Na Senior Libonge,Kilombero
VIJIJI 6 wilayani Kilombero vimekabidhiwa vifaa vya uendeshaji wa vitalu vya miti na bustani ya mbogamboga vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 6 kutoka asasi inayojishughulisha na uhifadhi wa mazingira na maendeleo katika bonde la Kilombero(KIVEDO).
Akikabidhi vifaa hivyo katibu mtendaji wa KIVEDO Hamza Kaposa amevitaja vijiji vilivyokabidhiwa vifaa kuwa ni Namwawala,Mofu,Kisegese,Mbingu,Mkangawalo na Udagaji lengo ni kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.
Kaposa amesema ili kufanikisha lengo hilo,KIVEDO kwa kushirikiana na vijiji hivyo vya mradi wataanzisha bustani za miti sita yaani kila kijiji kuwa na bustani moja kwa kuotesha,kukuza na upandaji miti na pia kupitia ufadhili wa shirika la Plan International watatoa vifaa kwa ajili ya uendeshaji wa bustani ya miti katika vijiji.
Katibu huyo amebainisha kuwa kila kijiji kinachukua jukumu la kuhakikisha kuwa vifaa vya mradi wa kusimamia na kuendeleza bustani ya miti vinatumika kwa lengo na madhumuni ya kutekeleza kazi za mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na siyo vinginevyo.
Amesema kuwa sababu ya kuchagua vijiji hivyo ni kutokana na vijiji hivyo hapo nyuma kufanyiwa utafiti na kugundulika vimeathirika na mabadiliko ya tabia nchi tokana na wananchi kutegemea kilimo na uvuvi katika maeneo hayo na pia wameona kuwa hatua zinazochukuliwa katika vijiji hivyo vitaleta mafanikio ya haraka tofauti na maeneo mengine.
Kaposa amesema ili kijiji kikabidhiwe vifaa vya kuendesha bustani ya miti kitalazimika kuwasilisha majina ya wanakijiji waliojitolea kuitunza na kuendesha bustani ya miti ili miti itakayozalishwa igawiwe kwa wanakijiji kwa ajili ya kuipanda mashambani,maeneo ya makazi na kwenye vyanzo vya maji na kingo za mito.
Aidha kijiji kinatakiwa kutenga eneo la ardhi kwa ajili ya kuanzisha eneo la kitalu cha bustani ya miti,iwe kwenye eneo la kijiji,taasisi ya serikali au mtu binafsi na gharama za utunzaji wa kitalu cha miti itakuwa ni jukumu la kijiji kwa kushirikiana na watu watakaokuwa tayari kujitolea kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Vifaa vilivyokabidhiwa vijiji hivyo ni pamoja na Matoroli,makoleo,viriba vya plastiki,visu,sprayer,ndoo,majembe,reki,watering cane,mapanga,mafyekeo,mifuko ya mbolea ya kukuzia na garden foxes.
Shirika la KIVEDO linatekeleza mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa muda wa miaka mine kwa ufadhili wa shirika la Plan International na pamoja na mambo mengine mradi unajikita katika shughuli za uhifadhi wa mazingira na maliasili na kuboresha upatikanaji wa mazao na masoko yake.
No comments:
Post a Comment