Na Senior Libonge,Kilombero
MKUU wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera amesema kuwa hataki kusikia tena katika mkoa huo wilaya yoyote inalalamikiwa na mkaguzi wa mahesabu kwa kupata hati chafu na ikifanya hivyo uongozi wote wa wilaya utawajibika.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na madiwani na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero na kusema kuwa kwa kuanzia sasa atafanya uchunguzi kila mwezi ili kugundua halmashauri ipi inaurudisha nyuma mkoa wa Morogoro katika ukusanyaji wa mapato.
Bendera ameuagiza uongozi wa wilaya zote kwa kushirikiana na madiwani kuhakikisha kuwa watendaji wote wanaosababisha uzembe wa kula fedha za halmashauri wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani.
“Kuna watendaji wanafanya mambo watakavyo kwa kula fedha za halmashauri na kumaliza hadi mbegu sasa nyinyi viongozi wa wilaya mna majukumu ya kuwashughulikia na mkishindwa mniambie mimi niwashughulikie lengo ni kuona halmashauri zote zinapata hati safi,”alisema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema halmashauri nyingi hazisimamii miradi ya maendeleo ipasavyo kwani miradi mingi haiendani na thamani halisi ya fedha kwa watendaji kufanya mambo wafanyavyo huku wakiachwa bila kuchukuliwa hatua na hatimaye wananchi kuichukia serikali kwa upuuzi wa watu wachache.
Amezisifu wilaya mbili za Kilombero na Ulanga kwa kufanya vizuri katika mahesabu ya mkaguzi kwa kupata hati safi zenye mashaka kwa miaka miwili mfululizo na kuchukizwa na wilaya za Kilosa na Moro vijijini kwa kutafuna fedha za umma na hatimaye kupata hati chafu.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa ametaja changamoto zinazosababisha kusuasua kwa miradi kuwa ni wananchi kutoshirikishwa ipasavyo katika miradi huku baadhi ya wanasiasa kushawishi wananchi kutochangia miradi na uwajibikaji mdogo katika ngazi za usimamizi wa miradi.
Ameziagiza halmashauri zote kujipanga na kuzingatia hoja za mkaguzi na maagizo ya Tamisemi,taarifa za mradi zijadiliwe katika menejimenti na madiwani na kutoa elimu na uhamasishaji kwa wananchi punde unapotokea mradi.
Aidha Bendera amezitaka halmashauri zihakikishe zinaheshimu maamuzi ya vikao vyao na wasiwe vigeugeu na wananchi wahamasishwe ili waweze kuchagia huku pia serikali za wilaya.
No comments:
Post a Comment