Na Senior Libonge,Kilombero
MAKUNDI makubwa ya mifugo yameanza kuondoka katika bonde la Mto Kilombero wakitekeleza agizo la serikali la kutaka mifugo yote iliyovamia katika bonde hilo kutolewa kwa hiari kabla ya nguvu za dola kuanza kutumika hapo Septemba 7 mwaka huu.
Nimeshuhudia malori makubwa yakiwa yamebeba mifugo huyo katika mji wa Ifakara tayari kwa safari ya kusafirisha mifugo hiyo na kuipeleka kusini mwa Tanzania kwenye mkoa wa Lindi ambapo serikali imetenga eneo maalum la kuishi mifugo.
Juzi viongozi wa wilaya zote mbili za Kilombero na Ulanga walikuwepo mjini Ifakara tayari kwa kuruka na ndege ndogo iliyoletwa na serikali kwa ajili ya kukagua mifugo ama wakulima waliobaki katika maeneo yaliyopigwa marufuku kuwepo na kweli zoezi hilo lilifanyika kwa umakini.
Katika ziara hiyo timu hiyo iliyoongozwa na mkuu wa wilaya ya Kilombero Hassan Masala na yule wa Ulanga Francis Miti walitembelea bonde lote la Kilombero ili kujionea uharibifu uliofanyika na kwa kiasi kikubwa walibaini kuwa mifugo mingi imeondoka katika bonde hili isipokuwa kwa wafugaji wachache ambao wamejifanya kuificha mifugo yao katika baadhi ya misitu ndani ya bonde hilo.
Baada ya kumaliza kuzungukia bonde hilo wakuu hao wa wilaya walisema kuwa operesheni ya kuwaondoa wafugaji hao imekwisha anza na zoezi linalofanyika hivi sasa ni viongozi wa vijiji na vitongoji kuwahamasisha wafugaji wote waliokuwepo maeneo hayo kuondoa haraka mifugo yao na kubakia ile mifugo halali inayotakiwa kubaki maeneo hayo.
Mifugo halali ni ile iliyowekwa alama na ambayo imekubalika na wananchi wa kijiji husika kuwepo maeneo hayo hasa kwa kuzingatia ukubwa wa eneo husika na mahitaji halisia ikiwemo ya ng’ombe wa kilimo(maksai).
Kwa sasa mifugo mingi imebainika ipo pembezoni mwa milima ya Udzungwa katika tarafa ya Mlimba ambapo haijajulikana kuwa wafugaji hao wameificha mifugo yao maeneo hayo ama wapo njiani kuisafirisha kuipeleka mikoa ya Iringa na Mbeya.
Hata hivyo wafugaji hao wavamizi sambamba na wakulima walioingia katika maeneo ya hifadhi wamepewa tahadhari kuwa kauli ya serikali ipo palepale ya kutaka wote watoke maeneo hayo ukizingatia kuwa serikali haitaki kutumia nguvu kuwaondoa ukizingatia kuwa ni wananchi halali wan chi hiyo.
Ila taarifa imesema kuwa serikali haitashindwa kutumia nguvu kuwaondoa wavamizi hao kama wakiendelea kukaidi agizo la kutaka kutoka eneo hilo ukizingatia mpango wa serikali hivi sasa ni kuliona bonde la Kilombero likirudi katika hali yake ya zamani ya kuwa na ardhioevu kwa ajili ya kilimo na hifadhi tofauti na hivi sasa ambapo asilimia kubwa ya bonde hilo limeharibika kutokana na uvamizi wa mifugo na wakulima.
No comments:
Post a Comment