Na Senior Libonge,Kilombero
MASHINDANO ya mchezo wa soka na netball ya kuibua vipaji ya Mbunge wa jimbo la Ulanga mashariki Celina Kombani yameanza kurindima katika tarafa mbili za mwaya na Vigoi katika jimbo la hilo mkoani Morogoro.
Katika michezo ya ufunguzi timu ya soka ya Usalama imeweza kuifunga timu ya UDC kwa mabao 5-1 katika kituo cha Vigoi wakati kituo cha Mwaya Moro stars iliweza kuifunga Cameroon ya Iputi kwa mabao 3-0.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo katibu wa chama cha soka wilayani Ulanga Joseph Mkude ambaye ni mratibu wa mashindano hayo alisema kuwa jumla ya timu 52 zimejitokeza kushiriki michuano hiyo ambapo zitachujwa na kubaki timu nane zitakazocheza hatua ya robo fainali.
Alifafanua kuwa katika kituo cha mwaya timu 36 zimejitokeza kushiriki wakati kituo cha vigoi timu 16 zinashiriki mashindano hayo.
Aidha alisema jumla ya timu nane za mpira wa pete zitashiriki michuano hiyo kwa kituo cha vigoi na nne kwa kituo cha mwaya.
Akizungumzia michuano hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Celina Kombani amesema anaamini kupitia michuano hiyo watapatikana wachezaji mahiri ambao wataweza kupiga hatua ya michezo na kufikia katika ngazi ya kitaifa.
Alisema anajivunia michezo hiyo kutoa wachezaji ambao wameweza kucheza mashindano mbalimbali akitolea mfano mchezaji Godfrey Albino ambae alianzia katika michezo hiyo na sasa ameweza kuwakilisha nchi katika michezo ya umoja wa shule za sekondari kwa nchi za afrika mashariki.
Mashindano ya Celina Kombani mwaka huu yamefadhiliwa na NSSF, Quality group na DDC Kariakoo ambapo mshindi anatarajia kujinyakulia zawadi ya kikombe,seti ya jezi,fedha taslimu na kutembelea katika jimbo jirani la Ulanga magharibi katika sehemu ya kuhamasisha michezo.
No comments:
Post a Comment