, Kilombero
WANANCHI wa kata za Chita, Mngeta na Mlimba wilayani hapa wametaka serikali itenge bajeti ili kuwalipa mishahara na marupurupu mengine wenyeviti wa vitongoji na vijiji kutokana na kazi kubwa wanazozifanya badala ya kujitolea.
Wamesema kuwa wenyeviti hao ni watendaji muhimu wa serikali katika ngazi za vitongoji na vijiji na hivyo kufanya kazi kwa kujitolea ni kutowatendea haki na kunawakatisha tama.
Mmoja wa wananchi hao, Cosmas Kibiki, amesema kuwa viongozi wote wanaochaguliwa na wananchi kuanzia rais, mbunge na diwani wanalipwa mishahara, posho na marupurupu mengine lakini wenyeviti wa vitongoji na vijiji wanasahaulika.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Mlimba A, Mussa Gili, amesema kuwa kuwalipa mishahara na marupurupu viongozi hao kutapunguza wimbi la rushwa katika ngazi hizo za utawala kutokana na ujira watakao upata na ambao utaweza kuongeza ari ya utendaji wao wa kazi.
Ameongeza kuwa baadhi ya wenyeviti wamekuwa wakishirikiana na watendaji wao kuhujumu mali za vijiji kama vile ardhi kutokana na kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato na kwamba ikiwa serikali ilikubali watendaji wa vijiji walipwe ingefanya vivyo hivyo kwa wenyeviti wao.
Hata hivyo, Geofrey Ngiyi, akichangia maoni yake katika katiba amesema kuwa mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata yatazamwe upya kwa vile yamekuwa ndiyo msingi wa migogoro ya ardhi katika vijiji.
Amesema kuwa hali hiyo inatokana na wengi wa wajumbe wa mabaraza hayo kutokuwa na elimu ya kutosha ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ha hivyo kushauri kuwa katika ibainishe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo wawe wasomi wenye utaalam wa kutatua migogoro hiyo.
No comments:
Post a Comment